Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Hayo yameelezwa leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutokuwajibishwa kwa Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari.
Sungura amesema taarifa zilizokusanywa na wadau wa habari zinaonyesha kuwa polisi wanatajwa mara kwa mara katika malalamiko ya kunyanyaswa kwa wanahabari, akieleza kuwa hali hiyo inahusishwa kwa kiasi kikubwa na majukumu ya jeshi hilo ya kukamata watu.
“Katika taarifa zetu inaonekana polisi ndiyo kundi linaloongoza kunyanyasa waandishi wa habari. Kwa sababu ya kazi yao ya kuwakamata watu, ndivyo wanavyofanya. Siyo waandishi wa habari tu, hata watu wengine wanakamatwa,” amesema.
Amesema kuna umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kisheria inayowalinda waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao ya kuhabarisha umma na kufichua masuala yenye maslahi kwa wananchi.
Sungura ameitaka Serikali kuhakikisha kuwa wanahabari wanapata ulinzi wa kutosha kisheria, akipendekeza nafasi ya uandishi wa habari itambuliwe kikatiba ili kuimarisha uhuru na usalama wa taaluma hiyo.
Amesema uandishi wa habari una jukumu muhimu katika kuisimamia Serikali na taasisi nyingine za umma, kwa kuwa unasaidia kufichua matatizo yanayohitaji hatua za mamlaka husika.
Akizungumzia changamoto za kisheria zinazoikabili sekta hiyo, Sungura amesema baadhi ya maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kuhusu vifungu vya Sheria ya Huduma za Habari bado hayajatekelezwa kikamilifu.
Amesema wadau waliwasilisha malalamiko kuhusu vifungu 21 vya sheria hiyo, lakini utekelezaji wake bado una changamoto.
Katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), Sungura, amesema tathmini ya MCT imebaini ukiukwaji wa haki za wanahabari 12 uliothibitishwa mwaka 2026, ikilinganishwa na matukio 51 mwaka 2025 na 33 mwaka 2024.
Amesema matukio hayo yanajumuisha kukamatwa kwa wanahabari, vitisho na vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa takwimu hizo zinahusu matukio yaliyothibitishwa na huenda zisiwe jumla ya matukio yote.
Kwa mujibu wa Sungura, Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 95 mwaka 2025 hadi nafasi ya 117 kati ya nchi 180 katika Fahirisi ya Uhuru wa Habari Duniani ya mwaka 2026 iliyotolewa na Reporters Without Borders.
Mkurugenzi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura.
UNESCO yaonya mauaji ya wanahabari kutowajibishwa
Wakati hali hiyo ikiendelea kujadiliwa nchini, ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusu usalama wa waandishi wa habari na kutokuwajibishwa kwa wahusika, iliyotolewa Oktoba 2026, inaonyesha kuwa asilimia 86 ya mauaji ya wanahabari duniani bado hayajapatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Kwa mujibu wa UNESCO, kiwango hicho kinamaanisha kuwa karibu mauaji tisa kati ya 10 ya wanahabari yanabaki bila wahusika kuwajibishwa kupitia mfumo wa mahakama.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa waandishi wa habari 189 waliuawa katika mashambulizi ya kikatili mwaka 2024 na 2025, ambapo asilimia 67 ya vifo hivyo vilitokea katika maeneo yenye migogoro.
Aidha, waandishi 50 waliuawa kwa kutumia ndege zisizo na rubani (drones) katika maeneo sita ya vita, jambo linaloonyesha namna teknolojia mpya inavyobadilisha aina ya vitisho vinavyowakabili wanahabari.
UNESCO imeeleza kuwa pamoja na kupungua kwa baadhi ya mauaji katika maeneo yasiyo na migogoro ya kivita, kutokuwajibishwa kwa wahusika bado ni changamoto kubwa inayochochea vitendo vya ukatili dhidi ya wanahabari.
Akizungumzia ripoti hiyo katika maadhimisho hayo, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Jean-Marc Pisani, amesema takribani mauaji tisa kati ya 10 ya wanahabari duniani bado hayajapatiwa ufumbuzi na wahusika kuwajibishwa.
Amesema tangu mwaka 2012, uhuru wa kujieleza umepungua duniani huku kiwango cha wanahabari wanaojidhibiti katika uandishi wao kikiongezeka kwa asilimia 13.
Ameeleza kuwa kujidhibiti huko ni moja ya madhara yasiyoonekana kwa urahisi ya kutokuwajibishwa, kwa kuwa mwandishi anaweza kuamua kutokuandika habari, kutokuuliza swali au kutofichua ukweli kwa hofu ya madhara yanayoweza kumkuta.
Pisani amesema vitisho dhidi ya wanahabari vimebadilika kutoka mashambulizi ya ana kwa ana na sasa vinajitokeza pia kupitia majukwaa ya kidijitali.
Ametoa mfano wa mwandishi wa habari mwanamke anayechapisha makala na kuanza kupokea ujumbe wa vitisho na matusi kupitia simu, akisema hali hiyo inaweza kumfanya ajiulize kama aendelee na kazi yake.
Amesema Tanzania pia inakabiliwa na changamoto za unyanyasaji wa mtandaoni, kuzuiliwa kwa wanahabari na kunyang'anywa vifaa vyao vya kazi, huku wanawake wakikabiliwa zaidi na vitisho vya kidijitali na ukosefu wa usalama kazini.
Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania, Anna Merrifield, amesema wanawake wanahabari wanakabiliwa kwa kiwango kikubwa na mashambulizi ya mtandaoni yanayolenga jinsia zao badala ya kujibu hoja wanazoziripoti.
Amesema mashambulizi hayo yanaweza kuongezeka na kugeuka kuwa vitisho au ukatili wa kimwili, hivyo kuitaka jamii, hususan wanaume wanaofanya kazi katika sekta ya habari, kushirikiana na wanawake wanahabari kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Idara ya Habari Maelezo, Evody Kyando, amesema Serikali hushirikiana na Jeshi la Polisi kufuatilia taarifa za matatizo yanayowakabili waandishi wa habari.
Kyando amesema ofisi hiyo inapopokea taarifa kuhusu mwandishi anayekabiliwa na changamoto, huwasiliana na taasisi husika, wakiwemo wasemaji wa polisi, ili kusaidia kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, amesema wanahabari wanapaswa kuzingatia sheria wanapotekeleza majukumu yao, huku akieleza kuwa sheria zinazoonekana kuwa na mapungufu zinaweza kujadiliwa upya.
Wadau hao wamezitaka mamlaka husika kuchunguza kwa haraka na bila upendeleo vitisho na mashambulizi dhidi ya wanahabari, kupitia mifumo ya kuzuia mashambulizi, kuwalinda walio hatarini na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya sheria.
Pia, wametaka kuimarishwa kwa mpango wa kitaifa wa usalama wa wanahabari, kuwekwa wazi kwa majukumu ya kila taasisi na kuongeza uelewa kuhusu usalama wa kidijitali, uwajibikaji na madhara ya vitisho dhidi ya wanahabari.