RUPIA: USHAHIDI WA TANGANYIKA, RWANDA, BURUNDI NA KIONGA ZILIKUWA NCHI MOJA.
Deutsch Ostafrika - Rupie (German East Africa Rupie) kwa Kiswahili, 'Pesa ya Afrika Mashariki ya Ujeramani' ni fedha iliyokuwa inatumika katika nchi katika nchi au Koloni la Ujerumani la Afrika Mashariki kuanzia mwaka 1890 hadi mwaka 1916.
Deutsch Ostafrika (German East Africa) ni lile eneo lililojumuisha nchi za Kionga, Tanganyika, Rwanda na Burundi. Lakini Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 - 1918) ndiyo iliyokuja kubadili jiografia ya utawala wa eneo hili. Mwaka 1916, nchi ya Kionga ilinyakuliwa na Ureno. Rwanda na Burundi zikachukuliwa na Wabeligiji na eneo kubwa lililobaki kilichukuliwa na Uingereza. Hili ndilo Waingereza waliliita Tanganyika.
Nchi ya Kionga iliunganishwa na kuwa sehemu ya Tanganyika mwaka 1894 chini ya Ujerumani. Baada ya Ureno kuinyakua mwaka 1916, ndipo
Mkataba wa Amani ulioitwa Versaille Treaty wa 19 Juni 1919 uliikabidhi Kionga kwa Ureno na tangu wakati huo ikawa sehemu ya Koloni la Ureno ambalo baadaye lilipopata uhuru likawa nchi ya Msumbiji. Mkataba ule ndio uliopitisha Mto Ruvuma kuwa mpaka kati ya Koloni la Waingereza (Tanganyika) na Koloni la Wareno (Msumbiji).
Kwa sasa, Kionga ni Jimbo la Cabo Delgado lililo Kaskazini mwa Msumbiji na Kusini mwa Tanzania linakopakana na Mkoa wa Mtwara na linakadiriwa kuwa na watu 2,500,000. Makabila katika Jimbo hili ni Wamakonde na Wamakua. Mwani ni kabila dogo linalopatikana huko pia.
Watu wa Jimbo la Cabo Delgado na Mtwara ni wamoja. Wamakua wa Msumbiji na Wamakua wa Tanzania husema lugha moja. Wamakonde wa Msumbiji na hata Wamakonde wa Tanzania husema pia lugha moja. Kabla ya mwaka 1916, Jimbo hili la Cabo Delgado lilikuwa sehemu ya Tanganyika na Rwanda na Burundi pia zilikuwa sehemu ya Tanganyika.
Credit:
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula