Wakati mama yake akiwa kitandani hoi bin taaban, hajiwezi na anahitaji msaada haraka iwezekanavyo, mtoto Rose (mwenye miaka kumi) aliishia kumtazama tu mpaka kifo chake!
Hakujigusa na wala hakutaka kujisumbua kwani alikuwa hampendi mama yake kwa namna alivyokuwa anamtenda.
Alimchukia toka ndani na chuki hiyo ilimfanya asijali hata pale mama yake alipokiri kuwa amefanya makosa, badala yake akaufunga mlango na kumwacha mama akitwaliwa na umauti.
Miaka mingi mbele, Rose anakuwa daktari wa magonjwa ya akili. Anaipenda kazi yake mno na anaifanya kwa moyo wake wote. Anapokea na kuwasaidia watu kiasi kwamba anakuwa tegemezi hospitalini hapo. Mambo ni shwari kabisa. Ana mpenzi anayempenda na pia ana kazi anayofurahia kuifanya.
Mambo yanakuja kubadilika pale usiku mmoja Dr. Rose anapokutana na mgonjwa wa ajabu, msichana wa chuo kikuu ambaye ametoka kushuhudia profesa wake akijiua mbele yake!
Msichana huyo anamweleza Dr. Rose kuwa tokea hapo amekuwa akifuatwa na roho ya ajabu ikimwambia kuwa naye atakufa! Roho hiyo ipo katika mfumo wa mtu anayetabasamu ikiwa inahama toka mtu na mtu, tukio na tukio.
Msichana huyo amejaribu kuwaambia watu wengine lakini hakuna anayemwamini. Kila mtu anamdhania amewehuka kiasi cha kukosa msaada, bahati mbaya hata huyu Dr. Rose naye anaamini mtu huyu ni mgonjwa.
Ghafla msichana huyo anadondoka chini akihangaika kama mtu aliyeshikwa na degedege kali! Dr. Rose anawahi kupiga simu ya msaada lakini anapokata simu hiyo nakumtazama mgonjwa wake anamkuta akiwa amesimama salama salmin kama si yeye alotoka kuhangaika kiasi kile!
Kama haitoshi mgonjwa huyo anatabasamu kiajabu, mkononi ameshikilia kwanguvu kipande cha chungu cha maua. Kufumba na kufumbua, msichana huyo akiwa anatabasamu, anajikata shingo na kuanguka chini akiwa mfu!
Dr. Rose anatoa macho kustaajabu. Anaogopa mno. Lakini asilolijua ni kwamba, huu ni mwanzo tu ... Mwanzo wa maisha yake kuwa kama ya digidigi porini huku watu wake wa karibu wakimwona amewehuka!
Dr. Rose anaanza kuona sura za ajabu zikimtabasamia huku akiupata ujumbe wa kifo chake vilevile kama alivyokuwa akielezwa na mgojwa wake wa mwisho!
Dokta anakuja kubaini kuwa kifo cha mgonjwa yule mbele yake kilikuwa ni kupokea kijiti cha laana, lakini chanzo ni nini? Na kwanini yeye?
Na je, atamudu kujinasua kabla hajakumbwa na umauti?