Duh, kwanza pole sana kwa uchungu huo unaokusibu.
Pili, naamini umeisoma vizuri mada yangu, mwanzo hadi mwisho na kuanza kuufanyia kazi ushauri nilioutoa katika mada hiyo.
Tatu, napenda kukushauri kibiblia maana Biblia ndio mwongozo wetu sisi tunaomwamini Mungu. Ukiuzingatia ushauri huu, utavuka salama katika hilo tatizo linalokuandama.
Umesema unampenda sana mpenzi wako. Sasa kama kweli unampenda sana, hupaswi kuhesabu mabaya yake. Nimeona umeorodhesha mabaya yake mengi: kukawia kupokea simu, unafiki, kukimbilia kwa ma-x wake, kutokujua kupika...
Hapo hujataja hata moja zuri alilo nalo.
Sasa sikiliza: Katika kitabu cha 1 Wakorintho 13:4-8, Biblia inatutajia sifa za mtu mwenye upendo: ni mvumilivu, ni mwenye fadhili, haoni wivu, hana majivuno, hana kiburi. Hakosi kuwa na adabu, hatafuti mambo yake mwenyewe, hakasiriki upesi, hahesabu mabaya (yaani haweki kumbukumbu ya mambo mabaya aliyo/anayotendewa)...
Hilo la kuhesabu mabaya ndilo linalokuhusu sana hapo. Na yamkini sababu kubwa ya yeye kukukimbia ni tabia yako ya kumhesabia mabaya kila mara.
Hivyo nakushauri, badala ya kutaja tu mabaya yake kila unapoongea naye, msifie/mtajie mazuri aliyo nayo utaona jinsi atakavyobadilika na kuvutwa kuwa karibu na wewe.
Katika Mt 18:21-22, Biblia inatuambia pia kwamba: ndugu yako akikukosea hata saba mara sabini unapaswa kumsamehe. Hiyo maana yake ni kwamba, msamaha haupaswi kuwa na kikomo. Ukisamehe leo, achilia. Akirudia kosa lile lile kesho, usimuulize kwanini amerudia kosa lile lile. Kosa la kesho, hesabu kuwa hilo ni la kwanza, maana jana uliishasamehe na kuachilia au kusahau.
Halafu, Maandiko yanatuambia katika Luka 6:41-45 hivi: "Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako?"
Hiyo ina maana kwamba kabla ya kumuona mwenzako kuwa ana tatizo, ujichunguze mwenyewe; uhakikishe kwanza wewe ni safi. Kwa mantiki hiyo, nikuulize: je wewe huna udhaifu hata mmoja? Jaribu umuombe huyo mpenzi wako akuambie bila kuficha, anakuonaje wewe, au umuulize akutajie bila kuficha, makosa anayoyaona kwako; utashangaa na wewe unayo makosa au udhaifu mwingi. Kwa sababu hiyo ukijua na wewe unao udhaifu, utajirekebisha kwanza kabla ya kumkosoa mwenzako.
Huo ndio ushauri wangu kwa kifupi.
Naomba nikuulize: huyo mpenzi wako, mmeoana au mko tu kwenye mahusiano yatakayowapelekea kufunga ndoa? Na je, hao ma-x wake ni Ex-boyfriends au ni Ex-husbands?