Kikwete aongoza mazishi ya Sheikh Yahya Send to a friend
Saturday, 21 May 2011 21:34
0
digg
Hussein Issa
VIONGOZI mbalimbali wa siasa na dini akiwamo Rais Jakaya Kikwete, jana walijitokeza kumzika mtabiri maarufu wa nyota Afrika Mashariki na Kati Sheikh Yahya Hussein aliyefariki dunia juzi.
Wakati viongozi wengine wakijitokeza msibani hapo tangu asubuhi, Rais Kikwete alishiriki msiba huo kwenye mazishi yaliyofanyika katika makaburi ya Tambaza yaliyoko jijini Dar es Salaam saa 10:00 jioni.
Viongozi wengine wa siasa walioshiriki mazishi hayo jana ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Nec Mkoa wa Dar es Salaam, Adam Madabida na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Kabla ya kupelekwa kuzikwa mwili wa marehemu ulipelekwa katika Msikiti wa Manyema Kariakoo, kuombewa kwa maandamano yaliyojumuisha maelfu ya watu, yaliyoanzia nyumbani kwake Magomeni Mwembechai saa 9:00 alasiri.
Baadaye mwili huo ulipelekwa katika Makaburi ya Tambaza kwa maziko huku ukiwa umebebwa na mamia ya watu waliojitokeza huku wakitembea kwa miguu.
Baada ya kufika katika makaburi, Rais Kikwete aliongoza umati wa watu kuuzika mwili wa marehemu.
Mzee wa upako ahudhuria
Baadhi ya viongozi wa kidini waliofika nyumbani kwa marehemu mapema asubuhi ni pamoja na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bin Simba na Mchungaji Adamu Lusekelo, maarufu kwa jina la 'Mzee wa Upako'.
Akizungumza katika msiba huo, Sheikh Simba alisema taifa limepoteza mtu muhimu ambaye pengo lake haliwezi kuzibika kiurahisi.Alisema anamfahamu Sheikh Yahya Hussein siku nyingi na alikuwa mtu wa karibu sana kwake wakishauriana na kutiana moyo katika mambo mbalimbali.
"Hili ni pengo bwana, halizibiki leo wala kesho. Nilimtumia huyu (Sheikh Yahya) kama mshauri wangu wa karibu. Moja ya mambo niliyoyapenda kwake ni kusikiliza anavyosoma Qur'an," alisema Mufti Simba.Akizungumza msibani hapo jana, Mchungaji Lusekelo alisema alioteshwa katika ndoto kifo cha Sheikh Yahya siku moja kabla.
Alisema Mungu alimwotesha kwamba Sheikh Yahya kapanda daraja na alipozunduka kutoka usingizini, akawa anaitafakari na kesho yake saa tano asubuhi, alipigiwa simu kujulishwa msiba huo. "Niliooteshwa na Mungu kuhusu kifo hiki hivyo huyu rafiki yangu ataenda kulala sehemu aliyoandaliwa," alisema
Viongozi CCM, Chadema, CUF
Mwakilishi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Adam alisema marehemu Sheikh Yahya alikuwa mtu wa watu hivyo ni vizuri akaenziwa kwa uchapakazi wake.
Alisema taifa limempoteza mtu mashuhuri na hata kwa upande wa chama (CCM) pia kimepoteza kada wake kwani Sheikh Yahya alikuwa mkereketwa chama hicho siku zote., alisema kwa sababu marehemu alikuwa hapendi unafiki na chuki, ni vizuri vyama vya siasa vikamuenzi kwa kuacha siasa za chuki.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Sheikh Yahya alikuwa mtu mnyenyekevu hivyo ni bora kila mtu amuenzi kwa matendo yake.Alitaka pia vyama vya siasa kuacha chuki baina yao ili kumuenzi Sheikh Yahya ambaye katika siku ya uhai wake hakupenda chuki na unafiki.
Masheikh wamlilia
Katika tukio jingine vilio na majonzi vilivyotawala msibani hapo jana viliwafanya baadhi ya masheikh kushindwa kusoma Qur'an.Hata hivyo habari zilizopatikana msibani hapo jana zimeeleza kuwa masheikh wengi walioshindwa kusoma Qur'an ni marafiki wa karibu wa marehemu.
Kila walipokuwa wakisoma, walikatizwa na kelele za vilio na simanzi kutoka kwa waombolezaji.Sheikh Yahya Hussein alifariki dunia juzi saa nne asubuhi katika Hospitali ya Mount Ukombozi alikopelekwa kwa matibabu, baada ya kuugua ghafla.
SOURCE MWANANCHI JPILI