JK azua mjadala
na Peter Nyanje, Dodoma
Tanzania Daima
HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kuwabana zaidi viongozi wa umma kupitia sheria ya maadili, haitokuwa na manufaa makubwa iwapo utekelezaji wake utasuasua.
Aidha, manufaa ya hatua hiyo yataonekana zaidi kutokana na uwajibikaji wa viongozi wenyewe na tafsiri sahihi ya yaliyomo kwenye sheria hiyo.
Maoni hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti jana na wanasiasa na wasomi mbalimbali waliozungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam na Dodoma.
Baadhi ya waliozungumzia suala hilo, ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF) aliyesema kuwa, iwapo utekelezaji wa kauli za Rais Kikwete utafanyika nchi itarajie mabadiliko.
Alisema, mabadiliko anayoyataka Kikwete hayatakuwa na maana iwapo watu watakaowania uongozi hawatafanya hivyo kwa dhamira ya kuwatumikia wananchi.
Hamadi Rashid alisema kuwa pamoja na hayo, ili sheria hiyo iweze kuleta mafanikio yanayotakiwa, ni vema kukawa na tafsiri sahihi ya nini hasa ni biashara.
Akifafanua, alisema kuwa zamani viongozi walikuwa wanakatazwa hata kumiliki kuku na baadaye masharti hayo yalilegezwa na kuruhusiwa kulima, na kutakiwa kuwa mfano kwa wananchi wengine katika kilimo.
"Sasa kama mimi kiongozi nikiwa namiliki ekari 100 za ardhi na ninazitumia kwa kilimo, hii itahesabiwa kama biashara au vipi?" alihoji.
Aidha, alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria ya maadili iliyopo, mwenzi wa ndoa wa kiongozi, naye anahesabika kama kiongozi na kutaka kufahamu haki ya wenzi hao itakuwaje wakati wenzi wao, ambao ndio viongozi, watakapotakiwa kuacha kufanya biashara wakati wana haki ya kikatiba kujishughulisha.
Hamad Rashid alisema kuwa, hata sheria iliyopo sasa inaweza kusaidia sana kuleta mabadiliko iwapo itafanyiwa marekebisho madogo na kutumiwa ipasavyo.
"Tatizo letu ni kuwa hata sheria iliyopo hatuitumii ipasavyo… inapasa imlazimishe kiongozi si tu kutaja mali zake, bali kutangaza hadharani na kumpa uhuru mwananchi yeyote kwenda kuhoji mali hizo.
"Pia inatakiwa tuwe na utaratibu utakaotuwezesha kila mwaka viongozi watangaze mali zao na kueleza wamezipata vipi ili wanapomaliza muda wao wa uongozi isiwe shida kuona mtu amepata wapi mali anazozimiliki ambazo hakuwa nazo wakati anaingia katika uongozi," alisema.
Hamad Rashid alisema viongozi wengi wanajiingiza katika biashara kwa sababu hawana uhakika wa maisha yao baada ya kustaafu kwa kuwa hawana mishahara mizuri na mafao bora.
Alisema ili kurekebisha hali hiyo, ni vema sheria itakaporekebishwa kuliangalia suala hilo, ili kiongozi aandaliwe maisha yake baada ya kumaliza utumishi ili kumfanya awe muadilifu anapokuwa madarakani.
"Viongozi wengi tuliokuwa waadilifu, akiwemo Hamad Rashid mwenyewe, tunaishi maisha ya dhiki," alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (Chadema), alisema hatua ya kuiboresha sheria ya maadili ni nzuri, lakini hofu yake ni kasi ya kufanya hivyo, jambo ambalo linaweza kuchelewesha utekelezaji wa azma hiyo.
Akitoa mfano, alisema kuwa katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge mwaka juzi, Rais Kikwete aliahidi kulifanyia kazi suala la fedha zinazotumika katika kampeni za kisiasa, lakini hadi sasa haieleweki limefikia wapi.
Alisema, wakati muswada wa sheria mpya ya rushwa ulipoletwa bungeni, yeye na mbunge mwenzake wa upinzani walitumia fursa hiyo kuibana serikali kueleza ilipofikia katika suala hilo, hata hivyo, hawakupata ufafanuzi wa kuridhisha.
Zitto alisema kuwa katika majadiliano hayo, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliahidi kuwa suala hilo lingeshughulikiwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
"Kwa kweli masuala haya, ambayo ni muhimu sana yanachukua muda mrefu kushughulikiwa kiasi kwamba yanapoteza maana yake," alisema Zitto na kuongeza kuwa mwaka juzi, alitumwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kwenda kwenye Bunge la Canada kujifunza zaidi kuhusu utekelezaji wa sheria ya maadili.
Aliporudi, aliandaa muswada binafsi unaolenga kufanya marekebisho makubwa katika sheria ya maadili na kuuwasilisha bungeni, hata hivyo Katibu wa Bunge alimfahamisha kuwa muswada huo hauwezi kuwasilishwa bungeni kwa sababu utekelezaji wa mabadiliko aliyoyapendekeza yanahitaji mabadiliko ya katiba kwanza.
"Sasa baada ya rais kuonyesha dhamira ya kuibadilisha sheria ya maadili, nitakaa chini na kuangalia la kufanya kuhusu muswada wangu binafsi," alisema.
Kutoka Dar es Salaam, Mwandishi Happiness Katabazi anaripoti kuwa, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema anachotakiwa kufanya Kikwete ni kuwafukuza watendaji wasio waadilifu kwanza, wanaotuhumiwa kushiriki kwenye mikataba yenye utata.
"Rais amekuwa na tabia ya kutoa lugha ya kufurahisha Watanzania kwa sababu ni Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo ilizika Azimio la Arusha, uamuzi ambao ulilalamikiwa na wananchi wengi kwamba siasa imekuwa biashara na mnada wa kula, lakini walipuuzwa.
"Anachotakiwa kufanya rais ni kuwafukuza watendaji wake wasio waadilifu wanaotoa tenda za ‘kishikaji' kwa wafanyabiashara walanguzi ambao ni wafadhili wakuu wa CCM wakati wa uchaguzi.
"Ni lazima atofautishe walanguzi na wafanyabiashara. Nyerere alipoanzisha Azimio la Arusha hakuwa mwendawazimu, lakini ni hawa hawa CCM walimpuuza na kwenda kulizika huko Zanzibar…hivyo waliruhusu siasa kuwa ya wafanyabiashara," alisema Mbowe.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kazi ipo kwenye maadili kwa viongozi na watendaji wa serikali ili waweze kuaminika kwa wananchi na kutunga sheria kwa kuwa sheria haitengenezi maadili bali siasa safi.
Kuhusu kauli ya rais ya kuwataka wabunge na mawaziri kushika moja kati ya siasa au biashara, Baregu alisema upo ushahidi wa mgongano wa kimaslahi kwa viongozi kwa baadhi ya mawaziri au wabunge katika suala hilo na si geni kwa sababu limeainishwa kwenye Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
"Kitendo cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alipokuwa madarakani kujiuzia kampuni ya makaa ya mawe Kiwira na mawaziri ni mgongano wa wazi wa kimaslahi, lakini Watanzania tulihoji na Rais Kikwete akamtetea kwa madai kuwa tumwache apumzike na kwamba siyo vema kumchunguza rais aliyemtangulia…hapa tunategemea nini kama siyo mgongano wa kimaslahi," alisema Profesa Baregu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Agustine Mrema, alimtaka rais awatajie Watanzania majina ya mawaziri wake ambao maslahi yao yamegongana na maslahi ya umma kisha aanzishe mchakato huo.
"Rais aache nadharia hapa…kwanza atutajie hao mawaziri wake ambao maslahi yao yamegongana na ya umma. Hivi ina maana alikuwa hajui athari zake? Na aliyemwambia wafanyabiashara peke yake ndiyo wanahujumu nchi hii ni nani? Kwani hajui kwamba kuna watu wanahujumu nchi hii kwa kutumia kalamu na karatasi tu tena bila ya kuwa wafanyabiashara?" alihoji Mrema.