Pasi na shaka Mkutano wa Chadema tarehe 12/08/2024 Jijini Mbeya, ulikuwa tofauti kubwa na mikutano mingine ya Chadema iliyowahi kufanyika nchini hivyo Uamuzi wa Serikali kuuzuia umeungwa mkono na baadhi ya wananchi na wanasiasa nchini.
Mohamed Issa Ubuguyu, mwanachama wa CUF, amesema Serikali iko sahihi kuzuia mkutano huo ikiwa imeona Kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.
Ubuguyu anasema, wakati mwingine wanasiasa wanatumia vibaya uhuru uliopo kwa nia ya kuanzisha harakati za machafuko ili tu kukidhi matakwa yao.
"Tuwe wakweli jamani, tunataka uhuru wa maoni, ambao tunao tusiutumie vibaya, na Serikali haifanyi kazi kwa kubahatisha, mkutano huo wa Chadema kabisa ulikuwa na viashiria vya vurugu.
"Tufanye siasa, lakini tutangulize maslahi ya umma, amani na utulivu ni kipaumbele Cha kwanza," anasema Ubuguyu.
Justice Mwalambalo, mwanachama wa ACT Wazalendo, anasema bayana kwamba, huenda Kuna kitu nyuma ya mkutano huo wa Mbeya na ndiyo maana nguvu kubwa ilielekezwa huko tofauti na miaka ya nyuma ambayo Bawacha imekuwa ikiadhimisha kongamano la vijana.
"Mbona tangu tumeruhusiwa kufanya siasa za majukwaani hatujawahi kuzuiwa? Wenzetu Chadema walizunguka nchi nzima na agenda ya Katiba Mpya na Mkataba wa Bandari na hakuna aliyewazuia, iweje iwe sasa? Serikali siyo wajinga, yawezekana kabisa kuna kitu wamekiona," anasema Mwalambalo.
Juma Mpula, mkazi wa Mtaa wa Mwakibete Jijini Mbeya amejaribu kuunganisha matukio huku akirejea kauli zilizotolewa na baadhi ya wanaharakati na wafuasi wa chama hicho siku chache kabla ya mkutano.
"Ukweli ni kwamba Chadema imekuwa ikifanya mikutano ya kisiasa na hata maandamano katika maeneo mbalimbali nchini kuelezea ajenda na masuala mbalimbali kuhusu itikadi za chama hicho pasipo kuzuiliwa na mamlaka za Serikali."
Mkutano wa Chadema uliopangwa kufanyika tarehe 12/08/2024 ulilazimika kuzuiliwa na mamlaka za Serikali kutokana na sababu kadhaa, zikiwemo viashiria vya uchochezi na uvunjifu wa amani.
Mpula ametolea mfano Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, Moza Ally, ambaye katika moja ya kauli zake alisikika akisema: “Kama kijana yeyote unayeipenda nchi yako ya Tanzania umeshalia miaka yako yote, siku hiyo ya Agosti 12, 2024 tunakwenda kuweka hatma ya taifa letu la Tanzania mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo Uwanja wa Ruanda Nzovwe, Mbeya..... Tupo Serious na jambo hili, kwa hiyo vijana wote wa Chadema kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua siku ya Tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja kwa serikali, vijana wa Kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.” mwisho wa kunukuu.
Mpula akasema: "Ukiangalia kauli zile utabaini kwamba kulikuwa na jambo walilokuwa wanalikusudia, sasa wamezuiwa wanaona azma yao haijatimia na wanataka huruma ndiyo maana wanapiga kelele," anakumbusha.
Mpula ameonya kwamba vyama vya upinzani visitengeneze matukio ili kuungwa mkono na wananchi, kwani kitendo hicho kinaweza kuleta athari ya amani na utulivu nchini.
Mwanamvua Nyambi, Mkazi wa eneo la Mbalizi amesema, vyama vya siasa na viongozi wao wawafikirie zaidi wananchi kwa kudumisha amani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.
"Hiki ni kipindi kigumu sana, lakini ndicho wanasiasa wanaotafuta 'kiki' hukitumia kujijenga bila kujali kitakachowapata wananchi. Matukio kama haya yaliwahi kutokea huko nyuma, walioumia ni wananchi wa kawaida tena kwa ukaidi wa viongozi wa kisiasa baada ya kuzuiwa kukusanyika," anakumbusha Mwanamvua.
My take
Naiomba Serikali iendelee kusimamia haki pale panapostahili na kuzuia machafuko ikiwa vyombo vya Dola vitabaini mikutano hiyo inaweza kuleta uvunjifu wa amani nchini.