Askari yeyote haruhusiwi kufanya upekuzi mahali popote pale bila kuwa na Hati ya Upekuzi inayotolewa na Mahakama. Muda rasmi wa kufanya upekuzi ni kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi 12:30 jioni.
Upekuzi utafanywa tu wakiwepo watu hawa:
1. Mwenye nyumba au mwakilishi wake
2. Mjumbe au Mwenyekiti wa Mtaa au Afisa Mtendaji
3. Jirani yeyote anayefahamiana na mwenye nyumba au mtu atakayeteuliwa na mwenye nyumba
Kabla ya upekuzi, mtuhumiwa ana haki ya kumpekua au kuwapekua askari kabla ya kuanza upekuzi. Hii ni kuepusha askari kuweka chochote kinachoweza kumweka mtuhumiwa kwenye makosa kijinai, kwani imeshatokea askari kupandikiza misokoto ya bangi au silaha kwenye maeneo yanayokaguliwa na kudai kuvikuta vitu hivyo mahali hapo.
Muhimu zaidi mtuhumiwa anayepekuliwa ana haki ya kuisoma hati ya upekuzi na iwapo hajui kusoma basi asomewe hati hiyo na mtu mwingine ambaye anajua kusoma na ambaye sio askari.
Mlalamikaji anaruhusiwa kuwapo kwenye upekuzi ili aweze kutambua vitu ambavyo ni mali yake iwapo tuhuma zitakuwa ni wizi wa mali au kujipatia mali kinyume cha sheria.
Kama kuna yeyote ambaye amepekuliwa kinyume na taratibu hizi, upekuzi huo utahesabika kuwa batili na hautatambuliwa kisheria.