Date::7/13/2009Mwananchi
Na Ramadhan Semtawa
MKURUGENZI wa Mashtaka (DDP), Eliezer Feleshi amesema ni vigumu kuwaburuza mahakamani watuhumiwa wanaohusika na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, akisema kufanya hivyo kunaweza kuiweka serikali mahali pagumu kwani serikali inaweza kuwakamata waliotumwa kuchukua fedha, lakini ikashindwa kuwanasa waliowatuma.
Kagoda inadaiwa kuchota Sh40 bilioni kwa kisingizio cha kufanya kazi za Idara ya Usalama wa Taifa, lakini kumekuwa na utata mkubwa kuhusu wamiliki wakuu wa kampuni hiyo.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, DPP Feleshi alisema kutokana na ugumu huo, ameagiza upelelezi zaidi wa jalada la Kagoda ili kupata vielelezo na uthibitisho kuhusu pande zote mbili za shilingi.
Mahojiano hayo yalilenga kufahamu nini hasa ugumu wa kufikisha mahakamani watuhumiwa wa Kagoda, wakati baadhi ya watuhumiwa walioiba Sh 90.3 bilioni kutoka makampuni 13, walishafikishwa mahakamani huku uchunguzi wa Sh 42.6 bilioni, ukiendelea nje ya nchi.
"HIvi ninyi (waandishi) mnaitakia mema serikali; hivi sasa kuna baadhi ya kesi zinaendelea kama za akina (majina tunahifadhi), mmeanza kuandika mara serikali hivi yashindwa, sijui hivi..." alisema.
"Hatufanyi mambo kwa kukurupuka, ndiyo maana nimeagiza upelelezi zaidi; leo hii naweza kuagiza fulani akasomewe mashtaka, lakini kesho anakuja kukuonyesha vielelezo kwamba mimi nilitumwa tu kuchukua pesa. "
DPP Feleshi aliongeza kusema: "Hivyo, ni lazima uangalie upande wa pili wa shilingi. Nani kamtuma akachukue hizo fedha na yuko wapi..., au wewe (mwandishi) unapenda kuangalia upande mmoja tu wa shilingi na kufanya maamuzi?"
Alifafanua kwamba fedha hizo ambazo zote zimeibwa katika Akauti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT), zinahusisha makampuni 12 ikiwemo ya kigeni, hivyo haiwezi kuwa rahisi kubaini wahusika wakuu mara moja.
"Hivi kitu kinachohusisha makampuni 12 tena mengine ya nje unaweza kukifanya kwa urahisi kiasi hicho, unaangalia mtu anakwambia labda mimi nilitumwa tu, sasa hapa tunatafuta nani kamtuma," aliongeza DPP Feleshi.
Alisema ni hatari kwa ofisi yake kukurupuka kuchukua maamuzi ya kufikisha watuhumiwa wa Kagoda mahakamani bila ushahidi wa kutosha, kwani serikali inaweza kuangushwa katika kesi.
Feleshi alitoa wito kwa Watanzania kupeleka uthibitisho wa nani hasa ambaye ni mmiliki wa Kagoda na ofisi yake itamlinda mtoaji taarifa hiyo.
"Kama kuna mtu ana uthibitisho wa vielelezo alete, nitamlinda."
Feleshi alisema Kagoda ni kampuni tata inayohitaji upelelezi zaidi ambao bado unafanywa na Kurugenzi ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai (DCI).