Leo 23 November 2023 meli ya uvuvi ya MV Pacific Star imefika bandarini Dar es Salaam na kushusha tani 50 za samaki mchanganyiko ambao siyo aina ya tuna / jodari.
Toka Maktaba :
ZANZIBAR WATAKA MGAO WA SAMAKI JODARI / TUNA
November 25, 2009 · by
zanzibarkwetu · Bookmark the
permalink. ·
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema haina taarifa zozote kuhusiana na kupata mgao wa samaki waliovuliwa na meli ya Kigeni katika bahari Kuu ya Tanzania (Samaki wa Magufuli) mwaka huu.
Samaki hao walitarajiwa kugaiwa hivi karibuni baada ya Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, John Pombe Magufuli kutangaza katika vyombo vya habari Mjini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alisema kuwa Serikali haijui lolote kuhusiana na kufaidika na mgao wa samaki unaogaiwa huko Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Waziri Magufuli tani 296.32 za samaki aina ya jodari zilizokamatwa zikivuliwa na wavuvi kutoka nje katika bahari ya Tanzania kwenye Ukanda wa Uchumi wa bahari Kuu nchini watagaiwa katika taasisi 115, zilizopitishiwa maombi yao kupata kitoweo hicho.
Zanzibar imekuwa na wasi wasi juu ya kupata mgao huo wa kupata samaki baada ya serikali kukiri kuwa hakuna tarifa yoyote iliyopokelewa kutoka serikali ya Muungano inayoeleza kuhusu mgao wa samaki hao na namna Zanzibar itakavyofaidika nao.
Waziri Hamza alisema kwamba taarifa walizozipata kuhusu samaki hao ni kupitia matangazo ya magazeti yanayotaka taasisi zinazohitaji samaki hao kuomba, lakini serikali haina taarifa rasmi kutoka serikali ya Muungano inayoelezea hilo wala hakuna barua yoyote iliyopokea.
Hata hivyo alisema zaidi suala hilo limefikishwa kwa Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Mazingira, ili lifanyiwe kazi kwa vile Wizara hiyo
ina vikao vya ushirikiano kisekta.
Suala la uvuvi wa Bahari Kuu ni miongoni mwa mambo yaliomo katika orodha ya mambo ya Muungano huku Zanzibar ikiwa ndio Makao Makuu ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ambapo majengo yake yanatarajiwa kujengwa Fumba Wilaya ya Magharibi Unguja.
Awali ziliwahi kuzuka hoja kadhaa kuhusu samaki hao ndani ya vikao vya Baraza la Wawakilishi vilivyopita, na wajumbe wengi waliulizia hatma ya Zanzibar kupata samaki hao ikiwa ndio Makao Makuu ya Mamlaka hayo.
Wajumbe wa baraza la wawakilishi katika kikao kilichomalizika mwezi huu walitaka kupatika mgao wao wa samaki kwa kuwa wao ni wadau wakuu katika suala hilo na kuiomba serikali iweke wazi juu ya gawio lake ambalo linatakiwa kupatiwa wazanzibari.
Waziri Hamza, alisema Zanzibar inashindwa kufahamu kwamba inatakiwa iombe mgao wa samaki hao kama utaratibu alioutangaza Waziri Magufuli kwa kuwa suala la Bahari Kuu kisheria ni kupata mgao wa mapato ya asilimia 40 na asilimia 60 ni ya Tanzania Bara yanayotokana na Bahari Kuu.
Alisema kwa hali hiyo, Zanzibar ilipaswa itengewe tani zake za asilimia 40 kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa matumizi ya Bahari Kuu na sio kutakiwa vikosi na vyuo kuomba msaada kwa samaki hao kama ilivyoelezwa.
“Ilitakiwa serikali ya Muungano kutoa mgao huu ni wa Zanzibar na hapo Zanzibar ijue namna ya kuugawa baada ya kukabidhiwa chao, sio suala la Idara zetu ziombe” alisema Waziri huyo.
Waziri alisema haiwezekani kwa taasisi za Zanzibar, kuomba samaki hao moja kwa moja katika Wizara ya Uvuvi ya Tanzania Bara, bila ya maombi husika kupitia katika Wizara inayosimamia shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu hapa Zanzibar.
“Zanzibar ina Wizara yake ilitakiwa Wizara ya Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo yaTanzania Bara, izungumze na mwenzake kwani wanavyo vikao vya mahusiano ya kisekta, hasa suala hili ni mambo ya Muungano, haiwezekani Idara za Zanzibar, zikurupuke ziende kuomba bara, bila ya maombi yao kupitia Wizara husika hapa Zanzibar” alisema Waziri huyo.
Alisema kiutaratibu taasisi za Zanzibar zingeweza kuomba samaki hao baada ya serikali ya Zanzibar kukabidhiwa mgao wake kutoka serikali ya Muungano kupitia Wizara husika.