Karakana ya Luban ya China yachochea maendeleo ya ujuzi kwa vijana nchini Madagascar

Karakana ya Luban ya China yachochea maendeleo ya ujuzi kwa vijana nchini Madagascar

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
20f1de58bfce4489b05f3c42251198e2.jpg


Tangu warsha ya kwanza ya mafunzo ya Luban ilipozinduliwa mwezi Machi 2019 nchini Djibouti, China imeanzisha jumla ya warsha 11 za Luban katika nchi 10 za Afrika. Kwa kuzingatia falsafa ya “kuwapatia nyavu na kuwafundisha uvuvi badala ya kuwapa samaki”, warsha za Luban zimejitahidi kuendeleza elimu ya ufundi barani Afrika, kuinua uwezo wa bara hilo katika uvumbuzi na maendeleo endelevu, na kutoa mchango muhimu katika kukuza mawasiliano na ushirikiano wa kiutamaduni kati ya China na Afrika.



Warsha ya Luban ni sehemu ya mpango wa kuijengea Afrika uwezo uliopendekezwa katika Hatua Nane za Utekelezaji zilizotolewa kwenye Mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2018 mjini Beijing. Kama hatua muhimu ya kuanzisha jukwaa la mawasiliano na ushirikiano wa kiutamaduni kati ya China na Afrika chini ya pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, warsha ya Luban imepiga hatua kubwa katika kuziba pengo la ushirikiano wa elimu ya ufundi kati ya pande hizo mbili.



Dimbbin’ny Riana Fitiavana Mamelasoa, mwanafunzi wa miaka 23 kutoka Madagascar anayesoma nchini China, anatumia mapumziko ya msimu wa baridi kufanya mafunzo kwa vitendo katika kampuni ya programu za kompyuta katika Manispaa ya Tianjin, kaskazini mwa China, ili kuboresha ujuzi wake kwa matumaini ya kuutumia nyumbani. Alifika China mwezi Oktoba mwaka jana kusomea teknolojia ya programu katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Makanika na Umeme cha Tianjin, baada ya kupata mafunzo ya awali katika Karakana ya Luban nchini Madagascar.



Anasema kuwa katika Karakana hiyo, alijifunza kwa kina kuhusu mifumo ya vifaa na usakinishaji wake. Kwa sasa, masomo yake yanalenga zaidi programu za kompyuta, mifumo ya software na uhandisi nchini China, huku akipanga kurejea Madagascar wakati wa msimu wa joto mwaka 2026 kufanya mafunzo kwa vitendo katika kampuni inayofadhiliwa na China.



Safari yake inaakisi mageuzi ya Karakana za Luban nchini Madagascar, ambayo ilisherehekea miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mwezi Desemba 2020 kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Antananarivo na taasisi za ufundistadi pamoja na viwanda vya China, na kuwa Karakana ya 10 ya Luban barani Afrika. Karakana hizi ni sehemu ya mradi wa elimu ya ufundistadi uliobuniwa kuendeleza ujuzi wa kiufundi katika nchi washirika.



Hapo awali, Karakana hiyo ilikuwa ikitoa mafunzo ya ufundi wa magari pekee, lakini sasa imepanua wigo wake kwa kuanzisha maeneo manne makuu ya mafunzo, yakiwemo uhandisi na teknolojia ya habari. Kwa sasa, inaendesha vituo viwili vya mafunzo na maabara tisa zilizo na vifaa 286 vya kufundishia. Walimu wanavielezea vituo hivyo kuwa vya kipekee nchini Madagascar kwa kuwa vinatoa mafunzo ya vitendo sambamba na matumizi ya mashine za kisasa.



Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, karakana hiyo imechangia kushughulikia uhaba wa ujuzi katika maeneo kama uzalishaji wa kiwango cha juu, nishati ya kijani na teknolojia ya kisasa ya magari, huku ikiimarisha mabadilishano ya watu kwa watu na ushirikiano wa kiviwanda kati ya China na Madagascar.



Kati ya wahitimu 29 wa kwanza wa Karakana hiyo, wengi wameajiriwa katika kampuni za ndani kupitia mafunzo kwa vitendo na kupata barua rasmi za ajira, huku wachache wakiendelea na masomo ya juu. Baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu tayari wamepata ajira kabla ya kuhitimu. Tangu wanafunzi wa kwanza walipoandikishwa mwaka 2022, Karakana hiyo imetoa mafunzo kwa wanafunzi 156 wa shahada ya kwanza. Walimu kutoka China na Madagascar kwa pamoja wameandaa vigezo vinne vya kufundishia vya kimataifa, kozi 25 za lugha, seti 28 za vitabu vya Kichina na Kiingereza, pamoja na zaidi ya dakika 5,000 za rasilimali za kujifunzia kwa njia ya video.



Mwezi Novemba 2025, Karakana ya Luban ya Madagascar ilijumuishwa rasmi kama mradi wa ushirikiano wa elimu ya ufundistadi kati ya China na Afrika chini ya mpango mpana wa Hatma ya Baadaye ya Afrika uliozinduliwa kwa pamoja na China na Afrika.



Wang Weiyuan, rais wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Makanika na Umeme cha Tianjin, alisema kuwa Karakana hiyo imeonyesha umuhimu mkubwa wa mafunzo kwa walimu na wanafunzi wa Madagascar, na ni ishara ya urafiki kati ya China na Madagascar, pamoja na daraja linalounganisha nchi hizo mbili.
 
Back
Top Bottom