*Baadhi wahofia siri za chama hicho kuvujia CCM
*Wapo waliosubiri kitoe tamko kuhusiana na hilo
Na Waandishi Wetu
BAADHI ya viongozi, makada na washabiki wa CHADEMA wameelezea kufadhaishwa na madai dhidi ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa mtu hadi kuvunja ndoa yake.
Wamesema uhusiano wake na Mbunge wa Viti Maalumu (Vijana) kupitia Bibi Amina Chifupa (CCM), umekiweka njia panda chama hicho.
Wakizungumza kwa wnyakati tofauti na gazeti hili jana Dar es Salaam, wengi walieleza kuwa na wasiwasi kwamba baadhi ya mambo muhimu yanayohusu CHADEMA pamoja na mikakati yake yatakuwa yamevujishwa kwa CCM kupitia kwa Bi. Chifupa.
Baadhi yao walielezea wasiwasi mkubwa kwamba huenda chanzo cha uhusiano huo kilikuwa ni mpango wa CCM kumtumia Bi. Chifupa kumshawishi Bw. Kabwe kuhamia CCM.
Bw. Kabwe amekuwa mmoja wa viongozi wa vyama vya upinzani ambaye amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu na CCM kuhamia chama hicho.
Wengine walielezea kusikitishwa kwao na Bw. Kabwe ambaye amewaangusha kwa kiasi kikubwa baada ya wanachama na mashabiki wa CHADEMA kuweka matumaini makubwa kwa mbunge huyo, kwamba ni kiongozi makini na mwadilifu.
"Siku zote tumekuwa tukijua kwamba kuna ufuska wakati wa vikao vya Bunge. Lakini sikuwahi kufikiria kabisa, kwamba Bw. Kabwe angekuwa mmoja kati ya watu wanaofanya vitendo hivyo. Kwa kweli ametuangusha sana," alikaririwa Bw. Pendael Macha ambaye lijitambulisha kuwa mmoja wa washabiki wa CHADEMA aliyekutwa akisubiri basi eneo la Mchikichini, Ilala.
Baadhi yao walielezea kusikitishwa kwao na kitendo cha mbunge huyo kujitetea kwa kusema kwamba atavifikisha mahakamani vyombo vya habari au watu wanaoingilia maisha yake binafsi.
"Mimi sijawahi kusikia kiongozi wa umma ana maisha binafsi. Wewe ukiwa mbunge, basi kila unalofanya linatazamwa kwa kina na linaongelewa na jamii. Cha msingi hapa ni kwa mwenzetu huyu kuja na kusema ukweli wake wa ndani na kama ni kuomba radhi, kwa familia ya Mpakanjia, kwa wana CHADEMA na umma kwa ujumla, basi tutamsikiliza," aliongeza.
Hata hivyo, wengine walilihusisha sakata hilo zima na siasa chafu zinazoendelea kuhusu nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Taifa wa CCM ambapo inasemekana Bi. Chifupa alionesha nia ya kugombea mwakani.
Hata hivyo, wengine walibainisha kwamba suala la msingi ni maadili binafsi ya wabunge hawa vijana wawili. "Hapa suala si siasa. Kama Amina angeheshimu ndoa yake na kama Zitto angemheshimu Amina kama mke wa mtu, yote haya yasingetokea".
Baadhi ya wananchi waliohojiwa, walishangazwa na ukimya wa CHADEMA katika suala hili, wakieleza kwamba CHADEMA ni chama ambacho hutoa matamko ya haraka haraka, mara linapotokea jambo lenye mjadala katika jamii.
Walisema hii ni dalili, kwamba mambo si shwari ndani ya chama hicho baada ya Bw. Kabwe kuwaweka njia panda wenzake na kuamua kukimbilia Kigoma, badala ya kubaki Dar es Salaam na kutafuta namna ya kukabiliana nalo.
Baadhi yao waliohojiwa kwa masharti ya kutotajwa majina, walitilia shaka zaidi kwamba huenda Bw. Kabwe alikuwa akivujisha siri za CHADEMA kwa Bi. Chifupa ambaye yeye na baba yake ni makada wa CCM.
"Kama kulikuwa na kupeana habari katika uhusiano huu, basi wenzetu wa CCM watakuwa ndio walionufaika. Kabwe ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na ni mtu aliye karibu sana na uongozi wa juu wa CHADEMA na anayejua mambo mengi sana ya chama chetu.
"Kwa upande wa Amina, yeye si kiongozi wa juu ndani ya chama na wala si mjumbe wa vikao vyovyote nyeti vya CCM," alisikitika kiongozi mmoja wa CHADEMA ambaye hakutaja jina lake litajwe kwa madai kwamba si msemaji wa chama.
Source: Majira, Ijumaa Mei 11, 2007;
http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=2869