Mlalahoi
JF-Expert Member
- Aug 31, 2006
- 2,182
- 885
Na: Athumani Hamisi
HabariLeo
HabariLeo
ALIYEKUWA mume wa Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Chifupa (CCM), Mohammed Mpakanjia amesema kupeana kwao talaka isiwe sababu ya kumfanya mbunge huyo ajifiche na kushindwa kutekeleza majukumu yake ya siasa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na HabariLeo Dar es Salaam jana, Mpakanjia alisema kupeana talaka ni jambo la kawaida katika maisha hivyo Amina awe huru kufanya shughuli zake za siasa.
Mpakanjia na Amina ambao wamedumu katika ndoa kwa miaka mitano na wana mtoto mmoja wa kiume wa miaka minne, walitalakiana Alhamisi iliyopita kwa sababu ambazo hazijabainishwa rasmi ingawa kuna madai yasiyothibitishwa kwamba ni saa chache baada ya Mpakanjia kudokezwa na Naibu Waziri mmoja madai juu ya mwenendo usiofaa wa mkewe.
"Anaweza kushindwa kufanya kazi zake nyingine na kujikuta anapoteza muda wake mwingi kujificha ama kutopatikana katika simu zake na sehemu muhimu anakotakiwa bila sababu za msingi," alisema Mpakanjia ambaye kwa sasa anauguza majeraha aliyoyapata katika ajali ya gari iliyotokea wiki iliyopita mkoani Morogoro. Alisema anajisikia vibaya kusoma katika magazeti kuwa Amina anajificha ama haonekani mitaani, kutokana na tukio hilo, jambo ambalo anadai limekuzwa kupita kiasi.
Alisema kuwa suala la mtalaka wake ni la kijamii na kuwataka watu waliolirukia, kuliacha na kumuacha Amina, awe huru katika kufanya kazi zake. "Nisingependa kuendelea kuzungumzia suala hili, napenda kulifunga rasmi na Amina awe huru kufanya mambo yake ya kisiasa.
Mpakanjia ambaye alifanya mahojiano na HabariLeo katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo, Dar es Salaam, alisema licha ya talaka bado ana ushirikiano mzuri na familia ya akina Chifupa akiwamo baba na babu yake.
"Niko hapa kumpokea babu yake Amina. Nimelazimika kuja licha ya kuwa naumwa kwa heshima na mapenzi makubwa ya familia. Ningekuwa na kinyongo nisingekuja," alisema. Wiki mbili zilizopita, Mpakanjia alijeruhiwa kwa kuungua sehemu kadhaa za mwili, baada ya gari lake kuwaka moto ghafla. Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser , liliteketea katika ajali iliyotokea mkoani Morogoro.
Hata hivyo, Mpakanjia, hakupenda kuzungumzia suala la kuwapo kwa barua aliyoiandika kwenda kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta na kama alitaka lizungumziwe katika chama.
"Kama kutakuwa na suala la nidhamu kichama, litashughulikiwa kichama na vikao vyake. Tatizo ni dogo sana lisikuzwe na kuharibu ‘CV' ya Amina. Nataka awe huru na shughuli zake za kila siku," alisema. Pia hakupenda kuzungumzia zaidi suala la talaka.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za ndoa ya Kiislamu ana nafasi ya kumrudia Amina endapo ametoa talaka moja.
Sheria ya ndoa ya Kiislamu, kuachwa kwa mke kwa talaka tatu ni ngumu kurudiana. Lakini mke huyo akiolewa na mume mwingine, kisha akaachika tena, mume wa kwanza anaweza kupeleka maombi yake tena na kumuoa upya. Lakini, endapo talaka moja itatolewa kwa mke na kuishi zaidi ya miezi, mwaka ama miaka bila kuolewa ama bila kupewa talaka nyingine mbili zilizosalia, inahesabika kuwa mwanamke huyo ameachika rasmi kisheria.
Kwa suala la matunzo ya watoto, sheria hiyo inamlazimisha mwanaume kumtunza mtoto/watoto. Ikiwezekana mke naye anastahili kutunzwa kama ana talaka moja ndani ya miezi kadhaa.
Katika moja ya vipengele vya kisheria, mume ataruhusiwa kuwachukua mtoto/watoto, endapo watatimiza miaka minane. Pia, haimzuii kuchukua mtoto/watoto kutoka kwa mwanamke, endapo itabainika kuwa hali ya mwanamke huyo kwa fedha ama maisha siyo nzuri.