Wadungu naomba nami nichangie mada hii ambayo wengi wanaona kama uhusiano wa DED na DAS ki-protokali unachanganya. Mchango wangu utazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
1. Mkuu wa Wilaya (DC)
Mkuu wa Wilaya anateuliwa na Raisi kwa mujibu wa kifungu cha 13 (2) cha sheria ya Tawala za Mikoa (The Regional Adminstration Act, 1997). Majukumu yake ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya. Kwa mantiki hiyo anakuwa muwakilishi wa Raisi katika kusimamia ulinzi, usalama na shughuli za maendeleo kwa ujumla. Akishateuliwa mkuu wa Wilaya anaapishwa na kusimamiwa kiutendaji na mkuu wa Mkoa (kifungu 13 kifungu kidogo cha 3).
2. Katibu Tawala wa Wilaya (DAS)
Kifungu cha 16 (2) cha sheria ya Tawala za Mikoa kinamtambua DAS kama principal adviser (yaani mshauri mkuu) wa DC. Kifungu hiki pia kinasema DAS anateuliwa kwamujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma. Bahati mbaya sina hiyo sheria hapa na nimetafuta mtandaoni sijaweza kuipakua. Ila natoa hoja yangu hapa kwa kuzingatia uteuzi wa Ma-DAS uliofanywa tarehe 5.8.2018 na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma. Katika tangazo lake kifungu cha 1.2 Waziri alisema, "Leo nimewaita kuzungumza nanyi kuhusu Uteuzi na Uhamisho wa baadhi ya Makatibu Tawala wa Wilaya. Kwa mamlaka niliyokasimiwa kwa mujibu wa Sheria nimefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wa Wilaya ili kujaza nafasi wazi kumi nane (18) zilizopo katika wilaya za Kinondoni, Mpwapwa, Dodoma, Iringa, Bukoba, Kigoma, Siha, Mtwara, Newala, Misungwi, Njombe, Kondoa, Manyoni, Kilindi, Chunya, Pangani, Bagamoyo na Handeni".
Hivyo, kwamujibu wa tangazo la Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma ambalo nimenukuu hapa, uteuzi wa DAS upo chini yake kisheria.
3. Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya (DED)
Kwa mujibu wa kifungu cha 22 (2) cha Sheria ya Utumishi wa Serikali za Mitaa ( The Local Government Service Act, 1982), DED anateuliwa na Raisi. Majukumu kiutendaji DED anakuwa Chief Executive wa Halmashauri na anaripoti kwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS).
Hitimisho
Kwangu mimi sioni mkanganyiko wowote wa kisheria kati ya DED na DAS, maana DED anateuliwa na Raisi na DAS anateuliwa na Waziri wa Utumishi wa Umma. Sema DAS anaweza kuonekana katika mazingira flani kuwa boss wa DED pale ambapo anatekeleza kazi anazotumwa na DC. Pia, nimewahi kuona mahala DAS anaudhuria vikao vya Council Management (CMT) ambavyo DED ndio mwenyekiti. DC ni mkuu kiitifiki kwa DED ingawa wote wanateuliwa na Rais, utofauti wao unatokana na majukumu. DC anapolinda amani, usalama na maendeleo ni pamoja na kazi anazofanya DED na wakuu wengine wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwenye ngazi ya Wilaya.
Huu ni uelewa wangu kwa kadri nilivyoelewa sheria husika, kama kuna mahala nimekosea niko tayari kukosoloewa maana mimi si mwanasheria kitaaluma. Asanteni