29, 2013 BY
ZANZIBARIYETU
Hamkani Si Shwari Tena
Ahmed Rajab
NOVEMBA
Ahmed Rajab
NOVEMBA 1960 Chinua Achebe, mshairi na mwandishi wa riwaya wa Nigeria aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 82, alifunga safari yake ya kwanza kuja Afrika ya Mashariki na ya Kati. …
Alifika Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar. Baadaye alizizuru Rhodesia mbili — ya Kaskazini (sasa Zambia) na ya Kusini (Zimbabwe).
Aliyoyaona yalimshangaza na kumshtua. Alikumbana na ukabila na ubaguzi.
Mshangao wa mwanzo aliupata wakati ndege aliyopanda ilipokuwa inakaribia kutua uwanja wa ndege wa Nairobi. Abiria walipewa fomu za uhamiaji kujaza. Akaona kuna vijisanduku vinne vya kuchagua kwenye fomu hiyo: kimoja kiliandikwa ‘Mzungu’, vingine ‘Mwasia’, ‘Mwarabu’ na cha mwisho kiliandikwa ‘Mwingine’.
Mwafrika alikua ‘mwingine’. Wakoloni walimnyima utu wake. Walifika hadi hata hatua ya kumpokonya ubinadamu wake.
Achebe alizizuru sehemu za huku kwetu mwezi mmoja baada ya Nigeria kupata uhuru wakati ambapo nchi zetu zilikuwa bado zikitawaliwa na Mwingereza ingawa zilikuwa karibu kupata uhuru.
Alipofika Tanganyika na Zanzibar, Achebe alifadhaishwa na namna Mwafrika alivyokuwa akidharauliwa na wasio Waafrika.
Jijini Dar es Salaam alisoma magazetini jinsi klabu moja ya wazungu ilivyokuwa ikijadiliana kubadili kanuni za klabu hiyo ili Julius Nyerere aweze kukaribishwa na mwanachama wa klabu kwenda kunywa pombe klabuni humo, ingawa hatujui iwapo Nyerere mwenyewe alitaka kunywa katika klabu hiyo.
Wakati huo Nyerere alikuwa amekwishachaguliwa waziri mkuu wa serikali ya mwanzo ya madaraka ya ndani.
Kuna maudhi mengine aliyoyaona. Kwa mfano, yale yaliomfika Mtanganyika mmoja tajiri mwenye asili ya Kihindi na ambaye Achebe alisema alikua ‘mtu mwema’.
Jamaa huyo alimlalamikia kwamba japokuwa alizaliwa Tanganyika na hakuwa na kwingine pa kukimbilia na ijapokuwa alitoa fedha nyingi za sadaka kuwafadhili wananchi wenzake Wakiafrika, bado hao wenzake hawakumkubali wala hawakuwa wakimuamini. Sababu ilikuwa damu yake ya Kihindi. Ilikuwa kama ya kunguni, ikinuka.
Inasikitisha kwamba ubaguzi aina hiyo bado upo nchini Tanzania ingawa tunajidai kuufumbia macho kana kwamba haupo.
Akiwa Dar es Salaam, Achebe alihudhuria mkutano wa kisiasa uliopangwa kuukosoa uongozi wa Nyerere. Mkutano wenyewe uliongozwa na Bibi Titi Mohamed, ambaye Achebe alimuelezea kuwa ni ‘kiongozi wa ajabu wa tawi la wanawake la TANU’.
Lawama hizo hazikutolewa kwa ukali bali zilitolewa kwa upole mno ukidhania kama vile badala ya kumkosoa Nyerere zilikua na lengo la kumdekeza.
Achebe alishangazwa na hali ya mkutano huo kwani mwanzo mwanzo aliuona kuwa kama uliopwaya akiulinganisha na mikutano ya hadhara ya kisiasa ya kwao Nigeria ambayo ni ya fujo, ghasia na kelele.
Mambo yaligeuka aliponyanyuka Nyerere kuhutubu. Aliposimama Nyerere kujitetea, Achebe alipigwa na bumbuwazi. Licha ya kwamba alimtegemea mkalimani wake kwani hakukijua Kiswahili, hata hivyo alivutiwa na balagha ya kisiasa ya Nyerere, ufasaha wake wa kusema. Na kusema Nyerere akisema, wakati mwingine akinguruma.
Miongoni mwa Watanganyika mashuhuri aliokutana nao Achebe ni Mtwa Mkwawa yaani Chifu Adam Sapi – mjukuu wa Sultan Mkwawa wa Wahehe, na aliyekuwa Spika wa bunge la kwanza la Tanganyika huru.
Achebe alipokewa vizuri alipoalikwa kwenda kunywa chai kwa Chifu Adam Sapi, mtu aliyekuwa mpole na mwenye haya. Siku ya pili alipokuwa Achebe anafunga begi lake kwa safari ya kurudi Dar es Salaam alisikia mtu akipiga hodi kwenye mlango wa chumba chake cha hoteli.
Alipofungua mlango alimkuta Chifu Adam Sapi Mkwawa amesimama akiwa na mshale mdogo wa Kihehe aliomtunukia zawadi.
Mtanganyika mwingine mashuhuri aliyekutana naye Achebe wakati wa ziara yake ya Tanganyika alikuwa mshairi Sheikh Shaaban bin Robert aliyemtembelea nyumbani kwake.
Pamoja na kuwa mshairi, Shaaban Robert alikuwa pia mwandishi wa riwaya, mwandishi wa insha na alitafsiri kwa Kiswahili mkusanyiko wa mashairi ya Omar Khayyam, mshairi wa kale wa Kiajemi ‘Rubaiyat ya Omar Khayyam’. Mkutano wa Shaaban Robert na Achebe ulikuwa wa aina yake kwani Shaaban Robert alizungumza kwa Kiswahili na Achebe kwa Kiingereza.
Ingawa walizungumza sana kuhusu fasihi, Shaaban Robert hakuwahi kuyasoma maandishi ya Achebe na Achebe naye hakuwahi kuyasoma ya Shaaban Robert aliyekuwa akiandika kwa Kiswahili.
Hata hivyo walipoagana, Shaaban Robert alimtunukia Achebe zawadi ya vitabu viwili vya mashairi yake.
Walipokutana kitabu cha kwanza cha Achebe na kilichompa umaarufu mkubwa ‘Things Fall Apart’ kilikuwa bado hakijatafsiriwa kwa Kiswahili. Kitabu hicho cha riwaya kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1958 kimetafsiriwa mara mbili kwa Kiswahili.
Kilitafsiriwa kwanza na Mohamed Mlamali Adam mwaka 1972 na kikapewa jina la ‘Hamkani si Shwari Tena’. Mara ya pili kilitafsiriwa mwaka 1973 na Clement Ndulute na kuitwa ‘Shujaa Okonkwo’.
Mbali na Kiswahili, kitabu hicho kimetafsiriwa pia katika lugha 49 nyingine na kimeibuka kuwa ni kitabu muhimu sana katika ile iitwayo fasihi ya Kiafrika.
Wiki iliyopita wengi walioandika kuhusu maisha ya Achebe walimuelezea kuwa yeye ndiye ‘baba wa fasihi ya Kiafrika’ na wengine walisema kuwa yeye ni ‘babu’ wa fasihi hiyo. Sikubaliani nao.
Sikubaliani nao kwa sababu kabla ya Chinua Achebe kuanza kuchapisha riwaya zake alizoziandika kwa lugha ya Kiingereza, tayari kulikuwako riwaya za waandishi kama akina Amos Tutuola na Cyprian Ekwensi.
Na wala kutomtambua Achebe kuwa baba au babu wa fasihi ya Kiafrika iliyoandikwa kwa Kiingereza hakumvunjii heshima yake. Bado ataendelea kuwa mmoja wa waandishi gwiji wa fasihi ya Kiafrika, msanifu riwaya aliyebuni mtindo wa aina yake wa uandishi wa riwaya uliojikita katika mazingira ya kijamii ya Kiafrika.
Ingawa niliwahi kukutana naye mara kama tatu hivi – zote jijini London, hata hivyo sikuwa nikimjua Chinua Achebe kama nimjuavyo, kwa mfano, Ngũgĩ wa Thiong’o au Nuruddin Farah au Taban Lo Liyong au Abdulrazak Gurnah miongoni mwa waandishi wa Kiafrika wanaoandika kwa Kiingereza (ingawa Ngũgĩ haandiki tena riwaya kwa Kiingereza) au mshairi wa Kiswahili Abdilatif Abdalla au mwandishi wa riwaya za Kiswahili, Adam Shafi – mmoja wa watu walionifungua macho kisiasa.
Pia sijapata kuwa mshabiki wa misimamo yake ya kisiasa hasa msimamo wake wa awali wa kuunga mkono kuzaliwa kwa Jamhuri ya Biafra, jimbo la Kusini-Mashariki mwa Nigeria lililojitenga Mei 30, 1967. Kutangazwa kwa jamhuri hiyo kulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Nigeria vilivyoendelea kuanzia Julai 1967 hadi Januari 1970.
Kwa hakika, nakumbuka niliuponda sana msimamo wake wa kisiasa nilipokuwa nakichambua kitabu chake cha
‘The Trouble With Nigeria’ katika jarida la ‘Africa Events’ mwaka 1984.
Nilimshambulia kwa kutolizingatia suala la tabaka za kijamii katika uchambuzi wake wa siasa za Nigeria.
Juu ya yote hayo, mara zote nilizokutana naye nilizidi kumheshimu kwa unyenyekevu na upole wake. Ni mtu aliyekuwa hana kiburi wala hakuwa akijiona kama alivyo mwandishi mwenzake wa Nigeria, Wole Soyinka. Tena Achebe alikuwa na tabasamu ya sumaku.
Kifo cha Chinua Achebe kimelitia bara la Afrika katika huzuni. Nina hakika kwamba katika pembe au kona moja ya Afrika au miongoni mwa wapenzi wake kifo hicho kimezusha hali ya hamkani na mambo si shwari tena