Vigogo watimuliwa katika kura za Kenya
Imeandikwa na Hassan Mhelela, BBC London.
Makamu wa Rais Moody Awori amepoteza kiti chake cha Funyula, magharibi mwa Kenya, baada ya kushindwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1983 na Dr Paul Otuoma.
Bwana Awori alikuwa miongoni mwa mawaziri kadhaa katika serikali ya Rais Mwai Kibaki ambao tayari wamepigwa teke na wapigaji kura.
Wengine ni mawaziri Mutahi Kagwe wa habari, Paul Sang wa Afya, Musikari Kombo wa serikali za mitaa, na Moses Akaranga wa Huduma za Umma.
Hadi sasa chama cha ODM kimejitosa mbele katika idadi ya viti vya ubunge, kikiwa kimenyakua jumla ya wabunge 53.
Chama cha Rais Kibaki cha PNU hadi sasa kimepata viti 15, huku cha ODM Kenya, kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, kikiwa na viti 2.
Baadhi ya wanasiasa waliopata ushindi mkubwa ni aliyekuwa Makamu wa Rais bwana Musalia Mudavadi wa ODM.
Wengine wanaosherehekea ushindi wao ni James Orengo wa eneo la Ugenya na Dalmas Otieno kutoka Rongo.
Lakini wapigaji kura waliwakataa vigogo wengine kama vile Nicholas Biwott na Waziri Simeon Nyachae.
Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi haijaidhinisha matokeo haya ambayo yanawakilisha asilimia 10 tu ya kura ambazo zimeshahesabiwa.
Katika hesabu za kura ya urais, vuta ni kuvute kati ya Rais Kibaki na mpinzani wake mkali, Bw Odinga ni ya kusisimua.
Wote wawili wamepigiwa kura kwa kiasi kikubwa. Mpinzani mwingine, Kalonzo Musyoka, anaendelea kushikilia nafasi ya tatu, huku matokeo yakionyesha kwamba huenda asizue miujiza kama vile alivyokuwa akiahidi katika kampeni zake.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wametoa wito kwamba muda wa kupiga kura uongezwe kuwezesha wapiga kura wote wapate fursa ya kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Source: BBC