Kabla ya kuendelea, turejelee kauli aliyoitoa Colonel Lionel Dyck, mkurugenzi wa jeshi binafsi la DAG ambaye mkataba wake wa kutoa msaada wa anga pale Msumbiji ulitamatika tarehe 6, April 2021.
View attachment 3004739
Alipohojiwa, alisema kauli hii; "Mungu, wasaidie watu wale."
Akimaanisha watu wa Msumbiji aliowaacha katika tabu. Tabu ambazo hakusimuliwa na mtu bali alizishuhudia yeye mwenyewe katika oparesheni yake nchini humo.
Na sisi pia tunaishi hapa. Eeh Mungu wasaidie watu wale (wa Msumbiji). Lakini pia tunaongezea, atusaidie na sisi ambao tumepakana nao.
Bwana huyu, Lionel Dyck, yeye amekwishaaga nchi hii ya Msumbiji lakini kwenye mioyo ya wananchi mia mbili na ishirini na nane katika mji huu wa Palma, atabaki kuishi milele.
View attachment 3004740
Hawatamsahau namna alivyotumia helikopta zake kuwanusuru na midomo ya bunduki za magaidi ambao walitumwa roho za watu siku hiyo.
Siku ya maafa.
Kwao wanamwona Lionel Dyck na jeshi lake kama malaika.
Helikopta yake iliwabeba, kidogo kidogo, zamu kwa zamu, na kila mara ilipoondoka wakadhani haitokaa ikarudi tena, lakini bado ikarejea na kuwakomba watu kwenda eneo salama huko peninsula ya Afungi.
Pichani ni watalii ambao walikwama kwenye hoteli wakati wa mashambulizi ya Palma yanarindima huko nje.
View attachment 3004741
Kwa kutumia mashuka meupe wakaandika ujumbe 'HELP', na bahati wakaonekana na kuokolewa na helikopta ya DAG.
Hivyo watu hawa, ukiwajumuisha na wale wananchi wa Msumbiji 228, wanakamilisha jumla ya watu 240 waliofanikiwa kuokolewa na oparesheni ya DAG.
Sasa tukiacha kuhangaika na haya matawi ili turudi kwenye mzizi wenyewe, basi hatuna budi kuurejea ule mwaka 2012 kule Mombasa, nchini Kenya.
View attachment 3004743
Katika mwaka huo, August ya tarehe 27, siku ya Jumatatu majira ya asubuhi, sauti ya bunduki inarindima ndani ya jiji la Mombasa na kusababisha taharuki kubwa.
Kwenye zoezi hilo, zilitumwa risasi kumi na nane kwenda ubavu wa kulia (upande wa dereva) wa gari aina ya toyota hiace nyeupe iliyobeba familia nzima ndani yake.
View attachment 3004744
Risasi hizo zilikuwa zimeagizwa kitu kimoja tu, kuja na roho ya bwana Aboud Rogo aliyekuwa ameketi katika usukani. Na kweli risasi zikafanikiwa.
Aboud Rogo anafariki papo hapo, wengine wote wakibakia salama salmin mbali na mkewe, bi. Haniya, aliyeishia kupata jeraha la risasi mguuni.
View attachment 3004745
Cha kushangaza siku hiyo, bwana Rogo alikuwa yu njiani akimpeleka mkewe hospitali kwani alikuwa na maradhi, ila ajabu akaishia kupelekwa yeye hospitali akiwa marehemu.
Kifo hiki cha Rogo kinakuja muda si mrefu, takribani wiki mbili zilizopita, baada ya kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (UN) na nchi ya Marekani kwa kutuhumiwa kuwa na mahusiano na Al-shabab ya huko Somalia.
View attachment 3004746
Bwana Rogo ambaye alikuwa muumin wa itikadi kali na mmoja wa viongozi wa kikundi cha Al-hijra kinachoaminika kuwa 'wing' ya Al-shabab nchini Kenya, alinyooshewa vidole na UN kwa kusaidia Al-shabab kwenye mambo matatu:
'Funding, recruiting and logistics'.
Kwa mujibu wa UN, bwana Rogo alikuwa akiifadhili kundi hilo la kigaidi kwa michango mbalimbali ya watu, alikuwa akisaidia kutafuta vijana wa kujiunga nalo na pia alikuwa anasaidia kuwasafirisha vijana hao kufika Somalia.
View attachment 3004747
Na kifo hiki cha Rogo hakikuwa cha kwanza wala cha mwisho kwa watu waliokuwa wanafanana naye kaliba. Wote waliuawa kwa mtindo huu huu. Wanapigwa risasi na watu wasiojulikana na 'wasiokamatikana'.
View attachment 3004748
Sasa wafuasi hawa wa Rogo, kwa mujibu wa ripoti ya Nation Africa ya Kenya, ndio mabwana wanaoleta matata kule Msumbiji. Wafuasi hao walitawanyika na kusambaa maeneo mbalimbali baada ya vifo vya wakubwa wao waliowashika mkono.
Hivyo kwa maelezo haya, na yale ya kamanda Sirro kusema magaidi wale waliovuka mpaka kutoka Msumbiji na kuvamia Mtwara ni mtandao ulioanzia MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji), yanatosha kutueleza mtandao huo haukuanzia hapa nchini.
Ulianzia huko Kenya, ukaja kwetu kisha ukaelekea Msumbiji. Kote huko unapopita, unapokelewa na wakazi ambao wengine kwa hali zao, wanashawishika kujiunga nao wakiamini ni njia ya kupambana na madhila yanayowasibu.
Watu hawa waliobeba chuki, ni rahisi kufanyiwa 'brainwashing' kwa kutumia mwamvuli wa imani. Baada ya hapo wanageuka kuwa watu wapya kabisa usiowajua.
View attachment 3004750
Wanabeba silaha kuingia ulingoni na ukikutana nao , my friend, usitegemee watakukumbuka ati wewe ulikuwa jirani yake, ulicheza naye mdako utotoni, ulikimbizana naye kwenye kombolela na kushikana kidali.
Kama bado unautaka ugali, basi tupa hiyo miguu kadiri uwezavyo, hata ukiweza kupaa angani basi wewe paa, utaenda kujiuliza uliwezaje ukiwa upo chini ya kitanda.
Mfano mzuri wa hii kesi ni vijana wawili; Nuro na Abu Dardai Jongo kule nchini Msumbiji ambao leo hii ni vinara wa mauaji katika kikundi hiki cha Ansar al-sunna.
View attachment 3004752
(Nuro Pichani)
Nuro alikuwa mfanyabiashara wa samaki hapo Cabo Delgado. Mtu poa na mcheshi. Akaja akapotea isijulikane kaenda wapi. Kuja kuonekana tena, si yule wa zamani. Anachinja watu kama utani.
View attachment 3004757
Abu Dardai Jongo yeye alikuwa na pikipiki. Alikuwa anfanya kazi ya kusafirisha watu toka mto Ruvuma mpaka Montepuez. Kitambo fulani, akaenda Macomia. Aliporejea, wenzake wanasema hakuwa tena yule Abu walokuwa wanamfahamu.
View attachment 3004759
(Abu Jongo pichani)
Haikupita muda akapotea moja kwa moja.
Tukirudi kwa jamii ya watu wanaoishi mkoa wa Pwani, mathalani Kibiti, Mkuranga na Rufiji, hamna asiyejua wengi wao hali ni dhalili. Pangu pakavu tia mchuzi.
Shughuli wanazotegemea ni kuchuma rasilimali zinazowazunguka kwa kutengeneza na kuuza mkaa, kukata na kuuza kuni na magogo ya mbao pasipo kusahau kilimo.
Hivyo watu hawa wanapokumbana na kodi kandamizi, ushuru mlima na tozo rundo kuanzia kwa maafisa wa serikali za mtaa, maafisa misitu na rasilimali mpaka polisi, huzaa chuki.
Chuki ambayo huja kuwa mtaji kwa wadhalimu.
Tunakumbuka mwaka 2013 namna gani watu wa Kibiti walifanya vurugu kubwa mpaka kufunga barabara, ikabidi IGP atoe kauli.
View attachment 3004760
Na pia tunakumbuka namna gani tulianza kuokota miili ya watu, wakilengwa haswa wafanyakazi wa serikali mathalani watu wa serikali za mitaa na polisi.
Ilitumika nguvu kubwa kuwazima mabwana hawa. Ilibidi watu wafe, hata wale ambao ni ndugu zetu, ili wengi wetu tubaki salama.
View attachment 3004761
Lakini ni dhahiri oparesheni hii (MKIRU) haikumaliza hawa 'mabwana' wote , ndo' wengine wanakimbilia Msumbiji wanapoenda kukutana na 'locals' ambao wanaungana nao na taratibu wanaanza kukua.
Wakati huo intelijensia ya Msumbiji iko wapi? Wamelala, udenda unatiririka mpaka masikioni.
Walidharau mwiba, guu likaota tende.
Maana kabla ya kufikia shambulizi lile la kwanza la Ansar al-sunna mwaka 2017 katika mji wa Mocimboa de Praia, tayari kuna matukio matatu nyuma yalishatengeneza 'alarm' ya hatari.
View attachment 3004762
Mwaka 2015, meya wa mji wa Mocimboa de Praia alinukuliwa akisema kuna tetesi za kundi la Al-shabab ku-recruit vijana wa mji huu na kitu hiki ni hatari kwa usalama.
Kipi kilifanyika? Hamna.
Mwaka 2016, kwa kupitia 'Nacedje Community Radio', mkuu wa shule moja ndani ya jimbo hili la Cabo Delgado anasikika akilalama kupungua kwa kasi kwa idadi ya wanafunzi shuleni, wanafunzi hao wakisema shule haina tija.
View attachment 3004763
Walikuwa wanaenda wapi? Hamna anayejua.
Viongozi wa dini ya kiislamu katika maeneo kadhaa, wakaripoti kuna mafundisho ya tofauti yanayozunguka mtaani, mafundisho ambayo ni kinyume na dini ya kiislamu, mfano watu kusali wakiwa na viatu.
Nani aliyekuwa anayatoa? Hamna anayejua.
View attachment 3004765
Wanakuja kutoa macho tarehe 5, Oktoba 2017. Ansar al-sunna wanakuja katika miili yao kamili, sio story tena. Wanamwaga mvua ya vyuma kwenye vituo vitatu vya polisi na kufungua rasmi mchuano mkali ambao unadumu mpaka leo hii 2024.
View attachment 3004766
Sio story, idadi kubwa ya wahusika wa kundi hili ni watu wa hapahapa Msumbiji. Wazawa. Hawa ndo' wale wanaozungumza kireno na kimwani - lugha ya pwani ya Cabo Delgado.
Kamanda Inacio Dina, msemaji wa jeshi la polisi, alikwishalisema hili.
Na hata kwenye ile ripoti ya gazeti la serikali ya Msumbiji la tarehe 17 April 2024, majuzi tu hapa, unaona ni namna gani watu wa Msumbiji walivyotawala orodha nzima ya washukiwa wa ugaidi isipokuwa watu wawili tu ambao ni watanzania.
View attachment 3004767
Lakini zaidi ripoti ile, inaacha swali muhimu juu ya ukwasi walionao hawa Ansar al-sunna pale unaposoma maelezo ya mshukiwa Ismael Sefo Sante (23), mfanyakazi wa kampuni ya usafirishaji ya Quimenci nchini Msumbiji.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, mshukiwa mwingine, Ally Yusuf Liwangwa au kwa jina maarufu Big Ally (47), mtanzania mfanyabiashara kutoka Dar, aliwasiliana na Ismael Sefo Sante na kumpatia 'deal' la kutafuta vijana hamsini kwa ajili ya kujiunga na kundi la Ansar al-sunna.
Deal lililoweka mezani dau la USD 15,600.
Kwa pesa za madafu ni milioni arobaini na laki tano sitini. Hapo kwenye ripoti zingine, hususani mahojiano yalofanywa na BBC Eye of Africa, mhojiwaji anasema pesa hiyo ni ya kuleta watu wawili tu kwenye kundi.
Just imagine.
View attachment 3004768
Hizi pesa zote wanatoa wapi? Kuna wanaosema ni funding toka kundi la Islamic state, lakini ni kwa maslahi gani? Wengine wanasema ni mali wanazokwapua kwenye uvamizi wao huku na kule.
Hamna anayejua maana hamna rekodi yeyote ya miamala yao. Yote haya yanafanyika kwa kificho.
Lakini swala lililo wazi hapa ni sababu ya wao kuweka makazi na kung'ang'ania hapa jimboni Cabo Delgado. Hili lina sababu nzuri na ya kusisimua kwani linatosha kwa kila 'angle'.
Kwenye ripoti ya maendeleo ya mwaka 2017, Msumbiji inaripotiwa kuwa na asilimia 46.1% ya watu wanaoishi chini ya dola moja kwa siku. Ukosefu wa ajira kwa vijana ni 41.7% na ni 25% pekee ya watu nchi nzima ndo' wanapata huduma ya umeme.
Hali ni mbaya zaidi jimbo la Cabo Delgado.
View attachment 3004769
Umaskini umekithiri kila pahali.
Watu wanautafuta mkate kwenye shughuli za uvuvi, kilimo na uchimbaji mdogo wa madini ya Ruby kwa vizazi na vizazi. Huko migodini Montepuez, vijana wengi wanajiajiri na walau wanapata chochote kitu.
Lakini baadae, katika kuongeza chumvi kwenye kidonda, serikali inawaondosha vijana hawa na mradi wanapewa kampuni kubwa ya Gemfields hivyo vijana wengi wanabakia bila ya kazi.
View attachment 3004771
Mwaka 2010, katika pwani ya mji wa Palma, inagundulikana reserve kubwa ya gesi asilia, reserve ambayo ni ya tatu kwa ukubwa barani Afrika.
Mali hiyo inavutia kampuni ya marekani, ANADARKO, ambao mwaka 2017 wanaanza kuchora mkakati wa kuhamisha watu ilikupisha mradi huu mkubwa lakini baadae kampuni ya kifaransa ya TotalEnergies inanunua hisa hii ya Anadarko kwenye uwekezaji wa gesi hapa Msumbiji kwa dola bilioni 3.
View attachment 3004773
Mradi unakuwa mikononi mwao.
Sasa rasilimali zote hizi ndani ya eneo hili, bado wananchi wanahaha kwa umaskini uliokithiri huku serikali ikiwatupa mkono.
Hapa ndo' Ansar al-sunna wanapopenyeza utambi wao. Wanashawishi watu hawa, na kama ganda la ndizi, wanawachota watu wakitumia mgongo wa imani. Vijana wanajiunga wakiamini hii ni njia sahihi ya kujikwamua.
Kwa lugha tamu ya ushawishi, wanawachota wafuasi na kukua taratibu huku macho yao yakiwa kwenye hizi rasilimali za Cabo Delgado.
Kuanzia kwenye uchumi HALALI wa gesi na madini kama vile Ruby na pia Graphite inayotumika kwenye utengenezaji wa battery za vyombo vya moto na simu za mkononi mpaka kwenye uchumi HARAMU wa pwani unaokua kwa sababu ya uingizwaji wa madawa (heroin) kutoka Asia.
View attachment 3004774
Uchumi huo unakadiriwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni mia moja.
View attachment 3004775
Mpenzi msomaji, mpaka kufikia hapa naweza sema haya ya nyuma yanatosha. Hata na hivyo hatuwezi kuyamaliza.
Turudi sasa mwezi July 2021, ambapo jumuiya ya SADC, Tanzania ikiwemo ndani yake, inatuma rasmi jeshi lake linaloungana na jeshi la Rwanda kuwakabili hawa Ansar al-sunna.
View attachment 3004777
Oparesheni hii inaitwa SAMIM (SADC Mission in Mozambique).
Je imefanyikaje na imefikia wapi? Na maslahi ya Rwanda yako wapi katika kuingiza jeshi lake hapa tena kwa miguu yote miwili?
Kwanini South Africa wamejitoa?
Nitakuja na uzi wa mwisho. Thanks.