Wana JF,
Imefikia wakati ambapo maamuzi machungu inabidi yafanyike hapa JF na kama itawezekana kwenye media za nyumbani. Kwa zaidi ya wiki moja sasa mimi na baadhi ya wana JF hapa tumekuwa tunafanya uchunguzi kuhusu uhakika wa habari za kifo cha aliyekuwa Gavana wa benki kuu - Dr Ballali. Wakati haya yakiendelea, mimi nilizikubali na kuziamini (msisitizo zaidi kwenye imani) habari za kifo cha Ballali ambazo ziliwekwa hapa na Invisible.
Kulingana na taarifa, vyanzo vya habari, mipango ya mazishi, sala na maombi kwa marehemu ambavyo vyote viliwekwa hapa JF, imani yangu ilizidi kukua na kupelekea uamuzi wa kukubali kuwa Ballali amekufa. Hata hivyo, uchunguzi wa siri unaonyesha utata na usiri mkubwa sana kwenye ugonjwa na hatimaye kifo cha Ballali. Kila nafasi na gharama iliyotumika kupata hii habari imefikia kwenye mwisho mfu (dead end) na mchanganyo ambao haustahili kuwepo hapa.
Binafsi niliahidi kuwa nitaomba msamaha hapa JF kama itathibitishwa kwangu kuwa Ballali yuko hai. Naomba sasa niseme kuwa sina sababu ya kuthibitishiwa kuwa Ballali yuko hai ili niombe msamaha kwa kuamini kifo cha Ballali. Pamoja na kuwa sina hakika kwa sasa kuwa Ballali yuko hai, lakini pia ni vyema ikiwa wazi hapa kuwa sina hakika (na sikufanikiwa kupata uhakika kwa asilimia mia moja) kuwa Ballali amekufa. Juhudi zote za kutafuta hili na lile kuhusu kifo cha Ballali zinafikia mwisho na mlango mzito sana wa kufungua ili kujua ukweli. Na kwa hili, naomba msamaha kwa wana JF na watanzania.
Nimekuwa natumia sana neno imani (kuwa na hakika na yasioonekana) katika hii issue ya Ballali. Niliamini kifo cha Ballali na imeshindikana kupata uhakika wa kutosha kufikia hitimisho la kifo chake. Kwa hili, naomba msamaha na kusema hapa kuwa sina imani tena kuwa Ballali amekufa. Nafasi nyingi sana zilijaribu kutolewa kwa Ballali kutoa story yake kuhusu yote yaliyotokea BoT. Kwa sasa kuna mengi yamepatikana na yatawekwa hapa JF kama ilivyo kawaida ya kila miziki inayopatikana hapa JF. Ila katika hili la kifo cha Ballali, naomba niseme wazi kuwa sina imani tena kama amekufa na kwa sasa ninapinga habari zote za kifo cha Ballali.
Kama vile ambavyo nilisisitiza kutolazimisha wasomaji hapa na watanzania walio nyumbani kuamini habari za kifo cha Ballali, sitafanya kinyume chake na kulazimisha watu kutokuamini kifo chake. Ninachosema hapa ni kuwa, safari zote nilizofanya kwenda Boston na baadaye DC kwenye ibada ya mazishi hazikunipa uthibitisho wowote wa kutosha kuwa Ballali yuko hai au amekufa. Nitaacha hili kwa wasomaji na watanzania kuamua waamini lipi kuhusu kifo cha Ballali. Ninachosema hapa ni kuwa, kuna juhudi kubwa sana zinafanywa na watu wakubwa kabisa katika serikali ya Tanzania na ya hapa Marekani ili habari nzima ya Ballali ibakie kuwa utata.
Hata hivyo, ningependa kuwakumbusha wale wanaodhani kuwa kifo au kupotea kwa Ballali kutapelekea hii case kuisha wajiandae kwa safari nyingine. Inajulikana kabisa kuwa Mramba, Mgonja na viongozi wakubwa serikalini kwa pamoja au kwa nyakati tofauti waliiidhinisha malipo toka benki kuu. Iko wazi kuwa auditing ya Deloitte ilisitishwa baada ya kugundua mambo mengi ambayo serikali haikutaka yajulikane. Inafahamika kabisa kuwa wahusika wa wizi wa BoT ni wengi sana na Ballali ni kipisi tu cha mkuyu mzima. Inafahamika pia wizi wa BoT sio wa EPA peke yake, kuna mengine mengi ambayo hayajafanyiwa uchunguzi.
Kupotea au kufa kwa Ballali sio mwisho wa huu mchezo na hii movie. Kwa sasa ndio mwanzo sehemu ya pili ya hii series inaandaliwa na wengine wote kwa kuanzia na mzee wa kula nyasi (Mramba), Mgonja na wenzake wajiandae kwa sehemu ya pili ambayo ndio kwa sasa wametia mafuta kwenye moto.
Huu ni mwanzo tu.....