Nimesikitishwa sana na waandishi wa magazeti ya leo walipo ibuka na Vichwa vya habari Lulu kortini kwa kumuua Kanumba je wana uhakika gani kuwa amehusika moja kwa moja na mauaji ya The Great? Nipashe kama mna data za uhakika Lulu Kamuua Kanumba mwageni Dataaaa
Lulu kortini kwa kumuua Kanumba
Polisi wamficha, wakwepa waandishi
Ajifunika ushungi, avaa kandambili
Msanii wa uigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta (18), maarufu kama Lulu, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba (28).
Tukio la msanii huyo kufikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka lilikuwa kama mchezo wa filamu baada ya polisi kufanya siri na hata kugombana na baadhi ya waandishi wa habari waliotaka kuingia katika chumba cha mahakama kufuatilia kesi hiyo.
Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Augustina Mmbando.
Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu alimtaka Lulu kutojibu chochote kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua Kanumba.
Kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), Lulu hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Hata hivyo, mara upelelezi utakapokamilika, kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusikilizwa.
Kaganda alidai upelelezi bado haujakamilika, hivyo akaiomba mahakama kupanga tarehe ya kuitajwa kwa kesi hiyo.
Hakimu Mmbando alisema mshtakiwa atakaa mahabusu hadi Aprili 23, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa.
Wakati mshtakiwa huyo akisomewa hati ya mashtaka alidai mahakamani hapo kwamba, umri wake sio miaka (18) kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka bali ana miaka (17).
Pia wakati mashtaka yanasomwa hali mahakamani hapo ilikuwa shwari, huku watu wengine wakinongona bila kuwa na uhakika kuhusu msanii huyo kufikishwa mahakamani kutokana na kutoonekana kwa wanafamilia wake na watu wa karibu.
Mazingira ya Lulu kufikishwa mahakamani hapo yalikuwa kama mchezo wa kuigiza kutokana na jeshi la polisi kufanya kuwa siri kubwa.
Gari aina ya Suzuki Vitara liliingia katika viunga vya mahakama hiyo muda ambao haukufahamika likiwa na makachero wa Jeshi la Polisi wanne, wanawake wawili na wanaume wawili na mshtakiwa.
Lilifuatiwa na gari lingine aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa na askari polisi saba waliovaa sare za jeshi hilo wakiwa na silaha.
Hata hivyo, baada ya muda NIPASHE kupitia chanzo chake ilipata taarifa ya msanii huyo kufikishwa katika viunga vya mahakama hiyo na kwamba jalada la kesi yake lilikuwa limeshapangiwa hakimu.
Hatua hiyo ilisababisha waandishi wa habari za mahakama kujipanga na kuweka lindo katika kila kona ya jengo la mahakama hiyo huku wengine wakiwa kwenye mlango wa kutokea mahabusu, kwenye korido za milango ya kuingia katika ofisi za mahakimu.
Hata hivyo, kundi la waandishi waliokaa katika korido ya ghorofa ya kwanza kuelekea kwenye ofisi za mahakimu, ghafla saa 5:20 asubuhi walifanikiwa kumuona mshtakiwa huyo akiwa katikati ya makachero wanawake wawili na nyuma wanaume wawili akiwa amejifunika ushungi wa rangi ya udhurungi, gauni kubwa maarufu kama dira la rangi ya njano na kandambili za rangi nyekundu.
Waandishi hao walikimbilia msafara huo uliokuwa na askari wanne pamoja na mshtakiwa, lakini kabla ya kuingia chumba cha hakimu, askari aliyekuwa ameshika simu ya upepo mkononi aliwazuia waandishi kuingia.
Hali hiyo ilisababisha majibishano ya muda na mwishowe alibadili nia ya kuzuia wanahabari hao kufanya kazi yao.
Mshtakiwa alisomewa mashtaka yake na baadaye alipitishwa njia ya mlango wa nyuma hadi kwenye gari aina ya Suzuki Vitara yenye namba za usajili T848 BNV yenye vioo visivyoonyesha ndani (tinted).
Ingawa gari hilo lilikuwa na namba za kirais, kwenye vioo liliandikwa namba PT 2565, na iliondoka mahakamani hapo kwa kasi kumpeleka mshtakiwa mahabusu ya Segerea kusubiri upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
Mapema jana saa 3:35 asubuhi, NIPASHE ilizungumza kwa njia ya simu na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela kuhusu hatima ya kufikishwa mahakamani kwa msanii huyo, mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:
NIPASHE: Shikamoo afande.
Kamanda Kenyela: Marahaba. Nipigie baadaye niko kwenye kikao.
NIPASHE: Sawa afande. Lakini nilitaka kujua kama Lulu atapelekwa mahakamani leo (jana) na itakuwa mahakama gani Kinondoni au Kisutu?
Kamanda Kenyela: Mmmh! Kwa kweli bado uchunguzi unaendelea. Hivyo, jalada liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).
NIPASHE: Ahsante afande. Shida yangu ilikuwa hiyo tu endelea na ujenzi wa Taifa.
Kamanda Kenyela: Nashukuru sana mwandishi.
Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi Aprili 7, mwaka huu, baada ya kudaiwa kutokea ugomvi kati yake na Lulu.
Maelfu ya watu, wakiwamo mawaziri, wabunge, viongozi wa siasa, vyama vya kiraia, wasanii wenzake na wananchi wa kawaida, walijitokeza katika msiba huo nyumbani kwake, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam na kwenye shughuli za kumuaga viwanja wa Leaders Club na kuuzika mwili wake katika makaburi ya Kinondoni.
Mazishi hayo yaliongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
CHANZO: NIPASHE