CCM na watawala waovu wameendelea na uovu wao dhidi ya haki. Anachofanyiwa Lisu na polisi, magereza na mahakimu na majaji mvhongo, ni mwendelezo wa uovu ule ule aliofanyiwa Ali Kibao, Mdude Nyagali, Soka na wengine wengi. Ni mwendelezo wa uovu ule aliofanyiwa Baba wa Kiroho na Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Father Kitima.
Hivi kuna mtu anaweza kusimama hadharani na kusema Ali Kibao, au Mdude au Soka walifanya kosa gani, hadi kuwaua, zaidi ya ukweli kuwa waliokuwa wakosoaji wa uovu wa watawala?
Hivi kuna mtu anaweza kusimama na kusema Fr. Dr. Kitima alikuwa ana hatia yoyote ya kumfanya ashambuliwe kwa lengo la kumwua, zaidi ya kitendo chake cha kukemea kwa nguvu zote uporwaji wa bandari zetu?
Hawa watu ni waovu wanaoamua kuwanyamazisha wote wanaokemea uovu wao, wanataka wote waungane nao kwenye uovu wao, anayekemea basi hugeuka adui yao. Lakini kuna faida ani kuwa rafiki wa watu waovu kama wewe siyo mwovu?
Yaani Lisu kusema kuwa tutakinukisha au tutafanya uasi, eti ndiyo uhaini!!
Ikumbukwe Lisu aliyasema hayo akiwa kwenye kikao cha ndani akiijibu barua ya wale waliojiita G55. Lisu alisema, "Nimeyasoma madai yao, wanasema eti tusiposhiriki uchaguzi, itakuwa ni uasi, ni kweli utakuwa ni uasi dhidi ya sheria na mifumo gandamizi inayosimamia uchaguzi. Uasi wa namna hiyo tutaufanya. Hatutashiriki uchaguzi kwa sheria hizi gandamizi, tutakinukisha, tutakinukisha kweli kweli"
Halafu kuna watu wendawazimu, wenye dhamira zao chafu, wanaamini wanaweza kuwapata watu punguani watakaoamini maneno hayo ya Lisu ndiyo ya kupindua Serikali!!
Kwa namna nchi inavyokwenda, ni lazima tukubali kuwa Taifa letu lipo kwenye laana ya kuwa chini ya watu waliojaa dhuluma, wasiopenda haki, ambao kuteka, kuua, kuumiza watu, kuwabambikia watu kesi, ndiyo nyenzo zao za kubakia madarakani. Uchaguzi unaitishwa kwa lengo la kubariki uovu wao na siyo kwaajili ya kuwapa wananchi nafasi ya kuamua nane wawaongoze.
Vita vya uhuru vilikuwa ni rahisi kuliko vita hii ya kuitafuta haki. Kwa sababu wakati wa ukoloni, adui yetu alikuwa anajulikana na kuonekana dhahiri, LAKINI vita hii ya dhuluma dhidi ya wananchi, ni ngumu sana, kwa sababu maadui zetu wanafanana na sisi, kuanzia rangi za ngozi, na muda mwingi wanafanya hadaa kutuaminisha ni wenzetu wanaopigania maslahi yetu kumbe ni maadui wabaya kuliko wale wa wakati wa ukoloni.
Tuamke, tuuvae weledi na utu mpya. Adui ni adui tu, haijalishi ana rangi kama ya kwako, anaongea lugha kama ya kwako, anajifanya muumini kama wewe au anakurushia sehemu ya pesa anayowapora ninyi wenyewe.
Tunaomba Mungu wetu utujaze werevu sisi watu wako ili akili zetu zipate kutoka gizani, na kuwatambua maadui zetu wanaotutumia dhidi ya wenzetu.