Rais Mstaafu Kikwete hata asipoambiwa na Magufuli anakila sababu ya kuondoa hofu.
Kwa mujibu wa ibara ya 46 ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema kwamba Rais akiwa madarakani hawezi kushitakiwa kwa makosa ya jinai wala madai kuhusiana na jambo lolote ambalo Rais alilifanya ama kabla ya kushika kiti cha urais au baada.
Na kama Kesi ilikuwa mahakamani ikimhusu Rais toka mwanzo mara tu mtu huyu anapokuwa Rais kesi hiyo inatakiwa isimame.
Makosa ya jinai ni kama mauaji, wizi, ubakaji nk. wakati makosa ya madai ni kama kutolipa deni, kuvunja mkataba, ugoni nk.
Lakini katiba inatoa mwanya wa kumshitaki Rais kwa makosa ya madai mfano Rais hajalipa deni lako na unataka kumshtaki unatakiwa umtumie notisi mwezi mmoja kabla ya kufungua kesi ukijitambulisha jina lako na anuani yako na ueleze unataka kumshtaki kwa kosa gani.
Hii ni ili kama anaweza akayamaliza ayamalize kabla ya kwenda mahakamani.
Kuhusu Rais Mstaafu ibara hiyohiyo ya 46(3) inasema kama Rais alimaliza muda wake wa Urais kwa njia ya kawaida (hakuondolewa madarakani na bunge) basi hakuna mashitaka yoyote yatakayofunguliwa mahakamani dhidi ya mtu aliyekuwa Rais kwa jambo lolote alilolifanya akiwa madarakani kama Rais.
Na hata kama sheria na katiba ikibadilishwa kuondoa kinga ya kushtakiwa kwa Marais wastaafu sheria hiyo mpya haiwezi kumgusa Rais mstaafu wa awamu ya nne na waliomtangulia maana sheria hufanya kazi kwenda mbele ikianzia pale ilipotungwa hairudi nyuma. ( The law does not operate retrospectively).
Hivyo Marais wastaafu wanatakiwa wawe na amani tu hata wasipoambiwa na Rais Magufuli.