Kama wewe ndiye Mungu mwenyewe na unayodai ni ya "kweli kabisa", basi kutokana na huo "ukweli kabisa" wewe ni Mungu. Ila siwezi kuthibitisha kuwa upo au haupo, isipokuwa tu kutokana na wewe kusema "ukweli kabisa" na "ukweli mtupu" na "usio na chembe ya uwongo", basi kwa msingi huo naamini wewe ni Mungu. Kwa mantiki hiyo, kama unachosema siyo "ukweli kabisa" na wewe unajua "siyo Mungu kabisa" na unachosema ni "uwongo mtupu" katika hayo unayoyasema, basi imani yangu ni ya kimakosa maana umeniaminisha kitu kisicho kweli na kisicho kuwepo. Kuna siku niliwahi kusema kwamba kila mmoja wetu ana imani. Nikatoa mfano kwamba ukitoka mfano Dar es Salaam kwenda Dodoma na kuiacha familia yako Dar es Salaam, ukifika Dodoma na kupiga simu kuwajulia hali nyumbani, ina maana unaamini kwamba familia yako - mke na watoto - uliowaacha nyumbani ni wazima/hai. Kama usingekuwa unaamini kuwa ni wazima/hai usingeweza kuwapigia simu. Kwa sababu huenda mara tu ulipotoka nyumbani walivamiwa na kuuliwa au moto ulizuka ukaunguza nyumba na wote wakafariki kwenye hiyo ajali ya moto. Ungeamini hivyo, basi ungerudi nyumbani kwenye msiba na hata wakati wa kurudi, ungerudi kwa kuamini kuwa njia/barabara uliyopita bado iko vilevile ulivyoiacha na ndiyo maana unaitumia tena na hata nyumbani kwako bado ni mtaa fulani, wilaya fulani na kama usingekuwa una hiyo imani basi usingeweza kurudi kwa maana kwa kuwepo kwako Dodoma huwezi kujua kinachoendelea nyumbani kwako Dar es Salaam.