Sura ya 12 inaendelea.
Siku za Jumatano, Ijumaa na Jumapili zilikuwa siku za mikutano kwenye Hekalu la Detroit lililoitwa Hekalu Namba Moja, lilikuwa ni dogo ukilinganisha na mengine. Karibu na hekalu hilo ambalo kihalisi lilikuwa tu ni fremu ya duka tu, kulikuwa na machinjio tatu za nguruwe. Kelele za nguruwe wakichinjwa zilisikika wakati wa mikutano yetu ya Jumatano na Ijumaa. Naelezea tu jinsi Waislamu tulivyokuwa miaka ya 1950 mwanzoni. Hekalu Namba Moja lilikuwa kwenye nyumba namba 1470 katika mtaa wa Frederick. Nadhani Hekalu la kwanza kuanzishwa, lilianzishwa mwaka 1931 na W. D. Fard huko Detroit, Michigan. Sijawahi ona Wakristo weusi wakijiendesha kama walivyofanya Waislamu, iwe mmoja mmoja au familia nzima. Wanaume walivalia nadhifu.
Wanawake walivaa magauni, bila kupaka vipodozi na walifunika vichwa vyao kwa vitambaa. Watoto walikuwa ni wenye adabu, si kwa watu wazima tu bali hata kwa watoto wenzao. Sikuwhi kuota kuona kitu kama kile kwa watu weusi, watu waliojifunza kujivunia weusi wao, waliojifunza kupenda weusi wengine badala ya kuwaonea wivu na kuwashuku. Niliguswa sana na jinsi wanaume weusi walivyosalimiana kwa mikono huku wakitabasamu, wakifurahi kukutana tena. Wanawake wa Kiislamu, waliiolewa na waseja walipewa heshima ambayo sijawahi ona watu weusi wakiwapa wanawake wao, na hilo lilinistaajabisha sana. Salamu zote zilikuwa za bashasha na zilizojaa heshima: “Ndugu”. . . “Dada”. . . “bibi”. . . “Bwana.” Hata watoto walitumia maneno haya walipoongea na watoto wenzao. Ilipendeza sana. Lemuel Hassan alikuwa ndiye Imam wa Hekalu Namba Moja. “As-Salaikum” alitusalimia. “Wa-Salaikum” tulijibu. Imam Lemuel alisimama karibu na ubao. Juu ya ubao kulikuwa kumechorwa kwa rangi—upande mmoja ilichorwa Bendera ya Marekani na chini yake maneno “Utumwa, Mateso na Kifo,” yakifuatiwa na neno “Ukristo” pamoja na alama ya Msalaba. Pembeni ya Msalaba kulikuwa na picha ya mtu mweusi akiwa amenyongwa mtini. Upande mwingine ilichorwa tuliyofundishwa kuwa ni bendera ya Uislamu, mwezi na nyota na maneno “Uislamu: Uhuru, haki, Usawa,” na chini yake “Nani ataokoka vita ya Armageddon?” Imam Lemuel alifundisha mafundisho ya Elijah Muhammad kwa zaidi ya saa moja. Nilisikiliza kwa makini nikimeza kila neno na ishara za Imam Lemuel. Mara kwa mara alifafanua zaidi kwa kuandika maneno muhimu kwa chaki ubaoni. Niliona ni ajabu kwa hekalu letu dogo kuwa na viti wazi. Nilimwambia kaka yangu Wilfred kuwa hakutakiwi kuwa na viti wazi wakati mitaa imejaa ndugu na dada zetu weusi walichotwa akili, wakinywa, kucheza dansi, kutukana, kupigana na kutumia madawa—mambo ambayo bwana Elijah
Muhammad ametufundisha kuwa yanachangia kuwafanya watu weusi waendelee kuwa chini ya mzungu. Kutokana na nilivyoona, mtazamo juu ya kutafuta waumini wapya hekaluni pale haukuwa chanya kabisa. Ilikuwa kwamba “Allah atatuletea” Waislamu wengine. Binafsi niliwaza kuwa Allah atakuwa na mtazamo kuwasaidia zaidi wale wanaojisaidia. Nimeishi kwenye maeneo ya maghetto kwa miaka mingi; niliwafahamu vyema watu weusi walioishi maeneo hayo. Iwe ni Harlem au Detroit, hawana tofauti. Nilisema kuwa sikubaliani na mtazamo huo, na kwamba tunatakiwa kutoka kwenda mtaani na kuwaleta wengi kwenye Uislamu. Kama unavyojua, maisha yangu yote nilikuwa mwanaharakati, sikuwa mtu wa subira. Kaka yangu Wilfred alinishauri kuwa na subira. Niliweza kuwa na subira kirahisi kwa sababu nilitarajia kuonana na mtu aliyeitwa “Mtume,” Elijah Muhammad mwenyewe.
Leo hii nina miadi mingi ya kukutana na watu maarufu duniani, na baadhi yao ni viongozi wa nchi. Lakini sijawahi kuwa na shauku ya kukutana na mtu kama Jumapili ile ya kuamkia Sikukuu ya wafanyakazi wa Marekani ya mwaka 1952. Waislamu wa Detroit walikuwa na safari, nafikiri yalikuwa kama magari kumi—kwenda Chicago kwenye Hekalu Namba Mbili, kumsikiliza Elijah Muhammad. Toka utoto sijawahi kuwa na shangwe kama tulivyokuwa tukiondoka na gari ya Wilfred kuelekea Chicago. Kwenye makusanyiko makubwa ya Waislamu nilikuja kuona, kusikia na makumi elfu ya watu weusi wakishangilia, lakini mchana
wa Jumapili ile mahekalu yetu mawili madogo yalipokusanyika-labda Waislamu mia mbili hivi, Wachicago wakitusalimu na kutukaribisha wa kutoka Detroit, nilipatwa na hisia ambazo sijawahi kuzipata tena. Akili yangu haikujiandaa kabisa kukutana ana kwa ana na Elijah Muhammad. Alipanda jukwaani akitokea nyuma ya Hekalu. Mtu mwenye umbo dogo, rangi ya kahawia na sura ya upole ambaye nilizoea kumuona kwenye picha alikuwa anatembea kuelekea jukwaani huku akiwa amezungukwa na Fruit of Islam(walinzi wa matunda ya Uislamu.) Ukiwalinganisha nao, Mtume alionekana dhaifu na mduchu.
Wote, yeye na walinzi walivaa suti nyeusi, mashati meupe na tai za kipepeo. Mtume alikuwa amevaa baraghashia iliyopambwa kwa dhahabu. Nilimkodolea macho mtu yule mkuu aliyetumia muda wake kuniandikia barua nilipokuwa mfungwa ambaye hakumfahamu hata kidogo. Mtu ambaye niliambiwa kuwa ametumia miaka yake akitaabika na kujitolea kutuongoza watu weusi kwa sababu anatupenda sana. Niliposikia sauti yake nilikaa kwa kuinamia mbele na kusikiliza kwa makini(Najaribu kukumbuka alichosema Elijah Muhammad kutokana na nilivyokuja kumsikia akiongea zaidi ya mara mia) “Kwa miaka ishirini na moja iliyopita sijaacha hata siku moja kusimama na kuwahubiria, nilipokuwa huru na hata nilipokuwa kifungoni. Nilikuwa kifungoni kwa miaka mitatu na nusu na pia zaidi ya mwaka mmoja kwenye jela ya jiji kwa
sababu ya kuhubiri kweli hii. Pia nilinyimwa nafasi ya kuonyesha upendo wa baba kwa miaka saba sababu ya kuwakimbia maadui wa neno hili na ufunuo wa Mungu uwapao uhai na kuwafanya kuwa sawa na mataifa yote huru, yaliyostaarabika na watu wa dunia hii kwa ujumla . . . . “ Elijah Muhammad aliongea jinsi ambavyo kwa karne nyingi kwenye nyika hizi za Amerika ya Kaskazini, “Shetani mwenye macho ya bluu-mzungu” alivyomchota akili mtu anayeitwa “Negro.” Alituambia jinsi ambavyo mtu mweusi wa Marekani amekufa “kimaadili, kiakili na kiroho.” Sababu ya kuchotwa huko akili. Alizungumza jinsi ambavyo mtu mweusi ndiye mtu wa asili aliyenyakuliwa kutoka nyumbani kwake na kuvuliwa lugha yake, utamaduni wake, muundo wake wa familia, jina lake la ukoo mpaka mtu mweusi wa Marekani aliposhindwa kujitambua yeye ni nani.
Alituambia na kuonyesha jinsi ambavyo mafundisho yake juu ya ukweli wa mtu mweusi yanamuinua mtu mweusi kutoka daraja la chini kabisa la kijamii katika jamii ya mzungu na kumuweka alipokuwa mwanzo, juu ya ustaarabu wote. Mwisho wa hotuba alipumzika kidogo kuvuta pumzi, kisha akaniita kwa jina langu. Nilikuwa kama nimepigwa na umeme. Aliniomba nisimame. Aliuambia mkusanyiko ule kuwa nilikuwa nimetoka gerezani karibuni tu. alizungumza jinsi nilivyokuwa “Imara” wakati nipo gerezani. Alisema, “kila siku kwa miaka kadhaa,
ndugu Malcom amekuwa akiniandikia barua kutoka gerezani. Nami nilimuandikia barua mara nyingi kadri nilivyoweza.” Nilisimama pale huku nikihisi macho ya Waislamu mia mbili yakinitazama. Nikasikia akinitolea mfano. Mungu alipojisifu juu ya uaminifu wa Ayubu, alisema Elijah Muhammad, Shetani alimjibu kuwa wigo wa ulinzi wake kumzunguka Ayubu ndiyo unamfanya awe muaminifu. “Ondoa ulinzi huo,” Shetani alimwambia Mungu, “nami nitamfanya Ayubu akutukane waziwazi.” Shetani anaweza kudai kuwa nilipokuwa nimezungukwa na wigo gerezani nilijidai tu kuwa Muislamu, alisema Elijah Muhammad, kisha akaendelea kuwa sasa nipo uraiani Shetani anadai kuwa nitarudia maisha yangu ya kunywa pombe, kuvuta sigara, kutumia madawa ya kulevya na uhalifu. “Basi sasa wigo uliomzunguka ndugu yetu Malcom umeondolewa, tutajionea wenyewe atakavyoenenda.” Alisema bwana Elijah Muhammad. “nina imani ataendelea kuwa muaminifu.” Na Allah alinibariki kuendelea kuwa imara na muaminifu katika imani yangu ya Kiislamu pamoja na majaribu mengi niliyokutana nayo. Na hata ulipotokea mgogoro kati yangu na Elijah Muhammad, nilimwambia bila unafiki wowote kuwa bado nina imani naye kuliko hata yeye mwenyewe anavyojiamini. Leo siko pamoja na bwana Muhammad sababu tu ya husda na wivu.Nilikuwa na imani na Elijah Muhammad kuliko ninavyoweza kuwa na imani na mtu yeyote duniani hapa.
Utakuwa unakumbuka nilisema kuwa nilipokuwa gerezani bwana Muhammad alifikia nyumbani kwa kaka yangu Wilfred alipotembelea Hekalu Namba Moja huko Detroit. Waislamu wengi wanasema huwezi kumtendea Elijah Muhammad zaidi ya anavyoweza kukutendea, basi Jumapili hiyo alitulika familia nzima pamoja na Imam Lemuel Hassan kupata chakula cha jioni kwenye nyumba yake mpya. Bwana Muhammad alisema kuwa watoto na wafuasi wake walikuwa wamemsisitiza ahamie kwenye nyumba hii kubwa. Ilikuwa nyumba nzuri na kubwa ya vyumba kumi na nane. Ilikuwa namba 4847 katika barabara ya Woodlawn huko Chicago. Nadhani ni juma lilelile ndiyo walikuwa wamehamia. Tulipofika bwana Muhammad alituonyesha eneo alilokuwa anaendelea kupaka rangi. Ilinibidi kujizuia, vingenevyo ningekimbia kuleta kiti ili Mtume wa Allah aketi, lakini kumbe naye pia alikuwa anatuwazia sisi. Tulitegemea kusikia busara zake wakati wa chakula lakini badala yake alitusisitiza tuongee. Nilikaa pale nikitafakari jinsi ambavyo hekalu letu la Detroit limekaa tu likisubiri Allah kuwaleta waumini, na zaidi-juu ya mamilioni ya watu Weusi kote Marekani, watu ambao hawajawahi kusikia mafundisho yanayoweza kumuamsha na kumchochea mtu mweusi . . . basi pale kwenye meza ya bwana Muhammad nikapata ujasiri wa kuongea. Siku zote nimekuwa mtu wa kuongea kwa uwazi. Kulipokuwa na ukimya nilimuuliza bwana Muhammad kuwa Hekalu letu Namba Moja kule Detroit lilitakiwa kuwa na Waislamu wangapi. Alinijibu “Maelfu.” Nilimjibu ndiyo, Kisha nikamuuliza “Unafikiri ni njia gani nzuri ya kupata hao maelfu?” “Wafuate vijana,” alisema. “Baada ya kuwapata, wazee watajiunga kwa kuona aibu.” Nikadhamiria akilini mwangu kuwa tutafuata ushauri huo. Tuliporudi Detroit niliongea na kaka yangu Wilfred. Nilijitolea kumsaidia kazi Imam Lemuel Hassan. Naye aliunga mkono wazo langu kuwa tutumie njia ya bwana Muhammad katika kupata waumini wapya. Kuanzia siku hiyo, kila siku jioni baada ya kutoka kazini nilienda kufanya kile ambacho Waislamu wakati huo tuliita “Uvuvi.” Nilijua lugha na mawazo ya watu walioishi maeneo ya maghetto: “My man, let me pull your coat to something-” Nilikuwa nimeshatuma maombi yangu na nikapokea “X” yangu kutoka Chicago. “X” ya Waislamu inawakilisha jina lake halisi la ukoo wake wa Kiafrika ambalo hatakuja kulijua. Kwangu “X” ilikuwa mbadala wa jina la Little ambalo mmiliki watumwa aliwapachika babu zangu. Kupata kwangu “X” kulimaanisha maisha yangu yote kwenye Taifa la Kiislamu nitajulikana kama Malcom X. Bwana Muhammad alifundisha kwamba tutatumia hizo “X” mpaka Mungu mwenyewe atakaporudi na kutupatia majina matakatifu kwa mdomo wake mwenyewe. Nilienda kutafuta waumini kwenye vibanda vya kuchezea pool, baa na vichochoro vya maeneo ya maghetto ya Detroit. Huko niliwapata ndugu zangu weusi wakiwa masikini, wajinga, waliochotwa akili, viziwi, vipofu na mbumbumbu wa kiakili, kiroho na kimaadili kiasi kwamba hawakuweza kuitikia. Ilinichukiza kuona ni mara chache sana watu walionyesha udadisi hata ule kidogo tu juu mafundisho yenye lengo la kumuamsha mtu mweusi. Wachache walioonyesha udadisi niliwabembeleza sana wahudhurie mikutano kwenye Hekalu Namba Moja, lakini kati ya wale waliokubali kuja— waliokuja hawakufika hata nusu. Polepole watu wakaanza kupendezwa. Kila mwezi magari kadhaa yaliongezeka kwenye msafara wetu wa kuelekea kwenye Hekalu Namba Mbili huko Chicago. Lakini hata baada ya kumsikia na kumuona Elijah Muhammad, ni wachache tu waliandika barua kwa Elijah Muhammad kuomba kuwa wanachama wa Taifa la Kiislamu. Lakini baada ya miezi michache ya kupambana Hekalu letu likawa na washirika mara tatu ya idadi ya mwanzo. Jambo hilo lilimfurahisha sana bwana Elijah Muhammad hadi akafanya ziara ya heshima kuja kututembelea. Bwana Muhammad alinisifa sana baada ya Imam Lemuel Hassan kumueleza jinsi nilivyofanya kazi kwa bidii kwa ajili ya Uislamu. Sasa msafara wetu ukawa umekuwa mkubwa. Nakumbuka kuwa tulienda Chicago ndani ya magari ishirini na matano. Na kila tulipoenda tuliheshimishwa kwa chakula katika nyumba ya Elijah Muhammad. Alipendezwa sana na uwezo wangu, niliweza kuona hilo kwa jinsi alivyoongea. Nami ni kama nilimuabudu.
Mwaka 1953 niliacha kazi kwenye duka la samani. Nilipata kazi yenye mshahara mzuri kidogo kwenye kiwanda cha Gar Wood huko huko Detroit. Kiwanda hicho kilitengeneza mabodi ya magari ya taka. Kazi yangu ilikuwa kusafisha baada ya wachomeleaji kumaliza kazi yao. Wakati wa chakula bwana Muhammad alikuwa anasema mahitaji yake makubwa ni kupata vijana wengi zaidi, vijana walio tayari kufanya kazi kwa bidii wawezavyo ili kuchukua majukumu ya maimam wake. Alisema kuwa mafundisho yanatakiwa kupelekwa mbali kuliko yalipofika, na kunahitajika kufungua mahekalu kwenye majiji mengine. Sikuwahi kufikiria kabisa kuwa nitakuwa mhubiri. Sikuwa hisi hata kidogo kuwa nina vigezo vya kumuwakilisha bwana Muhammad. Kama kuna mtu angeniambia niwe mhubiri ningestaajabu sana na kumwambia kuwa nina furaha kumtumikia bwana Muhammad katika nafasi ya chini kabisa. Sijui kama lilikuwa ni pendekezo la bwana Muhammad au ni mhubiri wa Hekalu namba moja, Lemuel Hassan ndiye alieamua niwahubirie ndugu na dada hekaluni mwetu. Nakumbuka nilitoa ushahidi jinsi mafundisho ya Elijah Muhammad yalivyonitendea: “Kama nikiwaambia maisha maisha niliyoishi hamtaniamini. . . . ninapomuongelea mzungu simuongelei mtu nisiyemjua. . . .” Muda mfupi baada ya hapo, Imam Lemuel Hassan akanitaka kuwahutubia ndugu na dada kwa hotuba ya bila kujiandaa. Nilisita na sikuwa najiamini, lakini nilijipa moyo kuwa nimewahi shiriki kwenye mijadala kule gerezani hivyo nikajitahidi kadri nilivyoweza. (Sikumbuki nilichosema lakini nakumbuka kuwa mwanzoni mada yangu kuu ilikuwa juu ya Ukristo na madhira ya utumwa, mada ambazo nilihisi ninazielewa vya kutosha kutokana na kujisomea gerezani) “Ndugu na dada zangu, dini ya mzungu aliyetufanya watumwa, yaani Ukristo, inafundisha watu weusi wa huku Amerika Kaskazini kuwa tukifa tutaota mabawa na kupaa mawinguni ambako Mungu ametuandalia makao yaitwayo Mbinguni. Huu ndiyo Ukristo wa mzungu unaotumika kutuchota akili sisi watu weusi. Tumeukubali! Tumeupenda! Tumeuamini! Na tumeuishi, lakini tukiwa tunaendelea kufanya hivyo, kwa maslahi yake; huyu shetani mwenye macho ya bluu ameugeuza ukristo huo ili aweze kutukandamiza . . . kufanya macho yetu yaendelee kuangalia keki kutoka angani na mbingu inayokuja . . . wakati yeye akifurahia mbingu yake hapa hapa duniani . . . kwenye maisha haya haya. Leo hii nahutubia mbele ya maelfu ya Waislamu, na nawafikia mamilioni wengine kupitia redio na luninga, lakini kwa hakika sipati hisia kama zile nilizopata kwa kuhutubia Waislamu wale sabini na tano au mia moja hivi pamoja na baadhi ya wageni wachache, wakiwa wamekaa pale hekaluni huku vilio vya nguruwe kutoka machinjioni vikisikika. Wakati wa majira ya joto ya mwaka 1953 niliwekwa kuwa Imam msaidizi wa Hekalu Namba Moja la Detroit—sifa zote zimuendee Allah.
Kila siku baada ya kazi nilienda kwenye maeneo ya maghetto ya watu weusi kufanya uvuvi. Niliwaona ndugu na dada zangu ambao shetani wa kizungu alikuwa amewachota akili. Nywele zao zilikuwa kama zangu zilivyokuwa kwa miaka mingi, zimelainika kwa kuwekwa dawa—zimenyooka kama za mzungu. Mara kwa mara mafundisho ya bwana Muhammad yalipingwa na hata kudhihakiwa . . . “Hebu niondokee, umewehuka!” Wakati mwingine kichwa changu kiliwaka kwa hasira na masikitiko kwa ajili ya ndugu zangu weusi waliokuwa vipofu. Nilisubiria kwa hamu sana kupewa nafasi nyingine ya kuongea kutoka kwa Imam Lemuel Hassan. “Ndugu na dada zangu, hatukushusha nanga kwenye jiwe la Plymouth—jiwe la Plymouth ndilo lililotushukia!”. . . ‘Fanya kila uwezalo kusaidia kazi ya Mtume Elijah Muhammad kwa watu weusi . . . siku zote mzungu ametutawala kwa kutufanya tumkimbile kumuomba, ‘tafadhali bwana, tafadhali mzungu, bosi utanidondoshea makombo mengine kutoka meza yako iliyojaa utajiri. . . .’ ‘Ndugu zangu na dada zangu weusi! Tunaposema weusi tunamaanisha wote wasio wazungu. Ndugu na dada hebu angalieni ngozi zenu! Sote ni weusi mbele ya mzungu lakini tuna rangi tofautitofauti elfu kidogo. Geuka na mtazame mwenzako! Una aina gani ya weusi wa Kiafrika uliochafuliwa na mzungu? mnaniona mimi, mtaani walizoea kuniita Detroit Red. Ndiyo! Ndiyo, shetani mbakaji mwenye nywele nyekundu ndiye alikuwa babu yangu! Wala si zamani, Baba wa mama yangu. Mama yangu hakupenda kuongelea hilo na huwezi mlaumu. Alisema hajawahi kumuona baba yake na alikuwa akishukuru kwa hilo, nami namuunga mkono. Iwapo ningeweza kutoa damu ya babu yangu huyo inayochafua mwili wangu na rangi yangu ningefanya hivyo! Sababu nachukia kila tone la damu ya mbakaji yule iliyomo ndani yangu! ‘Na hili si kwangu tu, limetokea kwetu sote! Tafakari kuhusu wakati wa utumwa, haikuwa rahisi kwa bibi na nyanya zetu kuepuka wabakaji wa kizungu waliowamiliki.
Mbakaji huyo aliyemtoa uanaume mwanaume mweusi kwa vitisho . . . na kumjaza hofu kiasi kwamba mpaka leo hii mwanaume mweusi anaishi akimuogopa mzungu siku zote. Na hata leo anaishi chini ya ukandamizaji wake. ‘Fikiria—fikiria juu ya mwanaume mweusi akiwa amejawa na uoga na hofu , akisikiliza kilio cha mke wake, mama yake , binti yake akibakwa zizini, jikoni na vichakani. Fikirini hilo ndugu na dada zangu! Fikiria kusikia mke, mama na binti yako akibakwa! Nawe ukiwa umejazwa hofu na mbakaji huyo kiasi kwamba huwezi kufanya chochote. Kisha watoto waliozaliwa akawaita majina mabaya kama mulatto, quadroon, octoroon na majina mengine mabaya anayotuita pale asipotuita Nigger “Geuka na muangalie mwenzako, na fikiria kuhusu jambo hili. Sote rangi zetu zimechafuliwa lakini shetani huyu bado anategemea wahanga wake tumpende!
Nilikuwa nikikabwa na jazba kiasi kwamba nyakati nyingine nilitembea mitaani hadi usiku sana. Wakati mwingine nilikuwa siongei na mtu yoyote kwa saa kadhaa, nakaa kimya nikitafakari mambo ambayo mzungu amewafanyia watu wetu hapa Marekani.
****