Kiwanda cha mvinyo cha Afrika Kusini kinalenga fursa za ukuaji chini ya sera ya China ya ushuru sifuri

Kiwanda cha mvinyo cha Afrika Kusini kinalenga fursa za ukuaji chini ya sera ya China ya ushuru sifuri

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
VCG31N1967158566.jpg


Chini ya mwanga hafifu wa mwanzoni mwa majira ya mpukutiko katika Kizio cha Kusini, mistari ya chupa inasikika kwa utulivu katika Kiwanda cha Mvinyo cha Diemersdal huko Cape Town Afrika Kusini. Msimu wa mavuno ndio kwanza umemalizika, na kuacha safu za mizabibu zikiwa zimechumwa zabibu zake vizuri, lakini kiwanda cha mvinyo kinaendelea katika harakati zake kikamilifu.

Kuanzia asubuhi na mapema, vigari vya kubebea husafirisha chupa tupu hadi kwenye mstari wa uzalishaji, ambapo husafishwa, kujazwa mvinyo mpya, kufungwa, kuwekewa chapa, na kupakiwa, kabla ya kuanza safari ya kuelekea bandari ya Cape Town na kuendelea hadi masoko ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na China.

Safari hiyo inaweza kuwa muhimu zaidi hivi karibuni. Wakati China ikijiandaa kutekeleza sera ya ushuru sifuri kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nchi 53 za Afrika kuanzia Mei 1, viwanda vya mvinyo kama Diemersdal vinajiweka katika nafasi nzuri kwa kile wanachokiona kama wakati muhimu.

Kwa upande wa Steffi Layer, meneja masoko na mauzo wa kimataifa wa kiwanda hicho, aliiambia Xinhua kwamba sera hiyo inazidi kupunguza gharama, na badala yake inaelekeza kwenye fursa pana kuanzia kuongezeka kwa faida na upanuzi wa soko hadi kuimarika kwa thamani ya chapa katika soko muhimu la kimataifa.

Likiwa kwenye mteremko wa baridi wa Durbanville huko Cape Winelands, shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 200 lina historia iliyoanzia mwaka 1698. Linazalisha aina mbalimbali za mvinyo, zikiongozwa na Sauvignon Blanc na Pinotage - aina ya pili maarufu Afrika Kusini ambayo pia imepata umaarufu miongoni mwa wanywaji wa China.

Diemersdal imekuwa ikisafirisha mvinyo wake China kwa karibu miongo miwili, ambapo usafirishaji awali uliongezeka kutoka asilimia 1 hadi 2 tu ya uzalishaji hadi kufikia asilimia 10 hadi 15 mwaka 2018, kabla ya kupungua kutokana na janga la UVIKO-19 na mabadiliko makubwa katika mahitaji ya kimataifa.

"Kwa kweli tumekuwa tukisafirisha mvinyo China kwa muda mrefu sasa. Ni karibu miaka 16 au 17 sasa tangu tuanze kufanya kazi na soko la China," Layer aliiambia Xinhua. Ingawa mahitaji yamepungua katika miaka ya hivi karibuni, aliongeza kuwa kuondolewa kwa ushuru kunaweza kusaidia kufufua maslahi na kuleta fursa mpya.

Layer alionesha imani kubwa katika uwezo wa muda mrefu wa soko la China, akiashiria mabadiliko ya ladha za wanywaji na kuongezeka kwa thamani ya utamaduni wa mvinyo.

"Katika miaka michache iliyopita, mahitaji yamepungua, lakini nadhani kuna fursa kubwa sana inayokuja sasa," alisema, akisisitiza shauku inayoongezeka ya mvinyo miongoni mwa wanywaji wa China, pamoja na utamaduni unaoendelea zaidi wa kula chakula pamoja na mvinyo.

Wakati huo huo, mvinyo wa Afrika Kusini unadumisha ushindani, alisema, haswa katika suala la thamani. Kwa mujibu wa Layer, mchanganyiko wa ubora wa juu na bei rahisi huruhusu wazalishaji kujitokeza kimataifa, akiongeza kuwa njia za usafirishaji za Afrika Kusini - ambazo tayari zimeunganishwa vizuri katika mtiririko wa biashara ya kimataifa - zinaongeza zaidi uwezo wake wa kuuza nje.

Kitu muhimu kwa Diemersdal ni matarajio kwamba sera ya ushuru sifuri ya China itafungua fursa katika nyanja nyingi, ikiwa ni pamoja na ushindani wa bei, uwepo uliopanuliwa wa soko, na nafasi nzuri ya chapa.

"Hata hivyo inatia hamasa, kwa sababu ni wazi kwamba mara tu ushuru utakaposhuka, bei ya mvinyo nchini China kwenye rafu pia itakuwa ya ushindani zaidi," alisema.

Layer aliongeza kuwa vizuizi vidogo vya uingizaji vinaweza kuwatia moyo waagizaji kuangalia upya mvinyo wa Afrika Kusini, huku wakiwapa wanywaji fursa kubwa zaidi ya ufikiaji. "Inaondoa kizuizi cha kufanya biashara kati yao," alisema.

Mbali na bei, Layer anaona fursa katika sehemu ya malipo, haswa kutokana na wanywaji wa China wanapendelea zaidi mvinyo mwekundu. "Walaji wa China bado wanakunywa mvinyo mwingi mwekundu," alisema, akibainisha kuwa mahitaji haya yanawezesha viwanda vya mvinyo kufanya kazi kwa bei ya juu na kupata faida kubwa zaidi.

Ili kutumia vyema mabadiliko haya, Diemersdal imeanza kuimarisha uwepo wake Asia. Layer alisema hivi karibuni kiwanda chao cha mvinyo kilishirikiana na mwakilishi aliyeko katika eneo hilo ili kuongeza ufahamu zaidi wa soko na kupanua ufikiaji wake, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika maonesho ya biashara, kulenga miji maalum, na kuboresha bidhaa wanazotoa ili kuendana vyema na ladha za wenyeji.



Layer alibainisha kuwa sera ya ushuru sifuri inaweza pia kutoa faida zinazoongezeka katika sekta pana ya mvinyo na mnyororo wa usambazaji. Kuongezeka kwa mauzo ya nje kunaweza kuongeza faida, kuwezesha uwekezaji mpya katika uzalishaji na usafirishaji, huku pia makampuni ya usafirishaji, waendeshaji mizigo na waagizaji yakizidi kunufaika.

Kwa upana zaidi, Layer anaona maendeleo hayo kama sehemu ya uhusiano wa kiuchumi unaoimarika kati ya China na Afrika Kusini, pamoja na ushirikiano mpana kati ya China na Afrika. Ingawa bidhaa za China -- kuanzia teknolojia hadi magari -- zinazidi kuonekana nchini Afrika Kusini, nchi hiyo inatoa bidhaa za kilimo kama vile mvinyo na vyakula vya baharini ambavyo vina mahitaji yanayoongezeka nchini China.

Kinyume na hali hii, Layer alionesha imani kwamba uhusiano wa karibu wa kibiashara utatoa faida za pande zote mbili. "Nadhani ni hali ya kunufaishana pande zote mbili," alisema.
 
Back
Top Bottom