Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
Akizungumza katika Kliniki hiyo Kaimu Afisa Maendeleo ya Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Bw. Emmanuel Amos, amesema, huduma zinazotolewa katika Kliniki hiyo ya ardhi zimelenga kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi ili kuwasaidia kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika sekta hiyo.
Amesema, huduma zinazotolewa ni pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi, utoaji wa elimu ya ulipaji wa kodi ya pango la ardhi, utoaji wa hati kwa wenye vigezo, pamoja na ushauri kuhusu mipango miji, uthamini na umilikishaji.
Akizungumzia ulipaji kodi ya pango la ardhi, Bw. Amos amewataka wamiliki wa ardhi kuhakikisha wanalipa kodi hiyo kwa wakati ili kuepuka usumbufu.
“Tunatoa Ankara za kodi ya pango la ardhi ili kurahisisha malipo kwa wananchi, hivyo ni muhimu kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa wakati,” amesema.
Amewahimiza wananchi kufika kwenye mabanda ya huduma yaliyowekwa katika viwanja hivyo ili waweze kuhudumiwa kwa karibu, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria katika kushughulikia changamoto za ardhi badala ya kuchukua sheria mkononi.
"Nwitikio wa wananchi ni mzuri na huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, huku wadau mbalimbali wakishirikiana kikamilifu kutoa elimu na kusaidia utatuzi wa changamoto za ardhi". Amesema.