1. UK haijazuia "watanzania" kuingia nchini mwao. Wamezuia WAGENI wanaotoka au waliopitia Tanzania ndani ya siku 10 kabla ya tarehe 22 Januari 2021. Raia wao na raia wenye haki za makazi UK wataruhusiwa ila kwa masharti ya kujitenga kwa siku 10. Hivyo hata kama ni raia wa nchi nyingine unaishi Tanzania au umepitia, na haukidhi vigezo vya uraia na haki za makazi, hautaruhusiwa kuingia.
2. Uingereza wana haki na wajibu wa kulinda wananchi wao na kutanguliza maslahi ya nchi yao. Ikiwa wamefanya utafiti wao na kuona kuwa WAGENI kutoka "Tanzania" wanaleta madhara, wanayo haki ya kujilinda.
Hata hivyo, bado kuna shaka hii hatua imechukuliwa kisiasa zaidi kuliko kiutaalam.
Mosi, je ugonjwa na 'variant' mpya ya COVID 19 inaangalia uraia? Ikiwa kama wanaoruhusiwa kuingia wanaweza kujidhibiti au kudhibitiwa ili wasiambukize wengine, kwa nini kusiwe na utaratibu utakaochuja wanaoweza kufuata njia hizo hizo?
Pili, ikiwa mashirika ya ndege yanalazimisha vipimo vya ugonjwa wa Korona kabla ya kusafiri, ina maana hawaviamini vipimo hivyo na hivyo kuvifanya batili? Kuna haja gani ya kufanya vipimo vya USD100 na bado vinaonekana havina tija?
Nota Bene: mtazamo huu hauainishi kama msimamo au hatua za Tanzania kukabiliana na magonjwa ya Korona ni sahihi au la.