KWA NINI WATANZANIA NI WAOGA? JE WEWE NI MWOGA?
Na, Robert Heriel
Kauli ya Mzee Butiku alipokuwa akihojiwa na ITV, Kusema woga wa Watanzania ni wakujitakia, sio kwamba wanazuiwa kusema ukweli. Na woga huo unatokana na ujinga kwa mujibu wa Mzee Butiku. Pia sababu nyingine ni kutokujiamini.
Mzee Butiku anaeleza kuwa, viongozi ni binadamu kama binadamu wengine, hatupaswi kuwaogopa. Kwani tumechagaua wenyewe kwa ajili ya kututumikia. Hivyo wakifanya mazuri ni wajibu wetu kuwapongeza na kuwasifia, na wakifanya vibaya tunaowajibu wa kuwakosoa.
Binafsi nimekuwa msema ukweli tangu mwaka 2013, nimekuwa nikiikosoa na kuipongeza serikali na viongozi wake. Nimekuwa nikikosoa viongozi wa dini na kuwapongeza ikiwa wamefanya mazuri au mabaya. Nimekuwa nikiwakosoa na kuwapongeza wat mashuhuri kama wanamuziki, waigizaji na watu wengine.
Katika uzoefu wangu wa kuelimisha, kuasa, na kuikosoa jamii yetu nimekumbana na mambo mengi, hata hivyo yote nafahamu ni sehemu ya kazi.
Nilichogundua woga wa watu wengi unatokana na sababu zifuatazo;-
1. USALAMA
Watanzania wengi huogopa pale waonapo usalama wa maisha yao ukiwa mashakani, pengine sio Tanzania tuu hata sehemu zingine duniani.
Kwa uzoefu wangu, nikiwa naandika makala hasa zile za kuonya jamii labda namuonya Kiongozi fulani, huenda ni Rais, waziri fulani, mkuu wa Mkoa, au kiongozi wa dini. Huwa ndugu zangu, Mama zangu, wajomba, rafiki zangu na wadau wanaonifahamu na wasionifahamu kwa sura hunitumia ujumbe na wengine kunipigia kuwa niache kukosoa, kukemea na kuonya uovu wa watu wakubwa kwani kwa kufanya hivyo nitajiingiza kwenye matatizo na usalama wangu utakuwa mashakani. Hoja hii ndio hoja kubwa zaidi kuliko zote.
2. MASLAHI BINAFSI
Woga wa Watanzania wengi pia unasababishwa na Maslahi binafsi ya watu. Kwa mfano unaweza kumkosoa kiongozi wa chama fulani, Mfano unapomsema Mhe. Magufuli au Mbowe juu ya jambo fulani lazima uelewe kuwa kuna watu wananufaika na viongozi hao. Hivyo kumkosoa kiongozi wanayenufaika naye ni kugusa maslahi yao. Hivyo watu hao wanaweza kukutisha na kukutuna kama sio kukudhuru kabisa.
Pia baadhi ya watumishi wa UMMA huwa waoga kukosoa viongozi wao kwa sababu ya kuogopa kufukuzwa kazi, hivyo huamua kuwa waoga ili kulinda maslahi yao. Woga huu ndio unashika nafai ya pili hapa nchini.
Baadhi ya viongozi wadhalimu hutumia kete hii kuwachapia watumishi wa Umma waliowaadilifu kwa kusema ukweli na kupinga uovu.
3. UJINGA
Woga namba tatu husababishwa na ujinga. Huu ni ule woga ambao mtu huogopa mambo kwa sababu ya ujinga wake, yaani kutokujua haki zake.
Woga huu pia husababishwa na kutojitambua(self-awareness). Ni kama vile zamani au kijijini watu kumuogopa askari. Woga huu pia huu ni Kutotambua nafasi za wengine.
Kwa mfano;
Kuna siku nilimkosoa na kumkemea Askofu Gwajima kutokana na kuteleza kwake katika mdomo, hata akasema mambo ya hovyo. Nilimkosoa kwa kujua yeye ni binadamu kama walivyobinadamu wengine.
Ajabu walinipigia baadhi ya watu(nafikiri ni wafuasi wake) wakinikemea, sikuwalaumu kunikemea, ila nilitaka kujua wananikemea kwenye nini. Wakaniambia ati; Hairuhusiwi kumkosoa mtumishi wa Mungu(wakimaanisha wachungaji, wachungaji. mashekhe n.k) nilipowauliza kwa nini wasikosolewe ikiwa wanafanya makosa? walishindwa kunijibu, nikawauliza mtumishi wa Mungu ni nani? Hapo ndipo nikajua kuwa kuna mambo hawayajui. Sikuwalaumu kwani nilliona wanauoga uliosababishwa na ujinga wao wa kutokujua nani hapaswi kukosolewa.
Asiyepaswa kukosolewa ni yule afanyaye jambo jema, wema, lakini kama mtu anafanya makosa lazima akosolewe.
4. KUTOKUJIAMINI
Zipo sababu zinazopelekea mtu awe mwoga hasa anapokosoa serikali, au viongozi. Moja ya sababu ni pamoja na dhamiri yake. Yaani kama mtu anamkosoa kiongozi fulani akiwa na dhamiri ya kumchafua ili apate maslahi yake binafsi au ya kichama basi lazima akose kujiamini.
Imezoeleka kwa wanasiasa kukosoa mahasimu wao wakiwa na dhamiri sio ya kujenga jamii bali kujijenga wao kisiasa.
Mtu kama anadhamiri ya kweli ya kukosoa serikali na kutoa way forward ya nini kifanyike, huku akiwa hana maslahi yoyote ile binafsi au kikundi chochote kile basi lazima ajiamini.
Mimi ninapoikosoa serikali au chama chochote cha siasa huwa nalenga kuijenga jamii, na ndio maana najiamini sana. Haijalishi watu wananichukuliaje kwa maana nikiisifu serikali watu wanasema mimi CCM, haya kukaa kidogo nikimsifu Tundu Lisu watu hao hao wanasema mimi ni CHADEMA.
Watu wengi wananiuliza; kwa nini unaikosoa serikali au viongozi wa dini au viongozi wa vyama alafu unaacha mawasiliano yako hapo na mahali ulipo? Unajiamini nini?
Ninachowajibu ni kuwa mbona nikiwapongeza hamniulizi maswali haya?
Pili nawajibu, najiamini kwa sababu sina dhamiri ovu. Kwani waovu hukimbizwa pasipokukimbizwa.
Tatu, naacha mawasiliano kusudi, kama kuna mtu atataka maelezo au ufafanuzi wowote wa kile nilichoandika awasiliane na mimi.
Nafahamu kuwa mtu hawezi kujificha awapo dunia hii labda awe amekufa.
5. KUOGOPA WAOVU NA WENYE HILA
Watu huogopa pia kwa sababu ya uwepo wa watu waovu. Waovu hutoka upande wowote ule.
Kwa mfano unaweza ukaikosoa serikali, alafu yenyewe wala ikawa haina habari na wewe kama itakuwa imeelewa lengo lako la kuikosoa. Lakini wakatokea waovu wakakudhuru ili ionekane serikali ndio imefanya jambo hilo. Na kwa vile hivi karibuni uliikosoa au unamazoea ya kuikosoa basi watu watajua ni serikali.
Kwa hiyo watu huwa waoga kusema ukweli kwa sababu waovu huweza kufanya chochote dhidi yao. Hivyo ni bora kukaa kimya
6. WAZAZI, MKE NA NDUGU.
Wakati mwingine uoga unaletwa na wazazi, ndugu na Mke. Watu hupenda kuwa wakweli, kukemea maovu lakini wazazi, ndugu, na wake zetu hutushauri na kutushinikiza tuwe waoga kusudi tubaki salama kwa kuhofia kuwa madhara ya kusema ukweli wakati mwingine hugharimu maisha. Hii pia nimeipata hata mimi, kwani wazazi, ndugu na marafiki wamekuwa mstari wa mbele kunisihi niachane na ukosoaji bali nielimishe tuu jamii.
7. SERIKALI YENYEWE
Woga wa Watanzania pia unasababishwa na serikali kutowajenga wananchi wake kuwa huru, kusema ukweli, na kukemea maovu. Kama serikali ingeamua kuwaambia wananchi wawe huru kusema ukweli basi wananchi wengi wangekuwa sio waoga. Lakini kutokana na kuwa ndani ya serikali kuna baadhi ya viongozi wasiowaaminifu, wezi, mafisadi, na kila aina ya uovu basi hutisha watu kwa njia nyingi ili maovu yao yasisemwe semwe wasijeingia matatani.
8. VIONGOZI WA DINI.
Viongozi wa dini wengi ni wanafiki, wabinafsi na watu wa maslahi yao. Moja ya sifa kubwa ya kiongozi wa dini ni kukemea uovu kwa nguvu zote. Ukiona unasali au kuabudu kwenye kanisa na viongozi wake hawakemei maovu kwa kuyataja kabisa, kwa mfano, ukiona tatizo limetokea ndani ya nchi kama ishu ya mauaji alafu kiongozi wako wa dini anashindwa kukemea uovu au wizi, au anashindwa kumkemea kiongozi wa kisiasa kama vile waziri au Rais wa nchi basi jua kiongozi huyo hastahili kukuswalisha, kukufundisha mafundisho ya Mungu. Kiongozi huyo atakufundisha uoga.
Kiongozi huyo atakufundisha kumuogopa shetani kuliko kumuogopa Mungu. Unajua Kiongozi anayekemea waovu bila kujali vyeo vyao anakufundisha kumuogopa Mungu na ndio maana anamkemea shetani kwa kuwakaripia wafanyao maovu. Lakini Kiongozi unakuta anashindwa kumwambia Kiongozi wa kiserikali kuwa acha dhambi, au acha kutoa kauli za hovyo, alafu huyo huyo ukitenda wewe muumini anakuwa wa kwanza kukufundisha, huo ni unafiki.
Makanisa na Misikiti siku hizi zimekuwa nyumba za kufundishia watu kumuogopa shetani.
Kiongozi wa dini bora ni yule mwenye uwezo wa kukemea kwa wazi kabisa matendo maovu yanayofanyika kwenye jamii yake. Mwenye uwezo wa kusema siwezi kumuapisha huyu kwa sababu hastahili kuwa kiongozi, atoe sababu zenye mashiko. Na sio kujipendekeza ili apate pesa.
Mwisho nimalize kwa kusema; Woga ni dhambi kubwa, kwani kupitia woga ndio maovu huongezeka.
Ipende Nchi yako, kuwa mzalendo.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar es salaam