Zitto sasa ataka nafasi ya mwenyekiti agombee Dk Slaa
Na Fred Azzah
MOTO wa Uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokarsia na Maendeleo (Chadema), bado unazidi kuwaka baada ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe kukataa mapendekezo ya wazee wa yeye kuwa Katibu Mkuu ili kumpisha Mbowe na badala yake kutoa masharti mapya ya kujitoa.
Habari zilizopatikana jana kutoka makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam zinaeleza wazee walieleza kuwa mgawanyiko uliotokana na vigogo hao wa Chadema, Zitto na Mbowe kuchukua fomu kuwania uenyekiti ni hatari kwa uhai wa chama.
Walisema ili kukinusuru chama hicho walipendekeza Katibu Mkuu wa sasa, Dk Willibrod Slaa agombee nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Zitto awe Katibu Mkuu wa chama ili kumwachia Mbowe kusimama kugombea uenyekiti.
Kikao hicho kilianza saa 4:00 asubuhi na kumalizika kikishirikisha Mwasisi wa Chama hicho, Edwin Mtei, Mwenyekiti mstaafu, Bob Makani, Victor Kimesera, Phillemon Ndesamburo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilibrod Slaa na Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Halima Mdee.
Ziito ndiye alianza kuingia katika kikao hicho saa 9:00 alasiri huku Mbowe akingia baadaye saa 11:00 jioni.
Pia inaelezwa kuwa moja ya ajenda kubwa ya kikao hicho ilikuwa ni kujaribu kukinusuru chama kwa kumtaka Zitto akubali kuondoa jina lake katika kinyang'anyiro hicho ili kumpisha Mbowe aweze kugombea ili kulinda hadhi ya chama.
Hata hivyo, taarifa za ndani zinaeleza kuwa Zitto alikataa pendekezo hilo na kuwaleza wazee hao kuwa yupo tayari kujitoa iwapo Mbowe na yeye atajitoa kugombea nafasi hiyo ili ichukuliwe na Dk Slaa kwa lengo la kuleta umoja ndani ya chama hicho.
Inaelezwa kwamba Zitto alipinga mapendekezo ya wazee kwa madai kuwa kama Mbowe ataendelea kugombea nafasi ya uenyekiti wakati amekuwa akimchafu kuwa ni fisadi, umoja katika chama hicho hautakuwapo.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kwamba Zitto alipendekeza badala yake wote wawiliyeye na Mbowe, wajitoe katika kinyanganyiro ili kukinusuru chama kugawanyika na nafasi hiyo ichukuliwe na Dk Slaa ambaye alikuwa katibu wa kikao hicho cha wazee.
Vyanzo vyetu vya uhakika vinasema Zitto aliwaeleza wazee hao kuwa yupo tayari kutokuwa na cheo lakini chama kibaki salama.
Hata hivyo, wazee waliamua kuwapa muda wa kujadili mapendekjezo ya wazee Dk Slaa, Mbowe na Zitto leo saa 3:00 asubuhi kabla ya kikao cha kamati kuu hakijaanza. Mkutano huo ulimazika saa 12:45 jioni.
Zitto alipotakiwa kutoa ufafanuzi wake alikataa na badala yake akataka aulizwe Slaa ambaye alikuwa katibu wa kikao hicho cha wazee.
Msimamo huo wa Zitto unatokana na kikao cha awali alichokaa na viongozi wa kambi yake kwenye Hoteli ya Tamali iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo wapambe wake walimtaka Zitto kukataa wazo la kumpisha Mbowe kwa kuwa ni haki yake ya kikatiba kugombea nafasi hiyo.
Katika kikao hicho kilichoelezwa kuwa ni cha kuweka mikakati ya kuendesha kampeni wafuasi wake hao walisisitiza kuwa hawatakubali mgombea wao ajitoe.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye alikuwapo katika hoteli hiyo alishuhudia Zitto akiingia saa 5:00 asubuhi katika hoteli hiyo na kwenda kukaa pamoja na baadhi ya viongozi wa chama hicho.
"Mwandishi tunaomba utupishe tunataka kuzungumza mambo yetu," alimwambia mmoja wa viongozi hao wa chama hicho ambaye awali walikuwa wamekaa pamoja kabla ya Zitto kuingia hotelini hapo.
Kikao hicho kilichokuwa na watu watano, akiwamo, Afisa Uhusiano wa Chama hicho, David Kafulila na Msafiri Mtemelwa kilifanyika nje ya vyumba vya hoteli hiyo.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho, mmoja wa watu hao walimdokeza Mwandishi wetu kuwa Zitto hatakubali wazo la kumpisha Mbowe kugombea nafasi ya mwenyekiti katika kikao cha baraza la wazee kilichokuwa kikifanyika makao makuu ya chama hicho na kwamba walikuwa wanaendelea na kampeni za mwisho kwa wajumbe wa mkutano mkuu ambao wameanza kuingia jijini Dar es Salaam.
Wakati juhudi za wazee hao zikiendelea, habari za ndani ya Chadema zinaeleza kuwa Zitto anaendelea na kampeni zake na hadi sasa anaungwa mkono na mikoa 15 na Zanzibar na kwamba ana nguvu kubwa iwapo jina lake litapitishwa kugombea nafasi hiyo. Leo Kamati Kuu ya chama hicho inakaa na kesho uchaguzi wa baraza la vijana na wazee.