Uchaguzi Chadema Kindumbwendumbwe Mbeya
Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Mbeya umeshindwa kufanyika baada ya kuzuka vurugu zilizosababishwa na wanachama na wagombea waliokuwa wakipinga kukiukwa kwa taratibu.
Dalili za kukwama kwa uchaguzi huo zilianza kujitokeza jana saa tatu asubuhi, ambapo wajumbe walipinga kauli ya Katibu anayemaliza muda wake, Ipyana Seme, ambaye aliwataka wajumbe waliojipeleka katika uchaguzi huo kuondoka.
Kauli hiyo ilipokewa kwa hisia tofauti na wajumbe ambao walipinga kuondolewa kwa wenzao wa wilaya za Mbozi na Ileje na baada ya kuona kelele zinazidi huku wajumbe wakimzonga, Seme aliondoka na gari na kurudi na askari Polisi.
Hatua hiyo ilitokana na kauli yake ya kuzuia wajumbe hao kwa madai kuwa hawajafanya uchaguzi katika wilaya zao, hivyo si wajumbe halali na hawana sifa za kushiriki mkutano huo, jambo ambalo lilipingwa na wajumbe wengine.
Katika uchaguzi huo, waliokuwa wanagombea uenyekiti ni Sambwee Shitambala ambaye aliwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Mbeya Vijijini na George Mtasha wakati ukatibu ulikuwa ukiwaniwa na Seme na Eddo Mkata.
Kutokana na vurugu na kutoelewana, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Ally Chitanda wa makao makuu ya Chadema, alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo saa mbili usiku kwa alichodai ni maagizo kutoka makao makuu kutokana na vurugu hizo.
Aidha, Chitanda alisema matokeo mengine ya watu waliochaguliwa kushika nafasi za Mwenyekiti wa Baraza la Vijana, Wanawake na Wazee, yatabaki kama yalivyo na nafasi za viongozi wa juu zitajazwa siku nyingine itakayotangazwa.
Akizungumzia kuahirishwa kwa uchaguzi huo, Shitambala alisema kanuni kadhaa za uchaguzi zilikiukwa ikiwamo ya kutokuwapo muhtasari wa kikao kilichopita na usajili wa wajumbe wa mkutano mkuu.
Hamuwezi kuwa kwenye mkutano na watu wanaanza kusema na yule ni mjumbe, Katibu tunamwambia alete muhtasari haleti, hatuwezi kufanya uchaguzi bila kufuata taratibu.
Katika uchaguzi hatuhitaji kuchaguliwa kwa kelele za mashabiki, hata kama walikuwapo mashabiki wangu, mimi sijali sana kuhusu kushinda, kwa sababu hakuna mishahara ila tunagombea ili kusaidia kuleta maendeleo, mimi nina kazi yangu na nimeajiri watu, alisema.
Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mtasha alisema kuahirishwa kwa mkutano wa uchaguzi huo kunatokana na vurugu ambazo zilitokea baina ya wajumbe ambao wanamuunga mkono yeye na wa mpinzani wake.
Mtasha alidai kuwa yeye alikuwa anaungwa mkono na wajumbe wa wilaya tano za Mbarali, Ileje, Rungwe, Mbozi na Chunya. Akizungumzia vurugu hizo, aliyekuwa mgombea ubunge Mbeya Vijijini kwa tiketi ya CUF na baadaye kujiunga Chadema, Daud Mponzi, alisema uchaguzi huo ni wa kwanza kufanyika ndani hivyo ni jambo la kawaida kutoelewana.
Hata hivyo, alishauri kuwa ni vizuri wagombea wakakaa na kushauriana juu ya namna ya kuendesha uchaguzi huo badala ya kufanya vurugu ambazo hazina maslahi kwa mtu yeyote yule. Mjini Sumbawanga, Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi, aliibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mkoa na kuwa Mwenyekiti.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Martin Juju, kutoka makao makuu ya chama hicho, alisema wanachama wa Chadema wanapaswa kutambua kuwa wamechaguliwa kwa lengo la kukikuza chama hicho na si kufurahia nyadhifa walizopata.
Alisema hivi karibuni utafanyika uchaguzi wa serikali za mitaa, wao kama viongozi wana wajibu wa kuhakikisha Chadema inaibuka na ushindi mkubwa, ili pia iwape nafasi wakati wa uchaguzi mkuu na kuwapa ushindi wa kishindo katika ubunge ambao wameuwekea mikakati ya kutosha na kutwaa majimbo mengi nchini. Katika uchaguzi huo, Juju alimtangaza Arfi aliyepata kura 38 na kumshinda Menrad Suwi aliyepata kura 10 kati ya 48 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano huo.
Alisema Ozem Chapita alipata kura 43 na kuwa Katibu huku mpinzani wake Charles Ndonde akipata kura 4 kati ya 47 zilizopigwa. Juju alimtangaza Katibu Mwenezi kuwa ni John Matongo aliyepata kura zote 47 zilizopigwa kutokana na mpinzani wake Suwi kujitoa dakika za mwisho.
Mjini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa alisema chama hicho kimesimamisha uchaguzi wa wagombea wa mikoa ya Mbeya na Mara baada ya kupata malalamiko juu ya wagombea. Alisema wagombea wa mikoa hiyo, walisimamishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, kutokana na malalamiko ya wajumbe, kuwa hawakuwa halali na kwa mujibu wa taratibu za Katiba imebidi kuchukuliwa hatua hiyo.
Mbeya na Mara jana tulisimamisha uchaguzi wao, yamekuwapo malalamiko ya msingi juu ya wagombea hao, hivyo tutaendelea kusimamia haki, alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa chama kiko makini na hawataruhusu kufanyika kwa hila, wala aina yoyote ya ufisadi katika kipindi cha uchaguzi wa viongozi wa chama hicho. Kuhusu hali inavyoendelea ya uchaguzi, alisema wanaendelea vyema na taratibu za kawaida za kurudisha fomu kwa ngazi ya Taifa kutokana na jana kuwa siku ya mwisho kurudisha.
Nimeshapokea fomu nyingi, ingawa siwezi kukutajia nani na nani waliorudisha hadi hapo kamati ya kuchambua itakapofanya kazi yake Agosti 29, alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa ngazi zinazogombewa na ambazo amepokea fomu za wagombea ni pamoja na ngazi ya uenyekiti, makamu mwenyekiti kwa Tanzania Bara na Visiwani, kiongozi wa vijana, wanawake na wazee. Mkutano mkuu wa Chadema, unatarajiwa kufanyika Septemba 3 hadi 4 ambapo utatanguliwa na wa Kamati Kuu na mabaraza matatu ya chama.
SOURCE: Habari Leo (25/08/2009)
Nawaombea wapenda demokrasia wezangu CHADEMA wafanye uchaguzi kwa hali ya usalama na amani; kuanzia hizi chaguzi za ngazi ya chini hadi ule Uchaguzi Mkuu.
All the best CHADEMA