HABARI MPYALA JANAMATANGAZOBEI ZETUWASILIANA NASITUMA HABARIjumatano, 2 septemba 2009
Yaliyopita
" 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 2009 2008 2007 2006
Pekua Tovuti


CHADEMA, kiberiti kimejaa
Absalom Kibanda
ZITTO Zubeir Kabwe, amefanikiwa kumtikisa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na chama hicho na kwa hakika bado anaendelea kukiweka roho joho wakati huu anapoendelea kujipanga kisiasa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Ni wazi kwamba mwangwi wa kishindo cha uamuzi wa Zitto kuamua kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya juu kabisa ya kimadaraka ndani ya chama hicho akikabiliana na Mbowe kabla hajafikia makubaliano na ushauri wa kamati ya wazee wa chama hicho bado unaendelea kukisika ndani na nje ya chama hicho.
Nikiwa miongoni mwa watu ambao tumekuwa tukiitakia mema CHADEMA na hata kuthamini kwa dhati mchango madhubuti wa viongozi wa chama hicho na wanachama wake katika kuimarisha mfumo wa ushindani wa vyama vingi tangu kuzaliwa kwake na hususan kuanzia mwaka 2005 walipomsimamisha Mbowe kuwa mgombea urais, nilipatwa na hofu kubwa kuhusu aina ya mabadiliko ya kiuongozi ambayo chama hicho kinaelekea kuyakamilisha wiki hii.
Si kwamba nilikuwa na hofu kwa kuwa nayaogopa mabadiliko ya kidemokrasia, bali kikubwa kilichokuwa kikinisumbua ni ukweli kwamba, chama hicho kilikuwa kikifanya mabadiliko wakati huu taifa linapojiandaa kwa ajili ya chaguzi kuu mbili, ule wa serikali za mitaa unaokuja siku chache zijazo na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani.
Hofu yangu kuhusu hofu hii ya mabadiliko ambayo yangeweza kuwa ya hatari, ilizidi kuongezeka kila mara nilipokuwa nikiyasoma magazeti ama ya serikali au yale yanayomilikiwa moja kwa moja kwa njia za panya na mawakala au makada wa kimikakati wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Nilipoanza kusoma habari katika magazeti hayo na kuona namna yalivyokuwa yakishabikia kwa mapana na marefu mpasuko ndani ya CHADEMA mara moja kengele ya hatari ilionekana kuanza kugonga kichwani mwangu na mwangwi wake ukanisukuma kuandika makala yangu ya wiki iliyopita iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho; ‘Naliona anguko la Zitto Kabwe'.
Kama hiyo haitoshi, mazungumzo ya ana kwa ana na yale ya njia ya simu ambayo niliyafanya na vijana mbalimbali walio ndani ya CCM wakiwamo wale walio na ushawishi mkubwa katika Jumuiya ya Vijana ya chama hicho tawala (UVCCM) na wabunge na kuwasikia namna walivyokuwa wakiufuatilia kwa umakini mkubwa uchaguzi wa CHADEMA na takriban wote wakisisitiza haja ya kufanyika kwa mabadiliko ya kiuongozi, mara moja niliiona hatari ikija.
Ilipofika hatua ya Zitto kuchukua fomu, ghafla homa ya uchaguzi ndani ya CHADEMA ikazidi kupanda na takriban vijana (siyo wote) wa CCM ambao wamekuwa na mawasiliano ya kirafiki na mwanasiasa mwenzao kijana kwa muda mrefu, walichukua maamuzi ya kumuunga mkono kwa nguvu kubwa na wote wakarejesha hoja nyingi zilizokuwa zikionyesha udhaifu mkubwa wa viongozi takriban wote wa chama hicho.
Ilipofikia hatua hiyo, mara Mbowe, Dk. Willibrod Slaa, Mnyika, Halima Mdee, Grace Kiwelu, John Mnyika na viongozi wengine wote wa CHADEMA ukimuacha Zitto wakaanza kuonekana kuwa ni watu wasiofaa, wakionekana kuwa hivyo ndani ya chama hicho na nje.
Katika mnyumbuliko huo huo, ndani ya CHADEMA ghafla taswira ya Zitto mwenyewe ikaanza kujipambanua na hali ikazidi kuwa bayana aliporejea kutoka nchini Ujerumani alikokuwa amekwenda kwa shughuli maalum ya ushauri kwa rais wa nchi hiyo. Nguvu zake halisi zikaanza kubainika.
Kile ambacho awali kilionekana kuwa ni uamuzi wake wa kujaribu kutikisa tu kiberiti kikaanza kubadilika kwa haraka na mara Zitto akajitokeza na kuwa tishio la wazi kwa uenyekiti wa Mbowe na kwa hakika akaanza kuwa tishio la majaliwa ya kisiasa ya chama hicho na kambi nzima ya upinzani wakati huu akili za Watanzania wadadisi wa mambo wanapoangalia mustakabali mwema wa ushindani mkali wa kidemokrasia hapa nchini.
Ni bahati tu kwamba kiberiti kingali kimejaa.
Kwa hakika tafsiri yangu ya haraka haraka ikanipa jibu moja tu tena la haraka kwamba, maamuzi hayo ya Zitto yalikuwa kwa makusudi kwa ujinga wa wapambe wake wa kushindwa kuona mambo kuwa ulikuwa ikilenga kumhakikishia Rais Jakaya Kikwete ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 80 alizokuwa amezipata mwaka 2005.
Ingawa baadhi ya watu wanaweza wakadhani mimi ni mwendawazimu ninapoliangalia tukio la Zitto kugombea uenyekiti wa CHADEMA wakati huu na kuwapo kwa jitihada za makusudi za kumsafishia Kikwete njia mwaka ujao, ukweli unabaki pale pale kwamba, makosa yoyote ya kisiasa yanayoweza kufanywa na viongozi waadilifu ndani ya vyama viwili vya CUF na CHADEMA wakati huu, yana nafasi kubwa ya kumhakikishia Rais wetu ahueni kubwa.
Ukiliacha hilo, mara moja nikakiona kitendo hicho cha Zitto mwanasiasa ambaye siku zote nimekuwa nikimuunga mkono anaposimamia na kupigania masuala ya msingi, cha kuamua kuutumia vibaya mwanya wa kidemokrasia wa kugombea uenyekiti wa taifa wa CHADEMA kuwa kilichokuwa kikilenga kwa kujua au kutojua, kupunguza makali na kasi ya chama hicho cha kushinda viti vingi katika chaguzi za serikali ya mitaa, udiwani na baadaye ubunge.
Nilipojiridhisha kwamba hayo yote yanaweza kutokea kwa sababu tu ya uamuzi wa Zitto kugombea uenyekiti na yakafuata hata kama atashinda au kushindwa katika mchuano huo, nikaona nitakuwa sikuitendea haki ndoto yangu ya siku zote ya kuona demokrasia ya vyama vingi inastawi katika nchi hii ambayo kwa takriban miaka 20 tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi CCM imeendelea kujivunia rekodi madhubuti dhidi ya upinzani.
Nilipoamua kuandika makala ya karipio na onyo dhidi ya Zitto katika safu hii, baadhi ya wasomaji wangu kwa makusudi au kwa kutojua wakakimbilia kuanza kunihukumu wengine wakisema najipendekeza kwa Mbowe ambaye ni mwajiri wangu, naganga njaa, nakandamiza demokrasia na wengine wakasema eti namzuia Zitto kutumia kipaji chake cha uongozi.
Ushawishi wote wa kundi hilo, ambao kwa kiwango kikubwa ulichagizwa na upotoshwaji mkubwa wa hoja yangu uliokuwa ikiratibiwa kwa karibu na vijana wa ndani wa CHADEMA waliokuwa wakimpigania Zitto na wale wa CCM na mawakala wao serikalini ulishindwa kulizuia Baraza la Wazee wa chama hicho, kumuacha kabla ya kumzuia kijana wao, kukiingiza chama chake na taifa katika balaa kwa kumsafishia Kikwete na chama chake mteremko. Ni jambo la kheri kwamba Zitto kwa dhati au kwa shingo upande aliliona hilo.
Kama alivyoandika Ansbert Ngurumo katika safu yake ya Maswali Magumu katika gazeti hili Jumapili iliyopita, Zitto na wapambe wake ambao nilifikia hatua ya kuwaita wajinga ambao waliamua kufumba macho na kuendelea kushangilia makosa ya kumruhusu Zitto kukimega chama ambacho siku zote amekuwa akionyesha kwa vitendo kubwa anakipenda kwa dhati wanapaswa kutulia na kutafakari kwa kina ni kitu gani hasa CCM na mawakala wake walikuwa wakikitafuta kutoka kwake hata ghafla kuanza kukiombea CHADEMA mema?
Kwa hakika unahitaji kuwa na akili za kuku za kusahau mapema ili kujidanganya kwamba, vijana ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji au wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wabunge, mawaziri na wanasiasa wengine serikalini wanaweza wakawa na mapenzi mema na CHADEMA hata kukiombea mema chama hicho wakati huu wakijua kuwa mwelekeo wa taifa ni Uchaguzi Mkuu ujao.
Hivi kweli wanasiasa katika vyama vya upinzani na Watanzania wengine hawajui kwamba, ndani ya vikao takriban vyote vya CCM na jumuiya zake, katika miezi na siku za hivi karibuni wamekuwa wakijadili namna wanavyoweza kushiriki katika kudhoofisha nguvu za CHADEMA kwa Tanzania Bara (baada ya kuidhoofisha CUF) na CUF kwa upande wa Zanzibar?
Hivi akina Mbowe, Slaa, Zitto, na wazee wa chama hicho wanaoongozwa na Mzee Edwin Mtei wamechukua hatua gani ili kuanzisha mchakato mahususi wa kufanya uchunguzi wa kina utakaowawezesha kubaini ni kwa kiwango gani nguvu za kifedha au za kiushawishi kutoka CCM na kwa mawakala wake zimefanikiwa kupenya akili za vijana na wazee wengi ndani ya chama hicho pasipo kujua au kwa kujua kiasi cha kujikuta wakiwa majeruhi wa kushabikia ujinga ambao kwa vyovyote vile matokeo yake yalikuwa yakiwachulia wao na chama chao anguko la kihistoria?
Maswali kama hayo tunapaswa kujiuliza hata sisi wana habari ambao kama ilivyokuwa kwa vigogo hao wa CHADEMA kwamba ni kwa kiasi gani kalamu zetu zimechochea au kudhoofisha jitihada mahususi ambazo ziko wazi na zinazolenga kukisambaratisha chama hicho cha upinzani ambacho hakuna shaka kimejipambanua kuwa chama shupavu katika miaka ya hivi karibuni?
Wakati sote tukitafuta majibu ya maswali hayo, tunao wajibu wa kutambua kwamba, pamoja na uamuzi wa Zitto kutangaza kujitoa katika kinyang'anyiro cha uenyekiti, ile sumu kali ambayo tayari imeshapenya mishipa ya uongozi ya chama hicho, haina budi kutafutiwa dawa mahususi ya kuipatia tiba ya haraka kwani tayari vijana wa kazi wa CCM na mawakala wao wameshatamba kwamba wameshakiachia vidonda vingi chama hicho ambavyo wanadai vitaendelea kukitesa hadi wakati wa chaguzi zijazo. Kwa sababu hiyo basi, ninaweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba, kile ambacho leo hii kinaendelea kuelezwa na kusisitizwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa ni demokrasia kandamizi ya ndani ya CHADEMA (eti kwa sababu ya uamuzi wa wazee wa CHADEMA kumzuia Zitto kugombea uenyekiti) si tu kwamba ni majuto ya kukwama kwa ajenda yao, bali ni mkakati mbadala wa kuendelea kukiumiza chama hicho kwa malengo ya kisiasa. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.