• Zitto asema anamheshimu, hana kinyongo
na Mwandishi Wetu
HATIMAYE, washindani wakuu wawili katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Zitto Kabwe, jana walimaliza upinzani kwa kushikana mikono, kuashiria mshikamano na umoja katika chama hicho.
Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa anayemaliza muda wake, na Zitto ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, walifikia hatua hiyo, ikiwa ni siku moja tu tangu Zitto awasilishe barua mbele ya
Baraza la Wazee, kuondoa jina lake katika kinyang'anyiro hicho.
Viongozi hao walifikia hatua hiyo katika kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichofanyika katika Hoteli ya Keys iliyoko Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Habari ambazo Tanzania Daima ilizipata kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa, Zitto ambaye uamuzi wake wa kuchukua fomu uliibua mjadala mzito ndani na nje ya nchi, alitoa kauli iliyoashiria wazi kumaliza upinzani uliojitokeza tangu alipochukua fomu.
Kwa hatua hiyo ni dhahiri kuwa
Mbowe ana nafasi kubwa ya kupitishwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) na wale wa Baraza Kuu, kabla ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Septemba 4.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms), Zitto alisema amekubali kujitoa ili kuweka mbele umoja wa chama.
"Namheshimu sana Mbowe
na wewe unajua. Wala siwezi kumvunjia heshima. Nimekubali kujitoa ili kuweka mbele umoja wa chama. Kama nimeyumba ni kwa ajili ya kukienzi chama, suala la uenyekiti limepita na sasa naangalia mbele kujenga chama. Mimi sina kinyongo," alisema Zitto.
Katika hatua nyingine, CC imepitisha jina la Mbowe kuwa mgombea pekee wa nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho taifa.
Mbali ya kupitisha jina la Mbowe, CC pia imeridhia uamuzi wa Zitto kujitoa kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa chama hicho.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya kikao zilisema kuwa,
CC imefikia uamuzi huo ili kumpa nafasi zaidi Mbowe ambaye katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
amefanya kazi kubwa ya kukiimarisha chama hicho kwa kiasi cha kukubalika na Watanzania wengi.
"
Kamati Kuu imepitisha jina la Mbowe, pia imeridhia barua ya Zitto,
hakukuwa na matatizo kupitisha jina hilo, na Zitto ametoa kauli nzuri yenye kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, tofauti kabisa na taswira iliyokuwa inaonyeshwa na baadhi ya vyombo vya habari," alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.
Hata hivyo, Kamati Kuu hiyo ilikuwa ikiendelea kupitisha wagombea wa nafasi nyingine ya Makamu Mwenyekiti, ambayo inawaniwa na watu wanne.
Zitto, aliwasilisha barua yake ya kujitoa katika mchuano huo juzi asubuhi.
Kabla ya Zitto kuwasilisha barua yake hiyo, alikuwa ameitwa kuhojiwa na Baraza la Wazee wa chama hicho linaloongozwa na Mwenyekiti mstaafu, Edwin Mtei.
Wakati akiwa katikati ya mahojiano hayo, Zitto aliwasilisha barua yake ya kuamua kujitoa, akisema anafanya hivyo ili kurejesha umoja na mshikamano ndani ya chama, ambao unaweza kupotea kutokana na kugombea nafasi hiyo na mwenyekiti wake.
Uamuzi wa Zitto kujitoa katika mchuano huo, umekuja siku kadhaa baada ya hatua yake ya kugombea kiti hicho kuzusha mjadala mkali ndani na nje ya nchi.
Kuibuka kwa mjadala huo, kwa kiwango kikubwa kumetokana na hatua ya mwanasiasa huyo kijana na mwenye ushawishi bungeni, kuamua
kukabiliana na Mbowe.
Uamuzi huo wa Zitto, ulionekana kuwashtua viongozi mbalimbali wa juu na wazee wa chama hicho.
Mbali ya hao, uamuzi huo ulikwenda mbele zaidi na kugusa mijadala ndani ya vyama vingine vya siasa, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), CUF, NCCR- Mageuzi na TLP.
Makada kadhaa wa CCM waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema, mabadiliko ya uongozi ndani ya CHADEMA ni jambo linalofuatiliwa kwa karibu.
Ukikiacha chama hicho tawala, uamuzi huo wa Zitto kugombea uenyekiti na kuchuana na Mbowe, ulionekana kuungwa mkono na wakati mwingine kushangiliwa na viongozi wa vyama vingine vya upinzani.
Hata hivyo, kikubwa kilichokuwa kikivuta hisia za watu wengi ni madai ambayo Zitto mwenyewe aliyakanusha mara kadhaa kwamba, uamuzi wake wa kugombea uenyekiti wa chama hicho ulikuwa na
msukumo kutoka nje ya CHADEMA.
Maandishi ya Kibanda kwenye Tanzania Daima amefurahi kiasi cha kurudiarudia maneno.Mzee Mtei ameonesha ubaguzi wa wazi kwa kuwa mwenyekiti wa kikundi cha wazee wenye Chama ambao wamemzuia Zitto.kisheria kutokana na mgongano wa kimaslahi Mzee Mtei hakutakiwa kushiriki kikao hicho kwani Mbowe ni Mwanawe/Mkwe wake.ilitakiwa Mwanasheria wa Chadema apinge ushiriki wa Mzee Mtei kwenye hili kwani Zitto hatendewi Haki.