Mama Zitto afyatuka, uchaguzi Chadema wafutwa
MAMA mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kabwe Zitto amesema, mwanae si fisadi na hanunuliki.
Amesema, viongozi katika makao makuu ya chama hicho ni 'wachafu', wanakiharibu chama.
Shida Salum amesema, Zitto hanunuliki na hawezi kununuliwa. Amesema leo Dar es Salaam kuwa, ofisi ya Makao Makuu ya Chadema itakiharibu chama hicho na anasikia aibu mwanae kutajwa kuwa ni mmoja wa mafisadi katika chama hicho.
Mwanachama huyo wa Chadema amesema, ofisi ya Makao Makuu Chadema imeingiliwa, na kwamba, chama hicho kimechafuka.
Salum ameyasema hayo mara baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa kufungua mkutano wa uchaguzi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA).
Mimi fomu ya Zitto niliifukiza nyumbani kwangu, Zitto sio fisadi, hanunuliki na hawezi kununuliwa, amesema mama Zitto.
Amesema,amekuwa katika chama hicho tangu mwaka 1992, na anasikia aibu sana zinapoibuka taarifa sasa kwamba mwanae ni miongoni mwa mafisadi.
Alisema amekuwa akifika katika ofisi ya makao makuu kila mara kuomba kuonana na Katibu Mkuu (Slaa) ili wazungumze kuhusu viongozi wanaomharibia chama,na wanaotaka kukigawa chama.
Siwezi kumkataa Zitto, katika uchaguzi huu ofisi imeingiliwa, jirekebisheni, chama kimechafuka, hali ambayo inafanya watu kukiogopa chama, amesema Mama huyo huku akishangiliwa na umati mkubwa wa kina mama waliofika kwa ajili ya uchaguzi huo.
Muda mfupi baada ya mama Zitto kuzungumza, Mwenyekiti wa Wanawake mkoa wa Dodoma, Sakina Sare, alisema yapo matatizo ya kiutendaji ndani ya viongozi wa makao makuu ya chama.
Amesema yeye aliingia kwenye chama tangu 1994,amewataka viongozi wa Chadema kuwasikiliza wanachama wake ikiwa ni pamoja na kupokea matatizo yao.
Kwa mfano, leo tunakaa katika uchaguzi wa Baraza la Wanawake, wakati huo huo fomu za kushiriki katika uchaguzi hazikuwafikia walengwa, hazikupatikana, amesema Sakina.
Amesema ipo haja kwa makatibu wakuu wa mikoa kuangaliwa kwa makini ili chama kisigawanyike au kutoa taswira mbaya kwa wengine.
Aliyekuwa Katibu wa wanawake katika mkoa wa Kagera, aliyefahamika kwa jina moja Ramlaza, alisema wanachama wamekuwa na manung'uniko mengi kuhusiana na uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kutopata fomu za ushiriki.
Amesema, maeneo mengine fomu za wagombea zilichelewa hivyo kuonesha utendaji dhaifu kwa ofisi ya makao makuu ya chama.
Dk. Slaa amewaomba radhi lakini amesisitiza kuwa, kama shutuma zilizotolewa na Mama yake Zitto ni za kweli basi hata mwanae ni mmoja wa viongozi wa chama hicho.
Katika hili la Mama yake Zitto siwezi kusema lolote, mimi ni Katibu Mkuu, mwanae Zitto ni Naibu Katibu, hivyo kama anaushutumu uongozi wa chama makao makuu, hata mwanae yupo katika kundi hilo, amesema Dk. Slaa.
Dk Slaa amesema, anafahamu kwamba, mafisadi wanawatumia vijana ndani ya chama hicho, atawafuatilia na kuchukua hatua dhidi yao kwa sababu chama hakitoruhusu kuyumbishwa ama kuwepo kwa makundi.
Wakati anafungua mkutano huo, Dk. Slaa aliwataka wanachama hao kutamka hadharani kama kuna mianya ya rushwa ndani ya chama hicho katika mchakato huo wa uchaguzi.
Alisema asiyetamka hadharani kama kuna sura hiyo, hizo zitakuwa propaganda za kisiasa, na kwamba, hawataacha kupambana na ufisadi.
Aidha, alisema chama kimeletewa taarifa kwamba watu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanasambaza kitabu cha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, marehemu Chacha Wangwe.
Alisema yeye binafsi hana matatizo na kitabu hicho lakini anahofia yayliyomo ndani kwa kuwa CCM ilianza kutoa waraka wa wangwe Julai 27, 2008 siku moja kabla ya kifo chake.
Kwa maana hiyo CCM walijua fika kuwa Chacha angekufa? Na kwa nini waraka huo ulitolewa na ofisi ya katibu Mkuu CCM Dodoma,? Alihoji Dk. Slaa wakati akiwaeleza wanawake hao kujihadhari kwa kuwa si kila mwanachama ni mwema.
Amesema, hoja inapoingizwa ndani ya chama lazima wawe makini na waijadili kwa kina bila kuzembea.
Kuhusu uchaguzi wa Baraza Kuu la vijana, alisema alipata taarifa jana usiku saa 3:00 kwamba zimetokea vurugu hivyo wanahitaji ushauri.
Alisema alizungumza na vijana takribani 110 usiku huo, wakitoa malalamiko yao kadhaa.
Amesema miongoni mwa malalamiko waliyotoa vijana hao ni pamoja na kuwepo kwa sura ya fedha kutembea ndani ya uchaguzi, wagombea kugawa karatasi za kupigia kura, na idadi ya kura kuongezeka.
Dk. Slaa alisema kutokana na hali hiyo, ilibidi kuitisha kikao cha dharura huku akiwa amewashirikisha baadhi ya wazee ambao kwa pamoja walikubaliana kuufuta uchaguzi huo, utafanyika ndani ya miezi sita.