Usalama wa Taifa na changamoto mpya
Evarist Chahali
Machi 30, 2011
Wakati umefika iache kuwa kitengo cha ushauri cha CCM
KILA mwisho wa mwaka, jarida maarufu duniani la TIME (la Marekani) huwa na utaratibu wa kumtangaza "mtu wa mwaka" (Person of the Year). Mwaka 2004 tuzo hiyo ilikwenda kwa Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush.
Katika mahojiano yake na jarida hilo, Rais Bush alitoa kauli moja ambayo kwangu imebaki kuwa nukuu muhimu. Kwa kifupi, alieleza kwamba ukisema kitu au kutenda jambo, na kisha wakajitokeza watu kukupinga au kukuunga mkono, basi, kwa vyovyote vile ulichosema au kutenda kimewagusa wanaopinga au kupongeza. Maana; kama kisingewagusa, wasingepoteza muda wao kukupinga au kukupongeza.
Katika Raia Mwema, toleo la Oktoba 13, 2010, kulikuwa na
makala yangu iliyohoji iwapo tuhuma zilizotolewa na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kuwa Idara ya Usalama wa Taifa inamhujumu zinaweza kuwa kweli au la.
Makala hiyo iliyobeba kichwa: Ni kweli mashushushu hutumiwa kuhujumu uchaguzi? ilimuibua msomaji mmoja aliyejiita Almasi Kajia ambaye aliijibu makala yangu kwa kueleza kuwa "
kazi ya mashushushu ni usalama si kuhujumu uchaguzi".
Kwa kuzingatia ‘hekima' za Bush, kuibuka kwa Kajia kujibu makala hiyo kunamaanisha aliguswa. Sasa kama aliguswa kama mzalendo au mtu mwenye maslahi kwenye taasisi hiyo, si suala la msingi.
Awali, sikutaka kumjibu lakini ukimya wangu wa muda mrefu ungeweza kuleta tafsiri potofu kuwa niliafikiana na utetezi wake kwa taasisi hiyo nyeti nchini mwetu.
Kwamba jukumu kuu la Idara hiyo ni usalama, hilo halina ubishi; kwani hata jina lake linaashiria hivyo. Lakini hata kazi ya askari wa usalama barabarani ni kuhakikisha usalama barabarani. Lakini, Kajia na wengine wote, tunajua namna trafiki wetu walivyogeuka ‘mamlaka ya mapato kwa njia ya rushwa'.
Hoja yangu hapa ni kwamba taasisi kuwa na jukumu fulani haimaanishi kuwa lazima inatekeleza jukumu hilo ipaswavyo. Na ni katika namna hiyo hiyo Idara ya Usalama wa Taifa kuwa na "kazi ya usalama" haimaanishi kuwa wanatekeleza jukumu hilo kwa ufanisi; japo si tu wanapaswa kufanya hivyo; bali lazima wafanye hivyo.
Si siri kwamba kushamiri kwa ufisadi Tanzania ni dalili za wazi kuwa taasisi hiyo haitekelezi wajibu wake ipaswavyo. Licha ya kanuni ya usiri kuendelea kuisadia idara hiyo kuogopwa na wengi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mafisadi, kadri siku zinavyokwenda ndivyo taasisi hiyo inavyozidi kuonekana kama ‘mbwa asiye na meno'.
Idara ya Usalama wa Taifa haina sababu yoyote ya msingi ya kuiacha Tanzania ikielekea kusikoeleweka.Watumishi wa idara hiyo wanatimiziwa kila hitaji lao la kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Lakini hiyo haikuweza kuzuia ujambazi wa EPA, utapeli wa Richmond, mazingaombwe ya Dowans, na mengineyo yanayofanya ufisadi kuonekana kana kwamba ni kipengele muhimu kwenye Katiba ya nchi yetu.
Tatizo la msingi la chombo hiki muhimu lipo kwenye kuishia kushauri tu. Wanakusanya taarifa, wanazichambua, na kisha wanashauri. Basi. Lakini hata ushauri wao ukipuuzwa,wao wanaona wameshatimiza wajibu wao.
Taasisi hiyo inafahamu fika kuwa popote pale ilipo, kuna nyakati inalazimika kulazimisha ushauri wake ufuatwe kwa maslahi ya Taifa. Wanajua sana namna ya kulazimisha ushauri wao ufuatwe kwa maslahi ya Taifa, lakini kwa sababu wanazojua wenyewe wameendelea kuridhika na nafasi yao ya ushauri tu.
Binafsi, naamini kuwa kama idara hiyo ingeamua kwa dhati kutimiza wajibu wake ipaswavyo, hii hali ya sasa ya kukithiri kwa ufisadi nchini, ingekomeshwa. Sambamba na hilo, viongozi wasio na uwezo wala maadili ya uongozi wasingejipenyeza hadi ngazi za juu za uongozi nchini.
Maana; ikiamua, idara hiyo inaweza kabisa kukabiliana na majambazi walioingia kwenye siasa kwa lengo la kukwangua kila raslimali ya nchi hii. Yote hayo yanawezekana iwapo kanuni za asili na taratibu za utendaji kazi zitafuatwa ipaswavyo, na kuweka kando ‘uswahiba'.
Tuwe wa kweli. Hivi kama Idara ya Usalama wa Taifa inatoa ushauri mzuri, lakini unaishia kupuuzwa, si kwa vile una mapungufu, bali unakwaza maslahi ya kundi fulani, kwa nini mbinu nyingine zisitumike kuwashughulikia wahusika?
Kuwa na rundo juu ya rundo la mafaili kuhusu fisadi fulani; huku fisadi huyo akizidi kuikongoroa nchi, ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
Lakini tatizo jingine linaloiharibu taasisi hii nyeti ni kuendelea kwake kuwa kama ‘Kitengo cha Usalama cha CCM '. Majambazi wa kisiasa na kiuchumi wanafahamu ukweli huo, na ukaribu wao na chama hicho - kama wafadhili au viongozi unawapatia si tu hifadhi; bali pia ukaribu na idara hiyo.
Tatizo hili ni la kihistoria na kiuongozi zaidi. Kihistoria, kwa vile katika zama za mfumo wa chama kimoja, taasisi hiyo ilikuwa ni chombo muhimu katika utendaji na ustawi wa chama tawala. Mageuzi katika mfumo wa siasa yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi yaliharamisha vyombo vya dola kujihusisha na siasa. Kwa bahati mbaya, haramisho hilo limeendelea kuwa la kinadharia zaidi kuliko kivitendo.
Kadhalika, kikatiba, Rais ndiye ‘mlaji' mkuu (consumer) wa taarifa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa. Hadi hapo, hakuna tatizo. Lakini Rais huyo huyo ndiye Mwenyekiti wa CCM. Sasa kwa vile siasa zinapewa kipaumbele zaidi ya maslahi ya Taifa, uwezekano wa CCM kuitumia idara hiyo kupitia nafasi ya Rais kama Mwenyekiti wa chama hicho, ni suala la wazi kabisa. Hilo si tatizo tu; bali ni jambo la hatari hasa kama itatokea nchi kuangukia mikononi mwa rais dhaifu kweli kweli.
Lakini laiti maslahi ya Taifa yangewekwa mbele ya maslahi ya kisiasa, pengine isingekuwa vigumu kwa taasisi hiyo kuhakikisha rais hatumii "kofia zake mbili" kukinufaisha chama chake kwa sababu, kwa kiasi kikubwa, maisha ya kila siku ya rais yapo mikononi mwa taasisi hiyo.
Kiungozi, teuzi nyingi za viongozi wa taasisi mbalimbali zimekuwa zikielemea zaidi kwenye maslahi binafsi ya anayefanya uteuzi badala ya uwezo wa wateuliwa au manufaa kwa umma. Matokeo yake ni wateuliwa kuwa wanyenyekevu kupita kiasi kwa aliyewateua; huku wakiendelea kujiona wadeni wa fadhila kwa kuteuliwa huko.
Teuzi zinazofanywa kwa misingi ya urafiki zinasababisha hali ya kulindana. Hali huwa mbaya zaidi katika mazingira ambamo mteuliwa anafahamu "machafu" ya mfanya uteuzi, na uteuzi huo unakuwa wa ‘kulinda kopo la uozo lisifunguke'.
Laiti tungekuwa na mfumo wa uwajibikaji ambapo watawala katika ngazi mbalimbali hawakurupuki tu na kuamua fulani awe fulani, mambo yasingekuwa hovyo kama yalivyo hivi sasa.
Katika ngazi za juu, pengine yafaa jina la mteuliwa kupelekwa Bungeni na "wawakilishi wa umma" wakauwakilisha umma kumpitisha au kumkataa mteuliwa aliyependekezwa. Kama ili mtu aajiriwe, japo kuwa mesenja tu ni lazima afanyiwe usaili, iweje basi watu wanaokabidhiwa majukumu makubwa kabisa na nyeti kama ya kuongoza Idara ya Usalama wa Taifa, wateuliwe na rais tu?
Nimalizie kwa kuikumbusha Idara yetu ya Usalama wa Taifa kwamba angalau hadi sasa bado ina heshima kidogo miongoni mwa Watanzania wengi. Lakini heshima hiyo inamomonyoka kwa kasi kwa jinsi inavyoshindwa kukabiliana na ufisadi unaootesha mizizi nchini. Sababu zipo nyingi tu kwa idara hiyo kuanza kujitazama upya.
Blogu:
KULIKONI UGHAIBUNI