Moja ya mambo yanayofanya uhusiano kati ya China na nchi za Afrika uwe imara ni upande wa China kufuata falsafa ya jadi ya China, yaani “usiwatendee wengine kile usichotaka kutendewa”. Falsafa hii si kama tu inatokana na machungu ya ubeberu wa nchi za nchi za magharibi dhidi ya China katika enzi ya Qing (1644 - 1912), lakini pia inatokana na moyo wa wachina wa kupenda kuona watu wote wanaondokana na taabu. Nchi za Afrika zimetambua kuwa ushirikiano na China ambayo sera yake ya kidiplomasia inaongozwa na falsafa hii, ni salama na wenye manufaa.
Kwenye ushirikiano uliopo kati ya China na nchi za Afrika, udhati, urafiki na usawa ni mambo ambayo yamekuwa yanazingatiwa. Machoni wa viongozi wa nchi za Afrika, China ni nchi yenye udhati, na kama ikiahidi jambo fulani kwenye ushirikiano kati yake na nchi za Afrika basi jambo hilo huwa linatekelezwa kama lilivyoahidiwa. Kuna mifano kadhaa ya mambo iliyoahidi China katika kipindi cha miaka kumi iliyopita na utekelezaji wake sasa unaonekana.
Kupitia mikutano mbalimbali ya baraza na Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), China iliahidi kutoa mafunzo kwa wataalam wa Afrika, kuongeza uagizaji wa bidhaa kutoka Afrika na hata kusaidia ujenzi wa miundo mbinu ikiwa ni pamoja na barabara, reli na viwanja vya ndege. Ahadi hizi zimetekelezwa kwa viwango tofauti. Ahadi ya hivi karibu kabisa ile iliyotolewa na Rais Xi Jinping kuhusu chanjo ya kuisaidia Afrika kupambana na janga la COVID-19, ambayo karibu kila nchi ya Afrika imenufaika nayo. Haya ni baadhi ya mambo yanayoonesha udhati wa China.
Umaalum mwingine unaonekana kwenye ushirikiano kati ya China na Afrika ni kuzingatia umma. Serikali ya China na chama cha kikomunisti mara zote kipaumbele kwenye utendaji wake ni watu, kutokana na kuamini mamlaka waliyonayo inatokana na umma na kazi zote zinatakiwa kutoa kipaumbele kwa maslahi ya umma. Uwekezaji kwenye miradi mingi inayotekelezwa na China barani Afrika imekuwa ikitoa kipaumbele kwenye kunufaisha umma. Tukiangalia miradi mingi inayojengwa, tunaweza kuona kuwa ni ile inayotoa ajira nyingi kwa wenyeji, na pia inachochea sekta nyingine kuendelea na kuwanufaisha watu wa kawaida.
Pengine ambacho kimesifiwa zaidi katika kipindi hicho cha miaka 10, ni China kuendelea kuziheshimu nchi za Afrika na kuziunga mkono zinapohitaji uungaji mkono. Moja ya changamoto kubwa zilizoko kwenye uhusiano kati ya baadhi ya nchi kubwa za magharibi na nchi za Afrika, ni nchi za magharibi kujifanya walimu wa nchi za Afrika. Kuna wakati wanatumia nguvu na ushawishi wao kuzishinikiza nchi za Afrika kufanya mambo ambayo nchi za Afrika hazitaki, na wakati fulani baadhi ya hayo mambo ni kinyume na maadili ya tamaduni za waafrika. China imeendelea na utaratibu wa kukaa na kujadiliana na nchi za Afrika kuhusu mambo ya ushirikiano bila kujifanya yenyewe ni mwalimu, badala yake inakaa na kujadili na hatimaye kufikia makubaliano kwa kuzingatia heshima na maslahi ya pande zote.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuheshimiana na kutafuta maendeleo ya pamoja, sio tu kumekuwa msingi wa mahusiano kati ya China na Afrika, lakini pia kumezifanya nchi za Afrika zijenge imani ya kisiasa kuwa China itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika katika hali ya usawa.