Huu mjadala ungekuwa na faida sana kama wachangiaji watatafakari zaidi ya ''kufungwa akili kwa dini zao''.
Kinachojadiliwa hapa sio ubaya wa dini wala ubaya wa Madrasa, ni upotovu uliokithiri wa baadhi ya walimu wa Madrasa.
Hapa jirani na kwangu kuna Madrasa, watoto wanaingia saa 12 mpaka saa 2 usiku. Nimependa utaratibu ambao wazazi wamejiwekea. Nilimuuliza jirani yangu, yeye ana asili ya Uarabani ( Yeye ni mtanzania mwenye asili ya Oman), kuhusu kwanza umuhimu lakini pia usalama wa watoto kwa muda huo wa usiku haswa kutokana na hivi vitendo. (Tulikuwa tunajadili ulawiti uliofanyika Tabora, miezi michache).
Kwanza alinionyesha umuhimu wa elimu hizo zinazotolewa Madrasa. Hapa nikaona umuhimu wa mafundisho sahihi ya dini kwa watoto.
Lakini akasema wao kwa utaratibu wa wazazi kwanza wanahakikisha kuwa hawana mwalimu mmoja wa Madrasa, wao wana walimu watatu; hapa akasema lengo ni kuwa ukiwa na watu tofauti ni ngumu kukuta wenye akili sawa.
Pia hawa walimu wamepewa miongozo na taratibu za kazi, ikiwemo kukutana na wanafunzi wote kwa wakati mmoja.
Hakuna muda wala jambo la kumkutaniusha mwalimu wa madrasa akiwa peke yake na mwanafunzi. Kama una jambo binafsi na mwanafunzi basi wasiliana na mzazi/wazazi wake.
Jambo la pili, wao wameajiri wadada wawili (Waislam) ambao wanakuwa eneo la Madrasa muda wote masomo yanapotolewa. Hawa kazi yao ni usafi wa madrasa na masualau mengine, lakini pia wana kazi maalumu ya kuhakikisha baada ya masomo, watoto wote wanatoka na kurudi nyumbani.
Maana walimu wengi wa madrasa hutumia sababu za mtoto kuwahi ama kuchelewa kuondoka ili afanye zamu ya usafi.
Labda hawa wameweza kwa sababu ya aina ya watu, wengi wana kipato kizuri na naona pia wamepata elimu dunia hivyo wanatambua umuhimu wa dini lakini pia vichwa vyao vinafikiri sawasawa kuhusu watu na tabia zao.
Ukweli ni kwamba, wazazi lazima tukubali kufikiri zaidi ya mapenzi yetu ya kutetea dini. Dini haina shida lakini watu wenye dini bado wana mambo yao.
Hoja kwamba hata kwenye dini nyingine haya mambo yanatokea, ni hoja dhaifu ya mtu asiye na uwezo wa kufikiri sawasawa, kama huko yanatokea sio tiketi kuwa huku napo yatokee.
Tuokoe kizazi chako, elimu ya dini ni muhimu lakini sio juu ya udhalilishaji wa utu wa watoto wetu.