Kuna mstari mwembamba sana kati ya Serikali na Chama tawala, hiyo inachangia changamoto nyingi za Kidemokrasia Tanzania

Kuna mstari mwembamba sana kati ya Serikali na Chama tawala, hiyo inachangia changamoto nyingi za Kidemokrasia Tanzania

Nchachali

New Member
Joined
Nov 29, 2025
Posts
3
Reaction score
2
Katika mifumo ya kidemokrasia Duniani, moja ya nguzo kuu za uchaguzi huru na wa haki ni kutenganishwa kwa Serikali kama taasisi ya umma na vyama vya siasa kama washindani wa uchaguzi.

Hata hivyo, katika baadhi ya nchi zinazoendesha mfumo wa vyama vingi baada ya historia ndefu ya chama kimoja, mpaka huo hubaki kuwa dhaifu na wenye utata.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabili mjadala huo, hususan wakati wa kampeni za uchaguzi, ambapo matumizi ya mali za umma huibua maswali ya usawa wa ushindani, uhalali wa kikatiba na imani ya wananchi kwa demokrasia.

Habari hii ya uchambuzi inachambua kwa kina mpaka mwembamba uliopo kati ya mali za Serikali na maslahi ya vyama vya siasa, kwa kuzingatia mitazamo ya kisheria na kisiasa kutoka kwa wadau waliobobea.
IMG_5626.jpeg
Akizungumza na moja ya Chombo cha habari, Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Nelson Mazengo anasema chanzo kikuu cha tatizo hili kinatokana na historia ya kisiasa ya Tanzania.

“Japokuwa mwaka 1992 Tanzania ilihamia rasmi katika mfumo wa vyama vingi, misingi yake ya kisiasa bado imejengwa juu ya mfumo wa chama kimoja, Chama tawala kimeshika hatamu za dola kwa muda mrefu kiasi kwamba inakuwa vigumu sana kutofautisha kati ya Serikali na chama,” anaeleza Mazengo.

Kwa mujibu wake, dhana ya “kushika hatamu” inamaanisha kushika usukani wa mamlaka ya Dola, hali inayosababisha shughuli za Serikali na za chama kuonekana kama kitu kimoja, iwe ni kipindi cha kampeni au hata nje ya kampeni.

Mazengo anaeleza kuwa matumizi ya mali za umma, kama magari ya Serikali, miundombinu na ushawishi wa viongozi walioteuliwa, huathiri kwa kiasi kikubwa usawa wa ushindani wa kisiasa.

“Mgombea wa chama tawala anapokuwa na upatikanaji wa rasilimali za Serikali kwa namna ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, mpinzani wake anakosa mazingira sawa ya kushindana, Hili linaathiri msingi wa demokrasia,” anasema.

Anaongeza kuwa hata mfumo wa ruzuku kwa vyama vya siasa, unaotegemea uwakilishi wa Bunge, unaendelea kulifanya chama chenye wabunge wengi kuimarika zaidi kifedha, hali inayoongeza pengo kati ya chama tawala na vyama pinzani.

Kwa upande wa sheria, Wakili Emmanuel Chengula anaeleza kuwa Katiba ya Tanzania inaweka changamoto ya kipekee pale Rais anapokuwa mgombea wa urais.

“Katika mfumo wetu wa kikatiba, Rais anapogombea muhula mwingine habaki kuwa raia wa kawaida, Anaendelea kuwa Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na kiongozi wa Serikali hadi pale atakapokabidhi madaraka,” anafafanua.

Kwa msingi huo, anasema haiwezekani kisheria kumvua Rais ulinzi, itifaki na rasilimali za Serikali wakati wa kampeni, kwa sababu nafasi yake ya kikatiba bado ipo.

“Huwezi kusema nchi haina Mkuu wa Nchi kwa kipindi cha uchaguzi. Katiba inamlinda Rais kuendelea kutekeleza majukumu yake hata wakati wa kampeni,” anasisitiza.

Hata hivyo, Wakili Chengula anabainisha wazi kuwa sheria hairuhusu matumizi ya mali za Serikali kwa shughuli za vyama vya siasa.

“Vyama vya siasa si sehemu ya Serikali. Vinapokea ruzuku mahsusi kwa ajili ya shughuli za kisiasa. Kutumia mali za Serikali kwa kampeni ni matumizi mabaya ya madaraka na ni kosa kisheria,” anasema.

Kuhusu ulinzi, anaeleza kuwa vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, vina wajibu wa kulinda raia wote bila upendeleo, na hilo halipaswi kutafsiriwa kama msaada wa kisiasa.

Katika suala la uwajibikaji, Wakili Chengula anaitaja Tume ya Uchaguzi kuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha usawa.

“Kama mgombea mmoja anatumia mali za umma na mwingine analazimika kutumia rasilimali zake binafsi, basi Tume imeshindwa kusimamia usawa wa ushindani,” anasema.

Anasisitiza kuwa Tume inapaswa kuchukua hatua za haraka pale inapobaini matumizi ya mali za umma kwa maslahi ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Nelson Mazengo, hali hii inaathiri moja kwa moja imani ya wananchi kwa demokrasia.

“Wananchi wanaanza kuamini kwamba ili ufanikiwe kisiasa ni lazima uwe ndani ya chama tawala. Hii ni hatari kwa mustakabali wa demokrasia,” anaonya.

Anasema tabia ya kuteua viongozi wengi wa Serikali kutoka chama kimoja, au hata kuwahusisha wastaafu wa vyombo vya ulinzi katika siasa za chama, inaongeza dhana ya upendeleo wa kimfumo.

Kwa ujumla, mjadala wa mpaka kati ya mali za Serikali na maslahi ya vyama vya siasa nchini Tanzania unaonesha changamoto ya kimuundo, kisheria na kiutashi wa kisiasa, Wakati sheria zikieleza bayana juu ya marufuku ya matumizi ya mali za umma kisiasa, mazingira ya kihistoria na ya kikatiba yanaendelea kufanya mpaka huo kuwa mwembamba na mgumu kutekelezwa.

Kwa jamii ya kimataifa na wadau wa demokrasia, uzoefu wa Tanzania unaonesha umuhimu wa mageuzi ya kisheria, kuimarisha taasisi huru na kujenga utashi wa kisiasa ili kulinda misingi ya uchaguzi huru na wa haki, na kurejesha imani ya wananchi katika demokrasia.
 

Attachments

  • IMG_5626.jpeg
    IMG_5626.jpeg
    182.2 KB · Views: 28
Pamoja na haya yote ikiwepo tume huru ya uchaguzi hiko chama tawala kitapigwa tu kwa kura.
Kwa sasa dola hata haiwezi tena kuisadia CCM katika kuipatia ushawishi kwa raia, kilichobaki ni msaada wa mabavu ya mtutu wa bunduki tu.
 
Back
Top Bottom