Wakuu hii imekaaje aisee? Isije tukauma Watoto wa watu huko mtaani wakafia ghetto au kupata Stroke ile yenyewe sio stroke ya yale mambo?
- Tunachokijua
- ‘Love bites’ ambayo pia hujulikana kama hickey, ni alama nyekundu au zambarau kwenye ngozi inayosababishwa na kunyonya kwa nguvu katika sehemu ya ngozi kitendo ambacho hufanywa na wapenzi wawili wawapo faragha lengo likiwa ni kufurahia raha na msisimko unaotokana kitendo hicho. Shingo imekuwa ni moja ya sehemu ya kawaida kupata love bites kwa sababu ya urahisi wa kufikiwa, japokuwa mtu anaweza kuipata sehemu yoyote ya mwili.
Bila shaka unaweza kuwa mmoja kati ya watu ambao wamepata au kumsababishia mtu mwingine ‘love bite’ hasa maeneo ya shingoni, eneo ambalo watu wengi huogopa kupata alama hizo kutoka na aibu ya kujulika juu ya kitendo alichokifanya na hata kusababisha kutokea kwa alama zinazojulikana kama ‘love bites’
Wakati mpenzi wako ananyonya na kung'ata taratibu ngozi, shinikizo hilo linavunja mshipa midogo ya damu chini ya uso wa ngozi. Kukusanyika kwa damu katika eneo lililonyonywa hufanya doa kubwa na zito, ambapo hutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu.
Kumekuwapo na hoja juu ya madhara ya ‘love bites’ hasa katika eneo la shingo, ambapo inadaiwa kuwa upo uwezekano wa alama hizo wanazowekeana wapenzi baada ya kunyonyana kwa nguvu na kung’ata taratibu sehemu ya shingo kuwa zinaweza kusababisha kiharusi (stroke)
Kiharusi (stroke) ni ugonjwa unaoshambulia mishipa ya damu inayokwenda kwenye ubongo na ndani ya ubongo. Kiharusi hutokea wakati mshipa wa damu unaobeba oksijeni na virutubisho kwenda kwenye ubongo unapozuiwa na chembechembe ya damu au kutokana na kupasuka mishipa ya damu, Inapotokea sehemu ya ubongo kushindwa kupata damupamoja na hewa ya oksijeni, husababisha seli za ubongo kufa.
Je ni upi uhalisia juu ya ‘love bites’ kusababisha ugonjwa wa Kiharusi (stroke)?
Ufuatiliaji wa JamiiCheck uliopitia tafiti mbalimbali umebaini kuwa upo uwezekano wa love bite kusababisha Kiharusi ambapo Kupatwa na jeraha kwenye mshipa wa carotid shingoni unaosafirisha damu yenye oksijeni kutoka kwenye moyo kwenda kwenye ubongo kunaweza kusababisha chembechembe ya damu au kuhamasisha chembechembe iliyoganda ambayo inaweza kusafiri hadi mshipa mdogo wa damu kwenye ubongo, na kusababisha kiharusi.
Kwa mujibu wa Tovuti ya ABC News Mwaka 2010 katika hospitali ya Middlemore katika jiji la Aukland nchini New Zealand aliripotiwa mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 44 akiwa amepoozakatika mkono wa kushoto ambapo madaktari waligundua kuwa kulikuwa na chembechembe ya damu kwenye mshipa wa damu upande wa kulia wa shingo yake chini ya mahali ambapo bado aliendelea kuonyesha alama ya ‘love bite’
"Kwa sababu ilikuwa ‘love bite, kulikuwa na kunyonywa kwa nguvu. Kwa sababu ya jeraha la kimwili, lilisababisha mpasuko kidogo ndani ya mshipa wa damu uliopelekea chembechembe ya damu”
alisema Dkt. Teddy Wu, aliyemtibu mgonjwa, akizungumza na vyombo vya habari vya New Zealand. Chembechembe hiyo ya damu ilionekana kusababisha kiharusi.
Katika kisa kingine, tovuti ya maktaba ya taifa ya tiba ya nchini Marekani inatoa ripoti ya Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 35 ambaye alikumbwa na hali ya mwili kuwa dhaifu upande wa kulia kutokana na kiharusi cha mshipa mkubwa wa ubongo wa kati (left middle cerebral artery stroke) ikiwa ni masaa 12 baada ya kupata "love bite" upande wa kushoto wa shingo yake.
Uchunguzi ulionesha karibu ya kuziba kwa mshipa mkubwa wa shingo wa kushoto (left internal carotid artery ICA), na pia uchunguzi wa CT angiography ulionyesha kutokea kwa damu iliyoganda (thrombus) kwenye ukuta wa mshipa huo ambapo uharibifu katika ukuta wa mishipa hiyo unaweza kupunguza au kuzuia mtiririko wa damu. Hali hiyo ya kuganda au kutengeneza bonge la damu linaloundwa kwenye mshipa wa damu husaidia kuzuia kuvuja kwa damu unapoumia lakini pia inaweza kusababisha matatizo ikiwa inazuia mtiririko wa damu.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa “love bites” shingoni ni chanzo kisichokuwa cha kawaida cha kiharusi kinachohusisha mzunguko wa damu.