Influenza
JF-Expert Member
- Jul 1, 2018
- 1,509
- 3,756
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, Gilles Muroto amesema leo alfajiri walipokea taarifa kutoka kwa Mbunge wa Viti Maaalum, akiwa na Dereva wa Mbowe, Wilhad Urassa (34) kuwa Mwenyekiti huyo wa CHADEMA wakati akipandisha ngazi kuelekea ndani kwake inadaiwa alishambuliwa na watu 3
Kamanda Muroto amesema “Inadaiwa watu hao 3 waliokuwa wamevaa jackets (makoti) walimshambulia kwa kumkanyaga na kumpiga mateke hasa mguu wake wa kulia. Kutokana na taarifa hizo majeruhi alipelekwa katika Hospitali ya Ntyuka anakopatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.”
Ameeleza, “Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi bila kuacha chochote ili kupata ukweli na usahihi wa tukio hilo. Tukio hili lisitumike kisiasa au kwa njia yoyote ya kujiongezea umaarufu kwa mtu au watu na ni marufuku kuingilia uchunguzi huo.”
Amesisitiza kuwa eneo lile lina Walinzi na Majirani watafanya uchunguzi kujua ukweli wa tukio. Pia, amewaonya Wafuasi wa CHADEMA wanaohamasishana kukutana kwani Jeshi la Polisi lipo macho na yeyote anayefanya mikusanyiko isiyo halali atashungulikiwa kweli kweli
Aidha, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amesema Polisi wanapofanya Uchunguzi hawapaswi kufunga milango ya uchunguzi na kuliita hili ni tukio la kawaida kwasababu viashiria vinaonesha tukio hili lina muelekeo wa kisiasa
Mnyika amesema kati ya watu waliokuwa wanamshambulia Mbowe wapo waliosikika wakisema “Wewe unaisumbua sana Serikali, tunakushughulikia tuone kampeni utafanyaje.” Ametoa wito kwa Polisi na vyombo vya Usalama kuchunguza tukio hilo kwa mapana ili waliohusika wachukuliwe hatua
Amesema siku chache kabla ya Mbowe kushambuliwa, katika mitandao ya Kijamii kulisambaa video ya mtu anayejiita Mchungaji wa Kitaifa, Mchungaji Mashimo akisema “Kuna tukio litatokea mbele kwa Kiongozi wa Upinzani kushambuliwa” na kati ya majina aliyoyataja, jina Freeman Mbowe lilikuwepo. Ametoa wito kwa Polisi wamkamate ili aleeze hizo kauli zake.