MWIGULU NCHEMBA JEMBE LISILOVUNJIKA MPINI,MGOMBEA PEKEE ATAKAYE IVUSHA TANZANIA KIUCHUMI/MAENDELEO YA UHAKIKA.
"NITAWAVUSHA", "Mabadiliko ni Vitendo Wakati ni Sasa".- Ni maneno mazito yaliyosikika masikioni mwa Watanzania siku Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba alipotangaza rasmi nia ya kutaka kuteuliwa na chama chake Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisikika akipaza sauti na kusema "Nimetathmini vya kutosha, nimejiridhisha vya kutosha hivyo ahadi yangu kwa Watanzania nitawavusha … ninaomba mniamini na mniunge mkono kwani nitawavusha". Moja kati ya mambo aliyozungumza na kuwagusa wananchi ni pamoja na kuifanya nchi iwe katika kipato cha kati, kujenga taifa linalojitegemea pamoja na kuwajengea uwezo wananchi kumiliki uchumi wao, kukomesha rushwa sambamba na kuongeza ajira kwa vijana kwa kufufua viwanda vya zamani na kuanzisha viwanda vipya.
Baadhi ya wananchi walisikika wakipaza sauti zao huku wengine wakisema "tunaimani nawe Mwigulu" wakionesha kuridhishwa na utendaji kazi wake sambamba na hotuba aliyoitoa siku hiyo ya kutangaza nia katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.
Mmoja wa wananchi waliopata nafasi ya kufika ukumbini hapo alisema ni wazi kuwa Mwigulu ndio chaguo jema kwa sasa kwani ana mambo mengi yanayombeba hasa ukizingatia hajawahi kukutwa na kashfa yoyote wala kukiuka maadili ndani ya chama chake.
Imani waliyoonesha wananchi hao kwa kijana machachari anayekubalika na wengi ambae amepata nafasi mbalimbali tena za juu ndani ya chama chake (CCM) zikiwemo Unaibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi pamoja na kuwa Naibu Waziri wa Fedha, hii ni kutokana na jitihada zake za kuwatetea wanyonge pamoja na kusimamia na kutekeleza ilani ya chama chake kikamilifu.
Wananchi wengi wamekuwa wakilalama ni kiongozi gani ambaye ataweza kusimama na kukomesha rushwa, ndipo Mwigulu alipojipambanua na kukemea vikali rushwa hata katika Sakata la Escrow lililosababishia serikali kukosa kodi kutoka katika bilioni 303 zilizochotwa kinyemela katika akaunti hiyo kijana huyu alitumia uwezo na nguvu zake kupingana na rushwa.
Nchemba hakuonesha unafiki kwa kumwonea mtu aibu hata kama ni wa chama chake (CCM), bali alisimamia ukweli katika jambo hilo na kuhakikisha haki inatendeka bila kumwonea au kumpendelea mtu yoyote mradi haki itendeke na kila mmoja aadhibiwe kwa makosa yake.
Alipotangaza nia akanukuliwa akisema "I will have zero tolerance on corruption" (sitavumilia rushwa) , haiwezekani rasilimali za taifa ziwanufaishe wachache wakati hospitali hazina madawa na shule zipo katika hali mbaya".
Kauli hiyo iliyotolewa na wananchi (tunaimani nawe) imezidi kupata mashiko baada ya kuona jinsi kiongozi huyu anavyoichukia rushwa na kusema waziwazi hatakuwa na uvumilivu hata kidogo na watu wanaotoa ama kupokea rushwa.
Akaongeza kuwa sheria iliyopo dhidi ya rushwa akiingia madarakani ataibadilisha mara moja ili kupambana kikamilifu na rushwa na ikibainika hakuna swalia mtume adhabu itakayotolewa ni kifungo kwani hakuna sababu ya wachache kunufaika kwa njia zisizo sahihi huku walio wengi wakiendelea kutaabika.
Alipokuwa akihutubia wananchi waliofurika ukumbini hapo kumsikiliza, Mwigulu alikuwa akiainisha na kufafanua agenda zake kwa umakini pasipo kusoma maelezo kwenye makabrasha tofauti na viongozi wengine waliotangaza nia wakitumia muda mwingi kutoa maelezo yaliyomo kwenye makaratasi, hii ikionesha umakini wa aina yake na namna alivyojipanga kuwatumikia Watanzania.
Nakumbuka kiongozi huyu alijinasibu akisema anafahamu vyema ajenda za Watanzania ndio maana ana dhamira ya dhati ya kuwavusha kutoka hapo walipo na kuwafikisha sehemu nzuri kwa kuwawezesha kumiliki uchumi wao.
Pasipo kupepesa macho wala kutikisa masikio Mwiguli alisema urais hauna uzoefu na kiongozi hapimwi kwa alichotenda hapo awali bali kwa anachoweza kufanya kwa wakati huu hivyo umri pamoja na uzoefu sio hoja za msingi na hazina mashiko.
Ni dhahiri kiongozi huyu anakubalika na makundi yoye yaani vijana, wazee na hata watoto kutokana na kuisimamia kikamilifu serikali na kuwa na shauku kubwa ya kuleta maendeleo kwa kasi katika taifa la Tanzania.
Chanzo: