Magufuli na daraja la Kigamboni, tushangilie?: Na M.M. Mwanakijiji
Nina uhakika katika siku za usoni Dar es Salaam watu watakuwa wanakuja kuangalia madaraja na mabarabara badala ya kuja kuangalia msongamano Dk. John Magufuli (wakati wa kusaini mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigamboni).
Siku ya Jumatatu kile kinachoitwa ndoto ya daraja la Kigamboni kilioneshwa kuwa kitaanza kutimia baada ya makubaliano ya ujenzi wa daraja hilo ambayo yatashirikisha serikali ya Tanzania, Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Kampuni ya China kutiwa saini. Watu wengi ambao labda kutokana na kutokujua historia au kutokutaka kujua historia wameonekana kushabikia kwa furaha hatua hii ya sasa kana kwamba ni zawadi na neema ya Mungu kwa Watanzania.
Dk. Magufuli, Waziri wa Ujenzi akizungumza katika hafla ya kutia sahihi makubaliano hayo alizungumza na kujaribu kushawishi watu waamini kuwa hatua hii imefikiwa baada ya uongozi mzuri wa Rais Jakaya Kikwete na hivyo wananchi waunge mkono na inaonekana wafanye hivyo bila kuuliza maswali!
Daraja la Kigamboni si zao la fikra za Kikwete
Katika kitu cha kushangaza kabisa ni kuwa Jina la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere halikutukuzwa katika hafla hiyo. Ni katika kile ambacho nimekiita kuanzia mwaka jana kuwa ni juhudi dhaifu za kulifuta jina la Nyerere katika mchango wa maendeleo. Katikati ya miaka 1970 ni uongozi wa Mwalimu Nyerere uliofanya upembuzi yakinifu wa kina wa ujenzi wa daraja la Kigamboni.
Wazo la ujenzi wa daraja hili haukutokana na serikali ya awamu ya nne kama Magufuli anavyotaka watu waamini! Ni wazo ambalo lilikamilika na kufanyiwa utafiti miaka karibu arobaini iliyopita.
Ubunifu wa michoro ya daraja ilikuwa imekamilika mwaka 1977 miezi michache kabla ya nchi kwenda vitani na kabla ya ukame uliofuatia mapema miaka ya 1980. Kwa wanaokumbuka watahusisha kuwa ni utawala huo huo wa Nyerere uliofikiria na kufanyia upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Stielgers Gorge ambalo lingeweza kuzalisha umeme wa zaidi ya MW 2000 na kuliondoa taifa katika tatizo la umeme. Gharama ya ujenzi wa Stielgers wakati ule ilikuwa kama dola bilioni 1.2 wakati ujenzi wa Kigamboni kwa fedha za wakati ule na kwa michoro iliyotolewa wakati ule ilikuwa ni kama dola milioni 28.6.
Kwa hiyo, tuweke rekodi kwa usahihi kwanza huwezi kutenganisha mpango wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni au baadaye Stielgers George na mawazo ya Rais wetu wa Kwanza Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Najua wengine watachukia, wengine watakereka lakini ukweli ni kuwa hawakuja na mawazo mapya! Hata hilo daraja la Mkapa si wazo la Mkapa!
Gharama ya ujenzi haijabadilika sana
Kama kweli na sina shaka ni kweli kwamba wazo la ujenzi wa daraja la Kigamboni ni wazo la miaka karibu arobaini iliyopita basi leo hii kusainiwa kwa mkataba huu kumekuja kukiwa kumechelewa sana. Ni wazi kuwa mazingira ya mebadilika na hivyo upembuzi yakinifu mpya ulihitajika.
Sasa hivi katika mpango wa sasa daraja litakuwa na njia sita (si mbili kama ilivyopendekezwa zamani) na urefu wake ukiongezwa kwa karibu mita mia moja zaidi na ikitumia bila ya shaka teknolojia na utaalamu ambao haukuwepo miaka arobaini iliyopita (japo kanuni za fizikia na uhandisi nyingi ni zile zile).
Leo hii tunaambiwa gharama ya ujenzi wa daraja hii inakadiriwa kuwa kati ya dola milioni 130-200. Tukichukulia fedha za mradi wa wakati wa Nyerere za dola milioni 28.6 na kuzileta kwenye fedha za leo ni sawasawa na dola milioni 107.7 Hivyo ni wazi kuwa kiasi hicho cha fedha kinachopendekezwa leo hii si kibaya sana ukizingatia ukubwa na teknolojia ambayo itatumika.
Mojawapo ya tafiti nyingine za Benki ya Dunia za miaka ya karibuni zaidi zilionesha kuwa daraja la Kigamboni lingegharimu karibu dola milioni 46 hivi (karibu sawa na kiasi kilichokombwa na Kagoda Agriculture katika kashfa ya EPA!) Lilichelewa kwa sababu ya umaskini au kukosekana uwezo?
Naomba nipendekeze kwa wasomaji wangu kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa daraja la Kigamboni hakukutokana na ukosefu wa fedha au uwezo wa kitaalamu hasa katika miaka hii kumi na tano hivi. Wakati mradi huu umebuniwa miaka ya sabini nchi ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi. Hata hivyo, baada ya mafanikio ya kampeni ya kusamehewa madeni yasiyolipika ambayo pia iliongozwa na Mwalimu Nyerere kabla ya kifo chake mwaka 1999 Tanzania ilikuwa katika nafasi ya kutumia neema hiyo kujenga miundombinu yake.
Kwa baadhi yetu tulitegemea kuwa mradi wa Kigamboni na ule wa Stielgers ingekuwa ni miradi mikubwa ya kwanza kufanyika. Wa Kigamboni ungeweza kutekelezwa mapema zaidi kwa sababu hauna gharama kubwa zaidi na ni rahisi zaidi kutekelezeka. Lakini haikuwa hivyo. Kilichotokea ni kuwa ni miaka hii kumi iliyopita tumeshuhudia ufisadi wa hali ya juu katika taasisi mbalimbali za serikali huku miradi ambayo ilikadiriwa kidogo ikila mabilioni ya fedha na watumishi wa umma wakiendelea kunufaika kwa migongo ya maskini wa taifa letu.
Ndani ya miaka hii kumi (ya 2000 hadi 2010) Tanzania imepoteza kwa njia ya ufisadi zaidi ya dola bilioni 10 (zaidi ya shilingi trilioni 11) huku Rais Kikwete akitudokeza kuwa karibu asilimia 30 ya fedha za bajeti ya taifa huishia mikononi mwa mafisadi.
Ndugu zangu, kuchelewa kwa ujenzi wa miradi hii mikubwa ambayo ingeweza kubadilisha maisha ya watu wetu ni matokeo ya moja kwa moja ya ufisadi uliokubuhu. Kiasi kilichopotezwa kwa ufisadi katika sekta mbalimbali kingeweza kujenga daraja la Kigamboni, Stielgers na miradi mingine mikubwa bila kuwaomba NSSF au taasisi binafsi!
Leo Magufuli anataka tushangilie kuwa NSSF wamefanya kazi nzuri ya kutoa fedha za wanachama wao kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni wakati serikali yake imekuwa dhaifu kukabiliana na ufisadi mkubwa na kuwaacha mafisadi waendelee kupeta?
NSSF na kuficha madhara ya ufisadi
Hili sitaki kuliandika sana kwa sababu watu wanaofuatilia wanaweza kuona mtindo mmoja ukijitokeza miaka ya karibuni. Pale ambapo serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza na kusimamia fedha za umma kutekeleza miradi mbalimbali inakimbilia fedha za wanachama wa mashirika ya hifadhi ya jamii. Tumeliona hili kwenye kashfa ya Kiwira ambapo serikali iliruhusu ufisadi wa hali ya juu ya mmoja wa waliowahi kuwa viongozi wake lakini badala yake NSSF ikataka iwekeze bilioni 400 za fedha za wanachama; tumeona pia kwenye barabara ambazo Waziri Magufuli na serikali yake wamepata shida kuzisimamia na fedha za walipa kodi wakikaribisha NSSF kuingia na kuwekeza huko; tumeshuhudia hili kwenye ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma vile vile ambapo NSSF na PPF wamewekeza fedha za wanachama wao katika miradi hiyo.
Leo hii NSSF inakaribishwa tena kwenye daraja la Kigamboni na iko tayari kubeba gharama ya karibu asilimia 60 ya ujenzi na baadaye uendeshaji wa daraja hilo kurudisha fedha zake.
Sasa kinadharia hili halina tatizo hata kidogo. Pote duniani mashirika mbalimbali ya umma na hata ya hifadhi ya jamii yamewekeza kwenye miundo mbinu. Lakini kuna tofauti moja inapokuja Tanzania. Wanasiasa wanapoingiliana sana na watendaji wa taasisi hizi maamuzi ya baadhi ya taasisi hizi yanakuwa ni ya kisiasa zaidi. NSSF imekuwa ni shirika ambalo liko karibu zaidi na wanasiasa wa CCM kiasi kwamba nikiliita kuwa ni shirika la uwekezaji la CCM sitakuwa nawaita jina baya. Liko kwa ajili ya kuficha udhaifu wa uongozi, maono na usimamizi wa fedha za umma wa serikali ya CCM.
Popote pale penye mradi mkubwa ambao Serikali imeshindwa kuutekeleza kwa sababu haina fedha a.k.a fedha zimeliwa na mafisadi NSSF itajitokeza kwa moyo mkunjufu kugawa fedha za wanachama kwenye miradi hiyo!
Wakati umefika kwa wanachama wa NSSF na mashirika mengine ya umma ambayo yanaingiza fedha kwenye miradi mikubwa ya serikali kuanza kudai mafao kutoka miradi hiyo. Hivi, mwana NSSF, PPF, au shirika jingine la hifadhi ya jamii anapata faida gani ya kifedha kwa shirika lake kuwekeza kwenye miradi mkubwa hii? Katika makampuni ya kawaida ya kibiashara kampuni inapowekeza kwenye miradi na kupata faida inagawa baadhi ya faida hizo moja kwa moja kwa wanahisa wake.
Je, mashirika yetu haya yanavyowekeza fedha hizi zote yanawagawia kiasi gani cha faida wanachama ambao fedha zao zinaingizwa huko? Mtu anayepata mafao ya shilingi elfu themanini kwa mwezi baada ya kustaafu anafaidika vipi na shirika kuwekeza mabilioni kwenye mafuta, barabara na madaraja au kuzalisha umeme? Je, wanachama wanaweza kudai kuwa asilimia kama 10 hivi kila mwaka ya faida yote ambayo NSSF inapata katika uwekezaji irudishwe kama gawio kwa wanachama wake? Au faida wataambiwa ni kuwa na wao watatumia madaraja na barabara hizo!
Nimeshawahi kusema huko nyuma kuwa mashirika ya umma kama NSSF ambayo yanawekeza mabilioni ya fedha za wanachama kwenye miradi hii mikubwa ambayo ni rahisi kuyumbushiwa na hali mbaya ya uchumi au matatizo mengine (fikiria daraja jipya likijengwa halafu likabomolewa na tsunami au tetemeko la ardhi!) yanahitaji kuwekewa utaratibu mkali sana wa uwekezaji. Hayapaswi kuachiliwa kuwekeza kana kwamba yao ni mashirika binafsi yenye lengo la faida tu!
Magufuli bila kupiga vita ufisadi anatuaminisha uongo. Mojawapo na ninaweza kusema kwangu ni tatizo kubwa la Magufuli ni kuwa haamini kabisa kuwa ufisadi ndilo tatizo kubwa kabisa linalokabili taifa sasa hivi na kuwa mambo mengi anayoyapigia kelele (kutofuatwa sheria kwa mfano) ni zao la ufisadi huo.
Magufuli anaamini kabisa kuwa serikali yake ni safi, uongozi wake ni bora zaidi na kuwa chama chake ni safi kabisa! Amefumba macho kabisa kama mbuni hasikii wala haambiwi kuhusu ufisadi.
Matokeo yake ni kuwa anajikuta anarudia vitu vile vile. Mara afute mkandarasi, mara aagize Kajima warudie barabara, mara apigie kelele watu wabomolewe nyumba.
Anafikiri kwa makosa watu hawajui sheria. Bila kupambana na ufisadi na mazao ya ufisadi haijalishi ni mradi gani ataupigia debe kwa kutumia takwimu zote alizonazo na hata maneno ya vijembe vya kisiasa hawezi kabisa kusimama kama kiongozi kati ya wananchi.
Watanzania wanahitaji kiongozi ambaye anafahamu na anapambana na ufisadi. Bahati mbaya sana yeye mwenyewe ni mmoja watu wambao walihusishwa na ufisadi mkubwa wa uuzaji wa nyumba za serikali miaka kadhaa iliyopita. Hadi leo hajaomba radhi taifa kwa kuruhusu jambo hilo ambalo lilisababisha gharama kubwa kwa serikali kwani pale ambapo ilikuwa rahisi kwa kiongozi kuhamia kwenye mji na kukuta nyumba ya serikali palipogeuka kuwa serikali ianze kuhudumia watumishi wake kwenye mahoteli!
Ninaogopa uongozi huu wa aina ya Magufuli. Sihoji dhamira yake hata kidogo ya kupenda au kutaka mabadiliko au kuona jiji la Dar watu wanaishi kwa starehe. Ninahoji kama anachosema kinawezekana bila kuwa shujaa wa kupambana na ufisadi.
Hadi leo hatujamsikia yuko upande gani kwenye kashfa za EPA, Meremeta, Kagoda, Mwananchi Gold, Richmond na Dowans! Sijui yuko upande gani kwenye kashfa ya ununuzi wa ndege ya Airbus 320 ambao wengine tuliipigia kelele miaka minne iliyopita. Magufuli yuko salama kwenye kiti chake cha enzi akiwa waziri lakini anapenda usalama tu wa ofisi yake. Hapendi kuudhi watu kwa kuchukua msimamo wa uthubutu. Binafsi sijali sana kama anasimamia barabara, daraja au jengo fulani kwani hayo yote yanaweza kufanywa hata na mafisadi na ukweli kuwa baadhi ya mafisadi waliokubuhu nchi hii ndio wasimamizi wenyewe wa miradi!
Binafsi nasubiri kwa hamu kumuona akichukua upande wa kupinga ufisadi katika serikali yake na siyo tu katika wizara yake. Nasubiri kumsikia akizungumzia ufisadi kama tishio la wazi la maisha na hali za wananchi wetu. Jiji la Dar-es-Salaam liko kama lilivyo si kwa sababu watu hawataki kufanya kazi bali kwa sababu hizo ajira zenyewe nyingi zimefungamana na ufisadi. Mtu asiyepiga magoti na kutoa sadaka kwenye madhabahu ya ufisadi habarikiwi!
Mtu akitaka kufanikiwa ni lazima aende kufanya hija kwa fisadi kiongozi au kuwadi wa ufisadi ili mambo yake yaende vizuri! Magufuli hatambui hilo anataka tuamini kuwa tatizo ni wananchi!
Nilikua ninaamini kuwa anaweza kuwa kiongozi mzuri lakini nimegundua kuwa bila ya madaraka Magufuli ni sifuli. Hana la kufanya, hana la kushawishi, na hawezi kusimamia kitu bila kuwa na madaraka. Ila anataka kuogopwa si kwa sababu anaweza kushawishi bali kwa sababu ana uwezo wa madaraka kufanya anayofanya. Binafsi nampa changamoto kuwa atoke kwenye kiti chake cha starehe na kusimama kupambana na ufisadi ambao Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliita ni adui mkubwa wa nchi wakati wa amani kuliko vita!
Kiongozi asiyetembua ukweli huo na asiyesimama kusimama na adui huyo mkubwa wa uhuru na utu wa Mtanzania haijalishi anatembea kwa miondoko gani au anafanya nini cha kusifiwa ni wa kuangaliwa kwa kuogopa. Mara zote uongozi ni uwezo wa kushawishi na siyo uwezo wa kutishia watu. Ni madikteta tu ambao wanaweza kuleta maendeleo kwa kulazimisha siyo kwa kushawishi. Matokeo yake ni kuwa maendeleo hayo ni ya picha!
Tanzania kuwa kama Nigeria
Tukikubali hili la kutukuza vitu na siyo utu na kuweka mkazo katika kupendezesha majengo badala ya utu wa mtu tunakubali kufuata njia ya Nigeria au nchi nyingine ambazo zina vitu vizuri lakini hazina utu. Jamani Nigeria ina mabarabara na madaraja ya kila aina. Daraja refu zaidi katika Bara la Afrika ni lile la Third Mainland Bridge ambalo lina urefu wa kilomita 11.8. Nigeria inayo mabarabara ya juu kwa juu (flyovers) na kwa hakika ina barabara nyingi tu za kisasa kulinganisha na Tanzania.
Lakini, Nigeria imejua amani na utulivu? Je Nigeria wana umoja zaidi?Je, Nigeria ufisadi umedhibitiwa? Je, Nigeria ingeweza kutulia na kushinda ufisadi leo hii ingekuwa wapi?
Ninachokiona ndicho ambacho Tanzania inakitaka na ndio maana maneno yaliyoniudhi ya Bw. Magufuli ni hayo ya kuonekana kutaka kujenga majengo ya kisasa ili watu waje kuyaona! Hatuhitaji daraja la kisasa ili watu waje kulishuhudia! Vinginevyo, tutajenga madaraja, tutajenga mabarabara na mabarabara ya juu kwa juu lakini watu wetu wataendelea kuwa maskini, utu wao ukidhalilika na wao wakiwa watumwa wa matajiri wachache ambao watapita kwenye mabarabara hayo huko mamilioni ya Watanzania wakijivunia picha za kwenye post cards - si mnakumbuka watu hupiga picha kwenye lile daraja la wenda kwa miguu la Manzese?
Ndugu zangu, tusikubali kuwa kama Nigeria. Tusikubali kujenga vitu kwa ajili ya sisi nasi kusema tunavyo. Kabla hatujajenga hayo mabaraba ya kwenda mbinguni (nina uhakika wapo watakaoenda mbinguni kupitia barabara hizo) tuboreshe kwanza na kwa kiwango cha juu hivi vidogo vilivyotushinda hadi sasa.
Jamani, kama NSSF wanazo fedha hizo bwelele kwanini wasijenge mitaro ya maji machafu na maji ya mvua ili watu wa Dar waishi kwa heshima na siyo kutegemea huruma ya wingi wa mvua? Kama serikali ina mipango ya kuboresha jiji la Dar kweli kwanini tumeshindwa kujenga barabara nzuri za kawaida kwenye maeneo ya watu, kuwahakikishia umeme na maji safi huku viwanja na bustani za mapumziko zikiwepo karibu kila kwenye halmashauri!?
Ndugu zangu, tunaweza kushangilia hotuba, tunaweza kushangilia picha (nina uhakika kuna watu walikuwa wanasisimka wakiangalia picha za hilo daraja). Lakini ukweli tunapaswa kufunguliwa na kutaka kushangilia tunapoona maisha yetu yanaboreshwa zaidi na utu wetu unainuliwa zaidi.
Kama watu hawana mahali bora pa kuishi, kula au mavazi barabara za mbinguni zitawasaidia nini? Daraja la Kigamboni haliwahusu maskini wanaoishi Kigamboni linahusu matajiri wanaoishi Kigamboni! Kwa sababu maskini bado watalipa fedha kutumia daladala kuvuka; matajiri wataweza tu sasa kwenda kwa raha zao kwenye viwanja vyao na nyumba zao huko!
Siamini mpaka nione
Binafsi naomba mniruhusu niwe Tomaso! Siamini mpaka nione. Siamini kama gharama itakuwa ni hiyo bilioni kama 200 hivi hasa nikikumbuka mradi mwingine wa hii serikali waujenzi wa maghorofa pacha ya Benki Kuu.
Binafsi siamini kuwa hata daraja likijengwa litadumu kwani kama mfano wa ujenzi wa miundo mbinu mingi ukiangaliwa tunajua ni nini kinatokea mara wakishamaliza kukata utepe na kutoa hotuba za kupongezana.
Uharibifu huanza. Jamani, si tumeona kwenye daraja la Mkapa? Hili daraja likikamilika na baada ya kula fedha nyingi tusije kuja kuambiwa kuwa daraja linafungwa kwa matengenezo makubwa. Si tumeona kwenye barabara hizi hizi za Magufuli! Nitatoa pongezi zangu za kwanza inshallah ujenzi wadaraja utakapoanza! Hatushangilii picha, hatupongezi maneno au kutukuza takwimu! Tunapongeza ubora ndugu zangu, tunapongeza ubora! Magufuli hajanishawishi hadi hivi sasa ni sifuli.
Chanzo: Mtanzania Daima:
Magufuli na daraja la Kigamboni, tushangilie?