Mimi naamini mtu mwenye hela ana kitu ambacho mtu asiye na hela bado hajakipata. Unaweza kuwa na elimu kubwa, vyeti, IQ kubwa na kuzungumza mambo ya maana, lakini kama huwezi kutumia akili yako kutatua matatizo na kujenga maisha bora, kuna sehemu unahitaji kujitathmini.
Pesa zinahitaji maamuzi, nidhamu, kutambua fursa, kuvumilia changamoto na kujua namna ya kutumia rasilimali ulizonazo.
Ndiyo maana kwangu, mafanikio ya kifedha ni moja ya viashiria vya uwezo wa mtu kufikiri na kutenda kwa matokeo.
Najua mtasema kuna matajiri waliozaliwa kwenye familia zenye pesa, wengine walirithi, na kuna watu wenye akili kubwa lakini hawana fursa. Nakubali, mazingira yana nafasi yake.
Lakini swali langu ni hili: Kama una akili, lakini kwa miaka mingi huwezi kuitumia kuboresha hali yako ya kifedha, je, hiyo akili inakusaidia nini kwenye maisha halisi?
Tujadiliane bila kuogopana! 🔥
Mkuu,
Inawezekana kuna mara nyingi tu mtu mwenye hela ana akili. Kuipata hela ni vigumu, kukaa nayo ni vigumu zaidi, kuiwekeza izidi ni vigumu zaidi.
Kwa hiyo, hoja yako ina msingi fulani hivi wa ukweli.
Lakini, ni muhimu kuwa na kitu Waingereza wanakiita nuance.
Bila ya kuathiri uzuri na umuhimu wa hoja yako ya msingi, kwamba mara nyingi mtu kuwa na pesa inaonesha kuwa na akili, kuna namna nyingi ambazo pesa inaweza kuwapo hata bila ya mtu kuwa na akili , au, mtu mwenye akiki akakosa pesa.
1. Mtu A ambaye hana akili sana anaweza kupata bahati ya kuzaliwa katika nchi tajiri, na wazazi tajiri, wakati wa utajiri, akapata mifumo yote ya kumsaidia kuwa na pesa, bila ya kuwa na akili kubwa sana, akawa na pesa kuliko mtu B ambaye ana akili kumshinda mtu A, lakini hakuwa na bahati ya kuzaliwa nchi tajiri, au kuzaliwa na wazazi matajiri. Mwishowe ikawa mtu B ambaye ana akili sana kumshinda mtu A akawa masikini na mtu A ambaye hana akili kama mtu B, akawa tajiri.
Wewe unafikiri wale mabikionea wote wa Kinarekani wana akiki kuliko Waafrika wote ambao si mabilionea?
Kuna watu hawana pesa kwa sababu wamezaliwa katika famikia masikini, kwenye nchi masikini zisizo na mifumo mizuri tu.
2. Utajiri wa pesa pia unaendana na mambo mengi. Kuna watu hawana nia ya kuwa matajiri wa pesa. Kuna ma engineer wamegundua vitu muhimu sana kuanzia the original web browser na vingine vingi. Wakaamua kuvigawa bure watu wafaidike, badala ya kuviuza.
Kwao hawa, utajiri wa kazi zao kuibadilisha dunia ni muhimu zaidi kulijo utajiri wa wao kupata pesa.
3. Kuna watu wanapata pesa kwa uhalifu, wizi, udanganyifu, kuuza madawa ya kulevya, kuuza watu, kuuza silaha zinazoangamiza watu. Hawa unaweza kuwaona wana akili kwa sababu wana pesa, lakini pesa zao zinatokana na kuvunja maadili, na kuna watu wengine wengi ambao wangeweza kupata pesa kwa njia hizo, kuwazidi wao, lakini wamekataa kupata pesa kwa njia zisizofuata maadili.