Kuna mtazamo usio sahihi kuwa Wakatoliki tunamuabudu Bikira Maria au tunamweka yeye badala ya Mungu na Yesu Kristo. Ukweli ni kwamba, Wakatoliki hawamuabudu Bikira Maria; tunamwomba atuombee (maombezi) kwa Mwanae, Yesu Kristo, ambaye ndiye Mwombezi na Mwokozi wetu pekee.
Hatusemi Maria ana mamlaka ya kusamehe dhambi, bali tunajua sala zake zina nguvu kubwa mbele ya Mungu.
Hapa kuna misingi mikuu ya Kibiblia na Kitheolojia inayofafanua jambo hili:
1. Maombezi ya Watakatifu: Kama mchungaji anaweza kukuombea, iweje Mtakatifu ashindwe?Katika Ukristo, sote tunajua umuhimu wa kuombeana. Tukipatwa na shida, tunakwenda kwa Wachungaji, Mapadri, au marafiki wa imani na kuwaambia, "Ndugu yangu niombee." Mtume Paulo anasisitiza hili akisema: “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote” (1 Timotheo 2:1). Kama mtu aliye hai duniani mwenye mapungufu anaweza kukuombea na Mungu akasikia, iweje mtakatifu aliyeko mbinguni, aliyetakasika kabisa na aliye karibu na Mungu, ashindwe kukuombea? (Waebrania 12:23). Watakatifu hawajafa; wako hai kiroho mbinguni na sala zao zinaelezwa katika Ufunuo 5:8 kama “vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni sala za watakatifu.”
2. Salamu Maria: Salamu ya Malaika na ElizabethMalaika Gabrieli alipotumwa na Mungu, alimpa Maria salamu ya upekee ambayo haijawahi kutolewa kwa mwanadamu mwingine yeyote:“Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyejaa neema, Bwana yu pamoja nawe.” (Luka 1:28)Muda mfupi baadaye, Elizabeth akijazwa na Roho Mtakatifu alithibitisha ukubwa wa Maria kwa kupiga kelele:“Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Imekuwaje mimi hata mama wa Bwana wangu anitembelee?” (Luka 1:42-43)Wakatoliki tunaporudia maneno haya kwenye sala ya Rozari, tunakariri maneno yaliyotamkwa na Mungu kupitia Malaika na Roho Mtakatifu.Hivyo kusali Rozari ni jukumu la mkristo yoyote maana ni maneno yaliyoko kwenye Biblia
3. Harusi ya Kana ya Galilaya: Nguvu ya Maombezi ya MariaKatika Yohana 2:1-11, kwenye harusi ya Kana, divai ilipoisha, watu hawakumfuata Yesu moja kwa moja—walimfuata Maria. Maria, kwa kujua shida yao, alimgeukia Yesu akisema, “Hawana divai.” (Yohana 2:3). Ingawa Yesu alisema saa yake ilikuwa haijafika, kwa sababu tu ya heshima ya maombi ya Mama yake, alifanya muujiza wake wa kwanza. Hii inadhihirisha wazi kwamba Maria ni mwombezi wa karibu sana ambaye Yesu hapingani na ombi lake la huruma kwa ajili ya wanadamu.
4. Yesu Msalabani: Maria Amekabidhiwa Kuwa Mama wa Waamini WoteYesu alipokuwa akifa msalabani, alituachia Bikira Maria kuwa Mama wa kiroho wa Kanisa zima. Kwenye Yohana 19:26-27, Yesu alimwona mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda (Yohana, anayewakilisha waamini wote), akamwambia mama yake: “Mama, tazama, mwanao! Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako! Tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.” Tunapomwomba Maria, tunatimiza agizo la Yesu la kumchukua Maria kama Mama yetu wa kiroho aliyetupatia msalabani.
5. Kukingiwa Dhambi ya Asili: Maria ni 'Eva Mpya' katika UkomboziIli Mungu asimame katikati ya wanadamu, ilikuwa lazima "Sanduku la Agano Jipya" (tumbo la Maria) liwe safi kabisa, bila waa lolote la dhambi. Ndiyo maana Kanisa Katoliki linafundisha Dogma ya Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili (Immaculate Conception).Eva wa Kwanza: Alikuwa bikira safi, lakini kwa kutokutii kwake, alileta anguko na dhambi duniani.Maria (Eva Mpya): Kupitia utii wake mkuu aliposema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” (Luka 1:38), alileta Ukombozi duniani kwa kumzaa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Maria ana nafasi ya kipekee na ya lazima katika mpango wa ukombozi wa mwanadamu.
6. Tofauti ya Heshima ya Kikatoliki na Ibada za Kiasili (Mizimu)Kuna makabila au tamaduni zinazoheshimu mizimu na kuabudu mababu zao kwa namna inayochanganya ibada na Mungu. Kanisa Katoliki halifanyi hivyo. Kanisa lina weledi mkubwa wa theolojia:Hatutambui mababu kwa sababu tu ya 'ukabila' au ushirikina.Sisi tunawaenzi watakatifu walioishi maisha ya kishujaa ya Kikristo yaliyothibitishwa. Ni heshima kwa kile kilicho bora, safi, na cha hakika kiimani. Hatutoi kafara au tambiko, bali tunatoa sala kwa Mungu kupitia maombezi yao.
7. Ushahidi wa Kihistoria: Matukio ya Kutokea kwa Bikira Maria.Mungu amekuwa akithibitisha nafasi ya Maria kupitia miujiza na matokeo makubwa duniani ambayo yamefanyiwa utafiti mkubwa wa kisayansi na kitatibu, na Kanisa kuyathibitisha: yakiwemoFatima (Ureno, 1917): Bikira Maria aliwatokea watoto watatu wa kichungaji (Lusia, Francisco, na Jacinta). Tukio hili lilihitimishwa na “Muujiza wa Jua” mbele ya umati wa watu zaidi ya 70,000 (pamoja na waandishi wa habari wasioamini) walioshuhudia jua likicheza na kushuka angani. Lourdes (Ufaransa, 1858): Alimtokea binti Bernadeta Soubirous na kujitambulisha akisema, "Mimi ndimi Kukingiwa Dhambi Asili". Pale Lourdes, chemchemi ya maji ya muujiza ilitokea, na hadi leo mamilioni ya wagonjwa wanapona maradhi yasiyoponyeka kitiba wanapokunywa au kuoga maji yale kwa imani.Hitimisho:Kumwomba Bikira Maria hakupunguzi uwezo wa Yesu Kristo wala Mungu Baba. Badala yake, kunatupa mshirika wa karibu sana mbinguni, Mama wa Mwokozi wetu anayepeleka sala zetu mbele ya Kiti cha Enzi cha Neema. Kama tunavyoomba sala za watu wa duniani, tunajivunia zaidi kuomba sala za Mama wa Mungu.Tumsifu Yesu Kristu!