Takribani mwezi mzima sasa, maeneo mengi ya Dar es Salaam na Pwani, yamekumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi. Kibaha - Pwani Mitaa mingi haina huduma hiyo kwa miezi kadhaa, Wananchi wanauziwa maji kwenye tenki kuanzia Sh 20,000, 25,000 hadi 30,000 kwa tenki moja la Lita 1,000.
Tatizo hili, mbali na kuwa kero kwa Wananchi, linaibua maswali mengi kuhusu uwajibikaji wa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu, hususan DAWASA pamoja na wadau wengine katika sekta ya maji.
Wakati maeneo kadhaa ya jiji yakikosa maji kwa siku nyingi, hakukuwa na taarifa za mapema kutoka mamlaka hizo ambazo zingewezesha Wananchi kujiandaa dhidi ya changamoto hiyo.
Ni baada ya malalamiko kuongezeka ndipo DAWASA ilitoa taarifa ikieleza kuwepo kwa upungufu mkubwa wa maji katika chanzo kikuu cha Ruvu. Hapo ndipo tukaona pia ziara za Waziri wa Maji maeneo mbalimbali ya jiji, akitoa ufafanuzi kuwa uzalishaji wa maji kutoka Ruvu umepungua kwa zaidi ya asilimia 50, hali iliyoleta msukosuko huu.
Swali muhimu la kujiuliza ni: Kwa nini mamlaka hazikutoa taarifa mapema ili kuwawezesha wananchi kujiandaa na changamoto hii? Zaidi ya hapo, karibu kila mwaka Dar es Salaam na Mikoa ya Pwani kwa jumla hukumbana na tatizo la upatikanaji wa maji na mara nyingi maelezo yanayotolewa yanahusishwa na upungufu wa mvua unaoathiri Mto Ruvu. Je, ni kweli hadi sasa hatujapata mbadala au mikakati madhubuti ya kuzuia tatizo hili kujirudia?
Cha kushangaza ni kwamba viongozi na wadau mbalimbali wamekuwa wakizungumzia mara kwa mara athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kupungua au kuongezeka kwa mvua, kuongezeka kwa joto, na athari nyingine. Iwapo tunatambua changamoto hizi mapema, kwa nini basi tunachelewa kufanya uwekezaji wa kutosha katika kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa uhakika?
Ni muhimu kutambua kuwa Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha shughuli za kijamii na kiuchumi; hivyo kukosekana kwa maji kunagusa moja kwa moja ustawi na maendeleo ya wananchi.
Wito wangu kwa mamlaka husika ni kwamba suala la maji halipaswi kuendeshwa kwa ubashiri. Linahitaji uwajibikaji wa dhati, mipango endelevu, na utekelezaji wa mikakati thabiti itakayotoa suluhu ya kudumu sio propaganda au ahadi zisizotekelezeka.
KIBAHA - PWANI, WENYE MADOZA WANANUNUA MAJI DAWASA KWENDA KUWAUZIA WANANCHI
Maeneo ya Kibaha Mkoani Pwani mitaa mingi haina maji ya DAWASA, hali inayowafanya Wananchi kununua kwenye madoza kwa gharama kubwa.
Wananchi wanalazimika kutumia Bodaboda kununua maji, wale wanaotaka kununua doza gharama zake ni kama nilivyosema hapo juu kuanzia Sh elfu 20 hadi 30 kwa dumu moja, jambo ambalo ni gumu kulimudu kwa Watanzani wengi wenye kipato cha chini.
Ajabu ni kuwa wanunuaji wa maji hayo wao wananunua kwenye Ofisi ya DAWASA, kwa bei ndogo ya isiyozidi Sh 3,000 kwa Tenki la Lita 1,000, lakini haohao DAWASA wanadai mitambo yao haina nguvu kusukuma maji kwenda kwa Wananchi wote waliounganishiwa huduma Kibaha.