Faana
JF-Expert Member
- Dec 12, 2011
- 38,657
- 44,759
Makongoro ni mwanajeshi wa akiba.
Alipigana vita vya Kagera!
Makongoro: Lowassa sikumuona Vita ya Kagera, Labda alikuja baada ya vita kuburudisha wanajeshi
CHARLES Makongoro Nyerere (CMN) ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliotangaza nia ya kutaka kuchaguliwa kuwania urais kupitia chama hicho mwaka huu. Raia Mwema lilifanya naye mahojiano wiki hii nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Endelea -RAIA MWEMA: Kwanini wana CCM wanatakiwa wakuchague wewe...
-RAIA MWEMA: Ni kweli kwamba baba yako, Mwalimu Julius Nyerere, hakujua kwamba uko vitani Uganda wakati wa Vita ya Kagera hadi baada ya vita kumalizika?
MAKONGORO: Ni kweli. Unajua mimi nilikwenda vitani nikiwa na umri wa miaka 18 tu ambao ndiyo ulikuwa umri mdogo zaidi kuruhusiwa kwenda vitani wakati huo.
Wakati vita inaanza mimi nilikuwa kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye Operesheni iliyojulikana kama Chakaza. Wale waliokuwa JKT walipatiwa mafunzo kidogo na kisha kupelekwa vitani.
Mimi pia nikaenda lakini sikumwambia baba. Ulikuwa ni uamuzi wangu binafsi. Kuna kaka zangu walikuwa jeshini tayari wakati huo lakini mimi nilikuwa mdogo sana.
Baba alikuwa na mambo mengi ya kufanya wakati wa vita na nadhani alijua naendelea na JKT. Kwa bahati nzuri pale nyumbani Msasani kulikuwa na simu na baada ya vita askari tulikuwa tukirusiwa kupiga simu nyumbani.
Sasa nikaanza utaratibu wa kupiga simu nyumbani mara kwa mara kila ilipofika saa kumi jioni. Baba alikuwa na utaratibu wa kurudi nyumbani saa tisa na akirudi moja kwa moja anakwenda mezani ale chakula.
Baada ya muda akabaini kuwa kila saa kumi wadogo zangu wakisikia tu simu wanakimbilia ilipo kwenda kusikiliza. Siku moja akawauliza, mbona mnakimbilia simu kila inapofika saa kumi na saa nyingine hamkimbilii?
Ndiyo wakamwambia tunaongea na kaka Mako (Makongoro). Akashangaa, akawaambia mnaongea naye kutoka wapi? Wakamwambia yuko Uganda. Nalisikia alishtuka sana na moja kwa moja akaja kwenye simu.
Mara nikasikia sauti ya Mwalimu ikiuliza Uko wapi Makongoro? Nikamwambia niko vitani Uganda? Akaniuliza uliendajeendaje? Nikamuuliza kwani vijana wenzangu kama mimi waliendajeendaje?
Basi, nikasikia anapumua na akaanza kuniuliza kuhusu habari za Uganda na mambo mengine. Nilikuwa sijawasiliana na baba yangu kwa muda wa miaka miwili tangu kuanza kwa vita.
-RAIA MWEMA: Mmoja wa washindani wako kwenye kinyanganyiro hiki cha kuwania urais, Edward Lowassa, amewahi kuhadithia namna alivyoshuhudia watu wakifa vitani wakati wa vita hiyo. Je, mliwahi kukutana mkiwa Uganda?
MAKONGORO: Sikumbuki kukutana na Lowassa wakati wa Vita ya Uganda. Lakini kulikuwa na askari wengi na inawezekana nilipokuwa mimi yeye hakuwepo. Siwezi kujua askari wote waliopigana vita ile.
Baada ya vita kumalizika, wasanii wengi kama vile Zahir Ally Zorro walikuja Uganda kututumbuiza lakini Lowassa pia sikumuona. Nasikia yeye alisomea sanaa Chuo Kikuu labda alikuja wakati huo lakini pia sikumuona.
Zorro na marehemu Kapteni John Komba niliwaona wakati ule. Lakini Lowassa sikumbuki kumuona. Labda alipigana mji mwingine au alikuja na wasanii kutumbuiza baada ya vita, lakini mimi sikumbuki kumuona.
-RAIA MWEMA: Washindani wako wanadai kuwa wewe hufai kupewa urais kwa sababu ni mlevi na unapenda kunywa pombe. Unazungumziaje shutuma hizi?