Hii article pia inaweza kuchangia katika mjadala huu
Ufisadi, rushwa kikwazo cha maisha bora
Dauson Harold
Tanzania Daima
JUZI kambi ya upinzani katika mkutano wao mkubwa wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga, Dar es Salaam, walitoa orodha ya majina ya vigogo wanaodaiwa kujihusisha na rushwa na ufisadi wakati walipokabidhiwa dhamana ya uongozi.
Sitaki kutaja majina wala kujadili kwa undani suala hilo, lakini jambo lililo wazi na ambalo nataka kulijadili katika makala hii ni suala la rushwa, ufisadi na dhana nzima ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Athari za rushwa na ufisadi katika serikali yoyote ile ni kikwazo kwa maendeleo na hata hapa nchini kadiri siku zinavyozidi kwenda, dhana ya maisha bora kwa kila Mtanzania inazidi kuwa ndoto kutokana na ukali wa maisha kuzidi kuongezeka kila kukicha.
Kila mara nawaza na kuwazua juu ya kauli aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete wakati anaingia madarakani. Nafikiria kama itawezekana, maana kila siku wananchi wanakosa usingizi kutokana na ugumu wa maisha.
Tukiangalia mfumuko wa bei kwa bidhaa mbalimbali, ni wazi kuwa ukali wa maisha kwa Mtanzania wa kawaida unaongezeka mara dufu hasa baada ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha, sote tunaona jinsi mambo yanavyozidi kuwa magumu.
Ongezeko la bei ya mafuta ni jambo linalofanya wananchi kuhoji, lakini kutokana na uchumi wa nchi kukua kwa kasi ndogo na kupanda kwa gharama za usafirishaji ni wazi kuwa hali ya kipato kwa walalahoi itashuka.
Tukiangalia ongezeko hilo tunazidi kuona jinsi linavyotuathiri wengi, kwani hata Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeruhusu kupanda kwa bei ya nauli kwa asilimia 50, imekuwa mwiba mwingine kwetu wa kipato cha chini.
Tukiangalia mfumuko wa bei ya vitu mbalimbali, tunaona jinsi Watanzania wanavyopoteza ndoto za maisha bora, kwani hii inaonyesha wazi kuwa haijulikani ni lini maisha hayo yatakuwa bora.
Wakati bei za vyakula na bidhaa mbalimbali zinakuwa juu, tunanona Mtanzania huyo kipato chake bado ni kidogo na hakiwezi kumudu gharama za maisha ya kila siku, sasa hapa maisha bora kwa kila Mtanzania yanatoka wapi?
Tunaona maandamano ya wafanyakazi, lengo lao ni kudai nyongeza ya mishahara lakini bado maandamano hayo hayajaleta mafanikio yoyote.
Masuala ambayo yanahitaji kupewa kipaumble ni pamoja na nyongeza ya mishahara ambayo itakidhi mahitaji ya wafanyakazi katika sekta binafsi na wafanyakazi serikalini.
Kutokuwepo kwa mishahara mizuri kimekuwa chanzo kikubwa cha rushwa katika taasisi za umma na binafsi kutokana na mishahara midogo isiyokidhi mahitaji ya mfanyakazi.
Wanachi wenye kipato kidogo wanashindwa kupeleka watoto shule kutoka na gharama zinazohitajika ili mtoto apate elimu ambayo iitamsaidia kuendesha maisha yake na kuondokana na ujinga.
Kwani katika taifa letu maadui wakubwa ni ujinga, maradhi na umaskini, ambapo sasa zaidi ya miaka 45 ya uhuru bado taifa linagubikwa na vitendo hivyo, ambapo watu hawana elimu, maradhi ni mengi na umaskini wa kipato kwa watu walio wengi ni duni.
Tungeona wakati bidhaa zinazidi kupanda na mishahara nayo ingeongezwa ili kukidhi gharama za kuendesha maisha, kama hatufanya hivyo, unafikiri rushwa itakwisha? Unafikiri maisha bora yatapatikana? Tutakuwa tukijidanganya kupambana na rushwa wakati bado kipato ni kidogo.
Tunaona jinsi Watanzania wa kipato cha chini wanavyoishi maisha ya shida, ambayo hata kupata mlo mmoja kwa siku ni ndoto, isipokuwa watu wenye kipato cha juu ndio wanaoweza kuishi maisha mazuri.
Tunaona hata watoto wa watu wenye kipato kikubwa katika nchi yetu ndio wanaosoma katika shule za gharama kubwa, lakini mtoto wa maskini anasoma katika shule zisizokuwa na mahitaji muhimu kwa wanafunzi kama ukosefu wa vitabu, walimu wa kutosha na wanafunzi bado wanaendelea kukaa chini.
Tunaona jinsi vijana wengi wasio na ajira na hata wale waliobahatika kupata ajira, mishahara yao ni midogo, kiasi ambacho hakiwezi kumudu hata kiwango cha mahitaji yao muhimu.
Tukiangalia maisha ya Watanzania wengi waishio mijini na vijijini bado ni duni, pamoja na Rais Jakaya Kikwete kutoa fedha za mikopo kukopesha watu wa kipato cha chini lakini bado hawajafaidika kwa mikopo hiyo.
Pamoja na fedha hizo kutolewa maarufu kama mabilioni ya Kikwete, bado fedha hizo hazikuwafikia walengwa na wengi waliishia kupewa ahadi ambazo kupata fedha hizo kwao zimekuwa ni ndoto.
Serikali ikitaka wananchi wawe na maisha bora kwa kila Mtanzania, lazima ihakikishe Watanzania wengi wanapata elimu ya kutosha, haisaini mikataba mibovu, lazima iwape wanachi kipaumbele katika kuwekeza hapa nchini, na kuongeza uzalishaji viwandani ambao utasaidia wananchi wengi kupata ajira na kuhakikisha wanapata masilahi mazuri.
Ili tufanikiwe, lazima tuwe na uongozi mzuri katika sekta zote za nchi yetu, tulinde rasilimali zetu ili ziweze kuwasadia Watanzania kupambana na rushwa na ufisadi, na tukiweza hilo, dhana ya maisha bora kwa kila Mtanzania, inawezekana.