1 Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo, akatoka Galilaya akafika mipaka ya Uyahudi, ng’ambo ya Yordani.
2 Makutano mengi wakamfuata, akawaponya huko.
3 Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?
-----------
Hapa tunaona swali la mtego. Na swali liko wazi, ni halali kumwacha mke kwa kila sababu?
4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,
5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?
6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
-----------
Majibu ya Yesu kwa hili swali yako wazi kabisa. Mungu aliumba mume na mke (kwa hiyo ushoga na usagaji hauwezi kuwa ndoa). Tena akasema wakiisha kuoana sio wawili bali mwili mmoja. Na anamalizia na kusema alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.
Yesu anaweka nukta, kamaliza kujibu swali lao kwa ukamilifu.
7 Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
-----------
Kwa sababu lengo ilikuwa kumtega, wanataka kumgombanisha na Musa ili watu wamwone mzushi. Maana watu walijua Musa ni nabii, na walikuwa wakimfuata Yesu kama mtu aliyetumwa na Mungu. Kwa hiyo kimsingi wanamhoji, kama wewe unatoka kwa Mungu na unasema hakuna talaka, basi mbona Musa, amabaye kila mtu anajua ni nabii akaturuamuru kutoa talaka? Huoni kama unapingana na Musa? Kumbuka lengo ni kumtega na sio kwamba hawajaelewa jibu!
8 Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.
------------
Anawajibu kuwa design ya Mungu ya ndoa ni maisha. Musa aliwapa ruhusa kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Yesu essentially anawashtaki hawa watu kwa Musa. Kwa wanaojua Biblia wanajua wana wa Israeli wana historia ya shingo ngumu. Walimtia presha Haruni mpaka akatengeneza mungu ndama wakati Musa kachelewa kurudi wakijua amekufa. Walifanya Musa akakosea mara kadhaa na mara ya mwisho ikamkosti kutoiingia Kanaani. Yesu kimsingi anawaambia "Wakaidi ninyi, mlisababisha Musa kuwapa hii amri kwa sababu mlikuwa jeuri, ila mpango wa Mungu sio huo".
Hawakubisha kwenye hili, Na ndipo unakuja mstari ambao kwa maoni yangu umetumika vibaya kuhalalisha iliyo haramu!
9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.
-------------
Biblia iko wazi kwanza kinachoongelewa hapa ni Uasherati ndio sababu ya kutenganishwa na sio uzinzi. Lakini pili itabidi uamini Yesu anajichanganya hapa maana keshasema mstari wa 4-6 kuwa ndoa ni maisha. Mungu hajichanganyi wala hajipingi. Wengine hukimbilia kusema maandiko ya asili ya Kiyunani yanasema blah blah. Wakasome Biography za Translators wa KJV halafu wajipime kama wanadhani wanajua Neno sahihi lilikuwa Uzinzi na sio uasherati. Kimsingi hapa at best hapako clear na at worst hapahusiani na wanandoa waliooana.
Kupotezea maandiko ambayo yako wazi na kujificha kwenye kichaka cha neno moja ni hatari sana kwa Mkristo!
10 Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.
--------------
Huu ni mstari ambao huwa hatuutafakari. Kama mke au mume akifumaniwa anapewa talaka inaishia hapo kwa nini wanafunzi wake wakasema hivi? Huu mstari unaleta maana tu kama Yesu alimaanisha hata ukifumania ni wako huyo. Vinginevyo mtu anisaidie kwa nini waseme hivi na ninaweza kuacha na kuopoa mwingine?
Kwa hiyo kwangu, maandiko haya na ukiongezea na 1 Wakorintho 7 ni definitive kwamba hakuna talaka katika Ukristo. Na Yeyote anayetoa talaka anakuwa anachukua nafasi ya Mungu ya kujaribu kutenganisha. Hii ni kufuru na ninaamini haitakiwi kufanyika!