Hao vijana wa wakati ule wanatoka maneo tofauti nadhani siyo vyema kuangalia majina yao na kuwajadili kama Waislam maana hata wanajeshi waliyota kumpindua Mwalimu Nyerere walikuwa na majina ya Kikristo lakini tuwajadili kama Watanzania siyo dini zao.
Takupa hiki kisa cha watekaji ndege kiduchu.
Baada ya maagano na ndugu, jamaa na marafiki, abiria walipanda katika ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania iliyokuwa na jina la Kilimanjaro, Boeing 737, kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Ijumaa ya Februari 26, 1982, saa 11 jioni.Uwanja wa ndege wa Mwanza ulikuwa na sifa mbaya kwa sababu haukuwa na usalama kiasi kwamba baadhi ya marubani walikuwa wakiutaja kama ‘kituo cha basi.’Makundi yaliyokuwa uwanjani hapo yalikuwa ya kawaida kama ya siku zote kwa wasafiri wa kwenda Dar es Salaam. Wasafiri wengi walikuwa ni Wahindi, Waarabu na Waafrika wachache. Ingawa mambo yote yalionekana kuwa ya kawaida, jambo dogo liliifanya safari hiyo isiwe ya kawaida.
Ndege ya Kilimanjaro ilipaa angani kutoka uwanjani hapo saa 11.20 jioni ya siku hiyo kwa kile kilichotazamiwa kuwa ni safari ya dakika 90 - maili 500, kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam.Lakini ikageuka kuwa safari ya juma zima - maili 9,500 - na kwa wakati mwingi abiria wa ndege wakisafiri ‘chini ya mtutu wa bunduki’ kabla ya kuwasili Dar es Salaam.Dakika tano tu baada ya ndege kupaa angani, vijana wanne walisimama ghafla kwa wakati mmoja. Mmoja wao alijipenyeza ghafla katika chumba cha rubani, halafu akaelekeza ‘bastola’ yake kwenye kichwa cha mmoja wa marubani wa ndege hiyo, Kapteni Deo Mazula, na kumtaka awapeleke kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.
Wakati huo huo, watekaji nyara wengine, huku wakipunga ‘bastola’ zilizotengenezwa kwa vigogo vya miti na ‘mabomu’ ya kutupwa kwa mkono, waliwatangazia abiria kuwa wao ni viongozi wa ‘Vijana wa Harakati za Mapinduzi Tanzania’ na kwamba shabaha yao ni “kuhakikisha kuwa Rais Julius Nyerere anajiuzulu.”Wakati hayo yakitokea, Rais wa Tanzania waliyemtaka ajiuzulu, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa Ikulu mjini Dar es Salaam akijiandaa kurudi nyumbani baada ya kupokea risala kutoka kwa Chipukizi nchini waliomwahidi kuwa “Tutaendelea kuwa watiifu, wakakamavu na wenye bidii kwa kuwa tunafahamu mchango wetu unahitajika sana katika ujenzi wa nchi.”
Mpaka wakati anaondoka kwenda nyumbani kwake, Msasani, akiwa amefurahishwa na risala aliyosomewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chipukizi, Frank Uhahula (15) wa darasa la saba katika Sule ya Mingi ya Tumbi, Kibaha katika mkoa wa Pwani, Mwalimu Nyerere hakuwa amejua kilichotokea upande mwingine wa nchi -Mwanza.Watekaji nyara hao waliwaamuru abiria wote wakae kimya kwenye viti vyao na kufumba macho yao na, kwa sababu ambazo hazikujulikana lakini za kustaajabisha, waliwalazimisha watumishi kuzima viyoyozi vya ndege. Wakati hali ya hewa katika ndege hiyo ilipoanza kuwa nzito na kukaribia kutovumilika tena, ndege hiyo ilitua mjini Nairobi kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta.
Lakini katika kipindi cha dakika kadhaa baadaye, Rais Nyerere alipewa taarifa za kutekwa kwa ndege hiyo na kuambiwa kwamba tayari ilishatua Nairobi, Kenya. Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, John Samuel Malecela, ambaye aliteuliwa rasmi kushughulikia utekaji huo, alitumwa kwenda Nairobi kushughulikia tatizo hilo. Mwalimu Nyerere alitaka kuwa na hakika kwamba Serikali ya Kenya haingeruhusu ndege hiyo iondoke Nairobi.Wakati huo huo polisi wa Kenya wakifunga uwanja wa Ndege wa Kenyatta, na wanajeshi walisambazwa uwanjani hapo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Robert Ouko, alikuwa uwanjani hapo akitokea Addis Ababa, Ethiopia, wakati ndege ya Tanzania ilipotua.Alipopewa habari za yaliyotokea, Dk Ouko hakusita, alikwenda kwenye chumba cha kuongozea ndege kujaribu kushughulikia jambo hilo.
Hii habari ndefu nadhani tawachosha tunaendelea muda mwingine.