Kambi ya kampeni ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe anayewania kutetea kiti chake, imeripotiwa kudhibiti kura zaidi ya 700 za wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho huku jumla ya wajumbe wote wanatarajiwa kufikia 1328.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika kesho, tarehe 21 Januari 2025, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu ya kampeni ya Mbowe, wajumbe hao halali na wenye sifa za kupiga kura wamewekwa katika kambi mbalimbali jijini Dar es Salaam, zikiwemo maeneo ya Ubungo, Manzese, na Buguruni.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha uaminifu wa wajumbe hao katika kumpigia kura mgombea huyo.
Mmoja wa wajumbe walioko kwenye moja ya kambi hizo ameithibitishia Jambo TV kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwamba wapo chini ya uangalizi maalum, na hawaruhusiwi kutoka nje ya maeneo waliyopo.
Ameeleza kuwa ulinzi umeimarishwa na unasimamiwa na moja ya kampuni za ulinzi jijini Dar es Salaam.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa huduma zote, ikiwemo chakula, malazi, na vinywaji, zinatolewa bure kwa wajumbe walioko kambini.
Aidha, wajumbe hao wameahidiwa zawadi maalum endapo Freeman Mbowe atashinda uchaguzi huo.
Usiku wa leo, Freeman Mbowe anatarajiwa kutembelea kambi hizo na kuzungumza na wajumbe wake katika hatua ya mwisho ya kampeni.
Jambo TV imesambaza waandishi wake katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchaguzi huu wa CHADEMA, ambao umekuwa gumzo nchini.