Nchi yetu ilirejea kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya kuwa kwenye mfumo wa chama kimoja kwa kipindi kirefu baada ya kupata Uhuru wetu toka kwa mkoloni mwaka 1961.
Tuliingia kwenye uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, na tukaendelea kuingia kwenye uchaguzi mkuu kila baada ya miaka 5.
Lengo kuu la kuwa na mfumo wa vyama vingi ni kwa serikali iliyoko madarakani kupokea mawazo mbadala toka kwa vyama vya upinzani yenye maslahi mapana kwa Taifa letu.
Ingawa katika kipindi chote hicho wapinzani wamekuwa katika mazingira magumu kutokana na nchi kutokuwa na uwanja sawa, kutokana nchi yetu kuendelea kuwa na Katiba ya nchi ya mfumo wa chama kimoja.
Ingawa Katiba hiyo imeendelea kuwekwa viraka ili angalau kukidhi mfumo wa sasa wa mfumo wa vyama vingi, lakini bado mfumo wa utawala wa nchi umeendelea kubaki kama mfumo wa chama kimoja.
Ingawa kwenye utawala wa awamu za 3 na 4 tuliona utawala angalau kwa kiasi fulani ni kama unakubaliana na mfumo wa vyama vingi, hali imekuwa tofauti kwenye utawala wa awamu ya 5, ambao unaonyesha viashiria vingi kuwa unatamani turejee kwenye mfumo wa chama kimoja.
Nitataja mambo machache yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 5 ambayo yanaashiria dalili za kuonyesha kuwa serikali ya awamu ya 5 inatamani nchi yetu irejee kwenye mfumo wa chama kimoja.
1. Mara tu baada ya kuingia madarakani serikali ya awamu ya 5 ikapiga stop matangazo live ya Bunge kwa kisingizio kuwa hizo ni nyakati za kazi, kwa hiyo waTZ wanatakiwa kuwa makazini muda huo.
Hata hivyo imethibitika kuwa sababu hiyo iliyotolewa na watawala siyo ya kweli, kwa kuwa tumeshuhudia matangazo live wakati huo huo wa kazi kwenye ziara za Mwenyekiti wa CCM Taifa kila anapofanya ziara ya sehemu mbalimbali nchini.
Sasa kama kweli sababu ilikuwa watu wasiangalie Bunge live wakati wa kazi mbona wananchi hao hao ni kama wanalazamishwa kumwangalia Mwenyekiti wa CCM Taifa kila anapotoa hotuba zake mbalimbali nchini?
Tumeshuhudia Rais wetu akipiga marufuku mikutano na maandamano yoyote ya kisiasa hadi mwaka 2020. Lakini hata hivyo tumeshuhudia yeye Mwenyekiti wa CCM wa Taifa akifanya shughuli mbalimbali za kisiasa sehemu mbalimbali nchini kwa mwamvuli wa shughuli za kiserikali.
Tumeshuhudia pia maandamano ya wananchi wanaodaiwa wanaridhika sana na uongozi wa Rais Magufuli wanaopendekeza badala ya kuongoza kwa mihula 2 ya miaka 10 kama anavyotakiwa kwa mujibu wa Katiba, badala yake awe Rais wetu wa maisha!
2. Tumeshuhudia Bunge letu lenye wabunge wengi wa CCM, likifanya juhudi kubwa la kuwatimua Bungeni wabunge wengi wa upinzani wenye kutoa hoja nzito za kuibana serikali yetu.
Mfano halisi ni hivi sasa ambapo wabunge Halima Mdee wa Kawe na Esther Bulaya wa Bunda mjini wakifungiwa kutohudhuria vikao vya Bunge hadi mwakani kwa kile kilichodaiwa na wabunge hao wa CCM kuwa wabunge hao waliofungiwa ni watukutu.
Hata hivyo tumeshuhudia baadhi ya wabunge wa CCM ambao wamekuwa wakitumia lugha za maudhi na hadi kuwatukana wabunge wenzao wa upinzani kama vile kuwaita wezi, lakini hatujaona Bunge hilo kuwachukulia hatua wabunge hao, jambo linaloonyesha kuwa kiti cha Spika ambacho kinakaliwa na wabunge wa CCM kinaonyesha upendeleo wa wazi kwa wabunge wa CCM.
3. Tumeshuhudia sehemu mbalimbali nchini hawa wateule wa Rais, hususani maDC na naRC wakiwanyanyasa wawakilishi wa wananchi wa vyama vya upinzani, hususani madiwani, wabunge na mameya kwa kuwaweka ndani pasipo sababu za misingi kwa kile wanachodai kuwa wanazo kisheria saa 'zao' 48 ambazo wanaweza kuzitumia pale wanapojisikia kumweka ndani mkazi yeyote aliyeko kwenye eneo lake ambaye ataona ametoa lugha ya uchochezi au amefanya vitendo vyovyote vyenye kuashiria uvunjifu wa amani wa eneo lake.
Hata hivyo tumeshudia wanaowekwa ndani na hao maDC na maRC ni watu wa upande mmoja pekee ambao ni viongozi wa vyama vya upinzani ambao wanatoa kauli za kuikosoa serikali.
Kama nilivyoeleza awali kuwa lengo la kuwa na mfumo wa vyama vingi nchini ni serikali kupata mawazo mbadala kutoka kwenye vyama vya upinzani yenye lengo la kuliendeleza Taifa letu kimaendeleo, sasa inapotokea serikali iliyoko madarakani haitaki kabisa kupokea mawazo mbadala,badala yake inataka kusikia maneno ya kusifiwa peke yake ni vyema serkali ikaandaa muswada na kuupeleka Bungeni ili nchi hii irejee kwenye mfumo wa chama kimoja ili kuwapunguzia mateso viongozi na vyama vya siasa vya upinzani na wananchi wengine wanaoikosoa serikali ambao kwenye hii serikali ya awamu ya 5 wanahesabika kama wahaini wa nchi hii.