LIPUMBA: Profesa wa uchumi anayepanda kisiasa kwa kasi
UKIMPELEKA katika mada za kiuchumi, umemfikisha nyumbani, anateremka bila nukta, kama hukumtia kamba na kumburura atakupoteza njiani. Lakini anayo sifa yake moja kuu nayo ni ya 'ualimu,' yuko tayari kurudia somo kwa mwanafunzi wake ili alielewe, akikuona kama dhana za kiuchumi zinakupiga chenga ataanza kukufafanulia dhana moja baada ya nyingine, taratibu bila haraka wala wasiwasi.
Huyu ni gwiji la uchumi nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Katika uhai wake hakutarajii kwamba siku moja atakuja kuwa mwanasiasa, lakini hakuna mtu anayeijua hatima yake, ama nini kitamtokea kesho ama hata dakika moja baadaye.
"Ilikuwa kama ajali na mwanadamu, Julai 1995 nilikuja kutoa ushauri, wakati huo nilikuwa katika tume ya Profesa Elaina, tulikuja kutazama namna gani tunaweza kuboresha mahusiano ya Tanzania na wahisani, wakati ule waziri wa fedha alikuwa Jakaya Kikwete, tuliomba kukutana naye mara tatu na zote tulimkosa, kila tukienda hayupo, hivyo hatukukutana naye, hivyo tulikwenda kukutana na viongozi wa taasisi za fedha na hata viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, CUF kikiwa kimojawapo.
Wakati huo CUF nilikuwa nafahamiana na Maalim Seif Shariff Hamad tu kwa sababu tulikuwa chuo kikuu pamoja. Wakati huo jamaa wa CUF nao wakawa wanamtafuta mgombea, ndipo wakaniomba nikubali kuwa mgombea wao, wakati huo Augustine Mrema alikuwa moto, nikaamini kwamba nikiingia naweza kuubadilisha mwelekeo wa mjadala, sikutegemea kuwa nitashinda kwa kwa sababu nilikuwa sijulikani.
"Kwa hakika ingawa nilikuwa sijajikita katika siasa, lakini niliweza kuibua hoja za msingi za kimaendeleo na kukipa shida kidogo Chama cha Mapinduzi, niliweza kubadilisha mwelekeo wa majadiliano, tukawa kweli tunajadili mambo yanayowakera wananchi, midahalo ilikuwa mizito na ya kuvutia.
"Nilifahamu kwamba CUF ina nguvu sana Zanzibar na nilikuwa naamini kwamba itashinda Zanzibar, lakini huku Bara kilikuwa dhaifu sana, kwa hiyo ukiwa na chama ambacho kitakuwa na nguvu Zanzibar, lakini Bara dhaifu, na kikachukua serikali, hali ya mahusiano yanaweza yakawa ya wasiwasi, kwamba ukitaka uendeleze Muungano, hata kama chama kitashinda upande mmoja wa Muungano, lakini pia kiwe kinakubalika upande wa pili, kwa hiyo nikaona nikiingia katika CUF nitaweza kukiinua kidogo na kukifanya kikubalike Bara.
"Nilifahamu kuwa sitaweza kushinda katika uchaguzi ule, na nilirudia tena mwaka 2000 ili kujiweka vizuri zaidi, katika uchaguzi wa mwaka huu, sina wasiwasi, Watanzania wananielewa na wanakielewa chama cha CUF, tumejikita vizuri mijini na hata vijijini," anaelezea Profesa Lipumba.
Kasi ya Profesa Lipumba kupanda katika ulingo wa siasa ni kuwa kutoka 1995 hadi 2000 alipanda kwa asilimia karibu 300, kwa kuwa mwaka 1995 alipata asilimia 6.4 ya kura zilizopigwa na mwaka 2000 akapata asilimia 16.3 ya kura. Mwaka 1995 alikuwa mgombea wa tatu akitanguliwa na Rais Mkapa na Augustine Mrema wakati ule akiwa NCCR-Mageuzi. Lakini mwaka 2000 alikuwa wa pili kwa kuwa nyuma ya Rais Mkapa. Mwaka huu matumaini yake ni makubwa zaidi.
Profesa Lipumba anasema amejifunza mengi katika siasa ambayo hakuweza kujifunza katika vuo vya elimu ya juu.
"Kwa hakika mimi nilikuwa siijui Tanzania, sasa kushiriki kwangu katika siasa kumeniwezesha kuijua Tanzania kuliko nilivyokuwa nikiijua, hasa ule ukatili wa vyombo vya dola nilikuwa siujui, sikufikiria kama Tanzania tuko katika hatua ya ukatili wa kukithiri dhidi ya binadamu, kwa mfano unapokwenda vijijini unakuta watu wanakwambia kuwa wanalishwa samaki wabichi kwa nguvu kwa sababu wanaambiwa wakati walipovua waliharibu mazingira, wapo watu waliochomewa nyumba kwa sababu wanaambiwa eti wako karibu na hifadhi. Kwa mfano wakazi wa Ulanga mkoani Morogoro, hawa watu wameishi pale miaka nenda, miaka rudi, lakini leo wanaambiwa kuwa wameingia katika eneo la hifadhi. Vitendo vya ukatili kwa kutumia vyombo vya dola dhidi ya raia ni vingi na vinachukiza," anasema.
Anasema ingawa siasa imekuwa ndiyo sehemu kubwa ya maisha yake, lakini gharama za siasa ni kubwa, "Wale wanaotumia siasa kama kitegauchumi, hawajui siasa. Siasa za kweli hazina kipato, ukimwona mtu anategemea kutajirika kutokana na siasa, huyo ni tapeli wa kisiasa, mwanasiasa ni lazima awatumikie wananchi wananchi na furaha yake ni kule kuona wananchi wanapata maendeleo. Faraja ya mwanasiasa ni kujenga nchi na kamwe si kujitajirisha, " anasema.
Profesa Lipumba anasema wakati akiwa chuo kikuu cha Dar es salaam kama mhadhiri yeye pamoja na wenzake walikuwa wakiishauri sana serikali kuhusu masuala mbalimbali ya kuichumi." Tuliwashauri mambo mengi tu, lakini hawakuyazingatia," anasema.
Mwaka 1991 hadi 1993 alikuwa mshauri wa Rais Mambo ya Uchumi, wakati huo Rais alikuwa Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
"Niliondoka kwa makusudi katika nafasi ya ushauri baada ya kuona kwamba kutoa ushauri kwa serikali ya CCM ni sawa na kutwanga katika kinu chenye maji, kamwe hutaweza kuukoboa mtama ama mpunga unaoutwanga. Viongozi wa chama hicho wana tabia ya kudharau ushauri wa kitaalam hivyo mwishoni mwa mwaka 1993 nilikwenda kusomesha katika Chuo cha Williams kilichoko Massachusets, Marekani kwa muda wa miaka miwili." anasema.
Alipoingia katika siasa, haikuwa rahisi sana kwa Profesa Lipumba kwani ilibidi ayatolee mhanga maisha yake na ya familia yake. "Kabla ya kushiriki kikamilifu katika siasa nilikuwa napata kazi nyingi za kutoa ushauri wa kiuchumi, hivyo sikuwa na wasiwasi na mkate wangu wa kila siku, lakini hivi sasa sina nafasi ya kufanya kazi hizo, siasa inachukuwa muda wangu mwingi sana," anasema.
Kadhalika Profesa Lipumba ilibidi aache aache kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, hata kama hakupenda kufanya hivyo, lakini mazingira yalimlazimisha.
"Baada ya kumalizika uchaguzi mwaka 1995, nilirudi Chuo kufundisha, nikafundisha mwaka mzima wa masomo (1996), tulipokuwa na likizo ndefu nilimtaarifu mkuu wangu wa kazi katika kitengo cha uchumi kuwa nakwenda New York Marekani kushiriki katika mkutano wa kamti ya Umoja wa Mataifa ya kuangalia sera za maendeleo na uchumi ambayo mimi nilikuwa ni miongoni mwa wajumbe wake, kulikuwa na utaratibu wa kuwa kamti ya wataalam wa mambo ya uchumi, inatoa ushauri kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Lakini pia nikamwambia mkuu wangu wa kazi kuwa kwa kuwa nina likizo ndefu baada ya kumalizika kwa mkutano huo nitaendelea kubaki nchini Marekani."
"Bahati nzuri wakati nilipokuwa najiandaa kwenda huko, nilipata nafasi ya kufanya uhakiki wa taratibu za kifedha nchini Tanzania, kazi hiyo nilipewa na Benki ya Dunia na nikakubali, kazi hiyo ilipaswa ifanyike washington, hivyo nilipomaliza kazi zangu New York, nilikwenda Washington.
"Wakati huo tayari tulikuwa na mgogoro Zanzibar, nikiwa Washington nilikutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, jamaa wa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani wakaandika barua wakaileta nyumbani na kusema kwamba nilikuwa nawashawishi wahisani kuzuia misaada, ili Tanzania isipate misaada.
"Kadhalika nilikutana na Makamu wa Rais wa Africa, Mudave ambaye ni Mzimbabwe, yule bwana kwa bahati baadaye alihudhuria mkutano wa O.A.U uliofanyika Gabon, akakutana na Rais Benjamin Mkapa, yule bwana kwa nia nzuri tu akamwambia Rais Mkapa kuwa, "Kule Washington yuko Mtanzania Profesa Lipumba ambaye tunashirikiana naye vizuri.
"Rais aliporudi nchini aliuliza uongozi wa Chuo, imekuwaje Lipumba yuko Washington? Walipoangalia ruhusa yangu wakasema kwa taarifa waliyonayo ni kuwa mimi niko New York, hawana habari ya mimi kuwapo Washington, lakini wakati ule nilikuwa likizo, hivyo nilikuwa na uhuru wa kwenda ninakotaka. Hiyo ikawa balaa, ikabidi Chuo kiniandike barua kunitaka nijieleze niko wapi na kwanini nisichukuliwe hatua za kinidhamu.
"Nilipokuwa Washington, nilipata mwaliko kutoka World Institute of Economic Research, Helsinki Finland, niende nikafanye utafiti. Niliporudi chuo nikakuta zile barua.
Nikawajibu na kuwaelezea shughuli nilizokuwa nazifanya Marekani, kisha nikaomba wanipe likizo bila malipo ya miaka miwili ili niende Helsinki, majibu ya barua yangu ile yalipokuja yakanieleza kuwa nimefukuzwa Chuo Kikuu.
"Nilipomaliza miaka miwili Finland, nilirudi nyumbani na kuanzisha kiofisi changu kidogo cha ushauri wa kiuchumi na utafiti, nikawa napata kazi mbalimbali za utafiti. Nilipata kazi ya huko Harare, nikapata utafiti mwingine wa UNDP kuhusu maendeleo ya binadamu kwa kuzingatia maisha ya Watanzania, wakati nafanya vishughuli hivyo CUF wakaniomba niwe mshauri wao. "Wakati wa uchaguzi mdogo wa Temeke na Ubungo, CUF wakaniomba niwasaidie katika kampeni, tukafanya kampeni na kuwasha moto kweli kweli, sasa mambo yakawa yanakwenda vizuri, mwaka 1999 wakaniomba nigombee uenyekiti wa Chama Taifa baada ya Mzee Musobi Mageni kusema anastaafu, nilisita sana kwa sababu nilijua nikishaingia humo itakuwa ni shughuli itakayonimalizia muda wangu wote, lakini baada ya kuiangalia hali yenyewe ilivyo na msukumo wa kutoa changamoto ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa nchini, nilikubali kugombea na kuanzia hapo nikawa mwenyekiti wa Taifa wa CUF," anasema.
Profesa Lipumba anagombea nafasi ya urais kupitia CUF kwa mara ya tatu sasa, anasema siyo kama hakuna watu wengine wenye uwezo wa kugombea nafasi hiyo, lakini kwa bahati mbaya mwaka 2000 na hata mwaka huu hakuna aliyejitokeza ingawa nafasi ilikuwa wazi kwa yeyote.
Hata hivyo, anasema pamoja na kushindwa mara mbili kushika kiti cha urais, lakini ana imani kwamba mara hii mambo yatakuwa tofauti kwa sababu sasa anao uzoefu na wananchi wamechoshwa na utawala uliopo madarakani.
"Sisi tunatoa matumaini mapya kwa wananchi walio wengi, hivyo CUF ni chama badala na kwa kuwa watu wanataka kuona mabadiliko, nina imani kwamba matokeo ya uchaguzi ya mwaka huu yatakuwa tofauti sana na miaka iliyopita.
"Serikali iliyopo madarakani imewachosha wananchi, imewachosha kwa sababu ya ubadhirifu wa serikali, kwa mfano, kulikuwa na ulazima gani wa kununua ndege ya Rais wakati wananchi wanakufa njaa? Hiyo inaonyesha dhahiri kwamba serikali haijali! Isitoshegharama za kuiendesha hiyo ndege ni kubwa mno.
"Na hata kile kitendo cha kuuza nyumba za serikali kwa bei poa na kusema kwamba utajenga nyumba nyingine kwa haraka, hayo ni matumizi yasiyo ya lazima.
Profesa Lipumba amesema ikiwa chama chake kitafanikiwa kuingia madarakani kitapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi holela ya fedha za walipakodi na pia itaimarisha ukusanyaji wa kodi.
"Hivi sasa Tanzania inakusanya asilimia 13 tu ya pato la taifa, wakati Kenya inakusanya asilimia 23, ili uchumi ukue vizuri lengo linapaswa liwe ni kukusanya asilimia 20 ya pato la taifa kama kodi kwa viwango nafuu, lakini misamaha ya kodi isiwe mingi," anasema.
Profesa Lipumba ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu wa Mzee Haruna Lipumba wa Ilolangulu Tabora, Mzee Haruna ni miongoni mwa waasisi wa Chama Cha TANU mkoani Tabora na ndiye aliyekuwa miongoini mwa wenyeji wa Mkutano Mkuu wa kwanza wa TANU uliofanyika Tabora.
Kama walivyokuwa vijana wa miaka 70, Lipumba naye alikuwa mkereketwa mkubwa wa TANU, aliwahi kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975 hadi 1976.
Lipumba amemuoa Georgina Mtenga na kujaaliwa kuzaa na naye watoto wawili wa kike, Imani (13) na Lulu Aisha (9).
Pamoja na kutingwa na siasa na uchumi, Lipumba pia ni mpenzi wa mpira wa miguu "Mimi ni mpenzi mkubwa wa Simba Sports Club; na kuna wakati nilikuwa navutiwa sana na mpira wa Tanzania, lakini siku hizi unanivunja moyo, kama Rais Msaafu, Ali Hassan Mwinyi alivyosema kuwa; mpira wa Tanzania sasa umekuwa kama kichwa cha mwendawazimu, kila mwenye kiwembe chake aweza kukinyoa! "Bahati mbaya sana michezo imedharauliwa katika nchi hii, lakini ukweli ni kwamba inasaidia sana kukuza akili, mimi nikipata muda huwa nakwenda kufanya mazoezi ya viungo," anamaliza